Na: Frank Shija -
MAELEZO
Halmashauri nchini
zimeshauriwa kupunguza mlolongo katika mchakato wa ukusanyaji wa ushuru
mdogomdogo unaotokana na kutumia mfumo wa kutumia wazabuni badala yake kazi hiyo ifanywe na watendaji wa
Halmashauri husika.
Ushauri huo umetolewa
na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) George Boniphace Simbachawene katika mahojiano na mtangazaji wa
Kituo cha luninga cha ITV kupitia kipindi cha Dakika 45 hivi karibuni.
Simbachawene alisema
kuwa kumekuwa na kasumba ya Halmashauri nchini kutumia wazabuni katika
ukusanyaji wa ushuru jambo linalochangia kusababisha mianya ya ubadhirifu wa fedha
za umma.
“Mawakala wa
ukusanyaji ushuru wamekuwa wadanganyifu na mara zingine wamekuwa wakiwasumbua
wafanyabiashara ni vyema sasa Halmashauri nchini zikafikiria kutumia watendaji wake
katika zoezi zima la ukusanyaji ushuru,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa sambamba
na ukusanyaji wa ushuru kufanywa na watendaji wa Halmashauri husika aliagiza
fedha hizo kuhifadhiwa katika akaunti za halmashauri hizo.
Katika hatua nyingine
Waziri Simbachawene amewapongeza watumishi wa Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa kwa utendaji wao ambapo amesema umeanza kutia faraja.
Hata hivyo alitoa rai
kwa watumishi hao kuendelea kubadilika na anayeona hawezi kuendana na kasi ya
Serikali ya Awamu ya Tano ni vyema akapisha ili Watanzania wengine waweze
kuajiriwa.
No comments:
Post a Comment