Kwa niaba ya Msarifu wa Taasisi
Mhe. Benjamin William Mkapa, Bodi ya Wadhamini, Menejimenti na
wafanyakazi wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa tunatoa shukrani za
dhati kwa kuweza kufanikisha harambee ya kuchangia. Mradi wa Mkapa
Fellows, iliyofanyika jijini Mwanza siku ya Jumamosi, tarehe 23 Agosti
2014 katika ukumbi wa Hotel ya JB Belmont.
Harambee iliyohudhuriwa na wageni
karibia 230 iliongozwa na Waziri Mkuu wa Tanzania,Mhe Mizengo Pinda
ambae alikuwa mgeni rasmi akiambatana na Raisi mstaafu,Mhe. Benjamin W.
Mkapa pamoja na Mama Anna Mkapa.
Harambee hii iliyofanyika na
Taasisi ya Benjamin W. Mkapa ni ya mara ya kwanza kutekelezwa na Taasisi
nje ya Mkoa wa Dar Es Salaam. Kwa hatua za awali tuliamua kuanzia
katika Kanda ya Ziwa,na kuwashirikisha washikadau waliopo katika mikoa
sita (6) ya Kanda ya Ziwa. Harambee ilifanikiwa kukusanya kiasi cha Tshs
1.38billioni na hivyo kuvuka lengo lililowekwa la kukusanya kiasi cha
Tsh 500 millioni katika Kanda hiyo.
Kiasi kilichokusanywa kitatumika
kutekeleza mradi wa Mkapa Fellows unaoendeshwa na Taasisi ya Benjamin W.
Mkapa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Mradi huu wa Mkapa
Fellows unatekelezwa katika mizunguko miwili; ambapo mzunguko wa kwanza
ulianza Januari 2013 na utamalizika Desemba 2014 na ulifikia Halmashauri
sita (6) nchini za Sumbawanga vijijini, Kalambo, Nkasi, Msalala,
Kishapu na Biharamulo. Baadhi ya mafanikio ya mradi huu hadi leo, ni
pamoja na tumeshaajiri na kuwapeleka katika wilaya hizo 6 wataalam wa
afya 30 kati ya lengo la miaka mitano la watalaam 180, na pia ujenzi wa
vyumba vya upasuaji 9 kati ya 30 umeshakamilika, na ununuzi na uwekaji
wa vifaa vya kutolea huduma pia kukamilika. Fedha za utekelezaji wa
mzunguko huu wa kwanza zilifanikiwa kupatikana kupitia mfadhili wa
Serikali ya Ireland na wafanyabiashara zaidi ya 50, wakiwemo pia Kampuni
ya African Barrick Gold.
Mzunguko wa pili wa huu mradi
utaanza Januari 2015 mpaka Desemba 2017 na utafikia Halmashauri 9 za
Shinyanga vijijini, Kahama,Meatu, Bariadi, Itilima, Busega, Maswa,,Chake
Pemba na Mkoa wa Kati Unguja.
Kwa muhtasari fedha hizi
zilizokusanywa katika Harambee hii ya Kanda ya Ziwa,zitasaidia kuchangia
katika bajeti inayohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi
kuanziaJanuari 2015. Hali kadhalika mradi wa Fellows ambao una bajeti ya
Tshs. 15bilioni kwa miaka 15, ilikuwa bado na pengo la Tshs. 10billion,
hivyo kwa kupata mchango wa kutoka Kanda ya Ziwa wa Tshs.
1.3billioni,sasa litapunguza hilo pengo hadi Tshs. 8.7 bilioni. Wakati
huo huoTaasisi itaendelea na mikakati mingine mbalimbali ya kutafuta
fedha za kutekeleza mradi huu hadi mwaka 2017.
Kwa nafasi ya pekee, Taasisi ya
Benjamin W. Mkapa HIV/AIDS (BMAF) inapenda kutoa shukrani zake kwa
Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda kwa kukubali mwaliko wa kuwa
mgenirasmi katika harambee hiyo. Pia shukrani zinatolewa kwa mawaziri na
manaibu mawaziri na viongozi mbalimbali ambao walituunga mkono katika
Harambee hii.
Taasisi inatoa shukrani zake kwa
Wakuu wa mikoa wa Kanda ya Ziwa kwa kukubali kwao kuongoza mikoa na
Halmashauri zilizopo chini yao, katika maandalizi na kushiriki
kikamilifu katika harambee hii. Aidha Taasisi ya BMAF inatoa shukrani za
dhati kwa wafanyabiashara wote wa Kanda ya Ziwa kwa kuweza kuchangia
katika mradi huu. Mafanikio haya ni mfano mzuri wa Public-Private
Partnership (ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya
umma/serikali), ambapo inaweza kuleta mabadiliko katika kuimarisha
huduma za afya nchini. Moyo na uaminifu waliotuonyesha ni mkubwa na tuna
Imani tutaendelea kushirikiana katika kuleta maendeleo ya sekta ya
afya, hususan katika maeneo ya vijijini.
Shukrani za pekee ziwaendee
wadhamini wetu waliofadhili hafla ya chakula cha jioni cha harambee,
ambao ni Anglo-Gold Ashanti, NSSF, Bank M, PPF,NHIF, Nyanza Bottling Co,
Montage Limited, JB Belmont, Afya Radio,Mwananchi Communication, Jembe
ni Jembe, Isamilo Hotel, Clouds FM naSahara Media Group.
Imetolewa na:
Dkt Ellen Mkondya-Senkoro
Afisa Mtendaji Mkuu
Taasisi ya Benjamin William Mkapa
S. L. P 76274, Dar es Salaam