Frank Mvungi- Maelezo
WAZIRI
wa wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi mkutano wa Kimataifa wa Ualbino
utakaofanyika mwezi Mei mwaka huu.
Hayo
yamesemwa na Afisa Mahusiano na habari wa Chama cha Albino Tanzania
(TAS), Josephat Torner wakati wa mkutano na waandishi wa Habari leo
jijini Dar es salaam.
Torner
alisema mkutano huo wa siku moja utafanyika katika hoteli ya Serena
Jijini Dar es salaam na utawahusisha washiriki toka mataifa mbalimbali
yakiwemo Nchi za Afrika Mashariki, Marekani, Nchi za Ulaya na Nchi za
Kusini mwa Afrika.
Alisema
moja ya matarajio ya mkutano huo ni kupata sauti ya pana ya Kimataifa
kuutaka Umoja wa Mataifa kuitangaza tarehe 4 mwezi Mei kuwa Siku ya
Kimataifa ya Ualbino.
Aliongeza
kuwa lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kutafakari vikwazo
vinavyosababisha tofauti ya umri wa kuishi kati ya watu wenye ulemavu na
watu wengine.
“Hii
inatokana na ukweli kwamba kwa Tanzania wastani wa umri wa kuishi kwa
watu wenye ualibino ni miaka 30 wakati kwa watu wengine ni miaka 60”2,
alisema Torner.
Alisema
sababu zinazochangia watu wenye ulemavu wa ualbino kuishi nusu ya umri
wa Watanzania wengine ni kukabiliwa na saratani ya ngozi.
Alitoa
wito kwa watu wote wenye ualbino,wazazi,walezi na wadau mbalimbali na
umma kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho haya.
Maadhimisho
ya Siku ya Albino yalianzishwa hapa nchini mwaka 2006 na tangu mwaka
huo yamekuwa yakileta hamasa katika nchi mbalimbali Duniani.
Kilele
cha maadhimisho hayo hapa nchini kinatarajiwa kuwa siku ya tarehe
4/5/2014 na kauli mbiu ikiwa ni Haki ya Afya,Haki ya Uhai.