Na, Lucas Mboje - Jeshi la Magereza,
SIFA ZA MFUNGWA WA PAROLE
Sheria
ya Bodi za Parole Sura 400 ya mwaka 2002 na Kanuni zake za mwaka 1997
inaainisha kuwa mfungwa anayetumikia kifungo cha kuanzia miaka minne (4)
na kuendelea anastahili kunufaika na mpango wa Parole kama atakuwa na
sifa zifuatazo:-
i) Asiwe amehukumiwa kifungo cha maisha;
ii)
Asiwe ni mfungwa anayetumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi wa
kutumia silaha, madawa ya kulevya na makosa yanayohusiana na kujamiiana;
iii) Asiwe ni mfungwa ambaye kifungo chake kimebatilishwa kutoka kwenye kifungo cha kunyongwa;
iv) Awe anatumikia kifungo kisichopungua miaka minne (4) au zaidi na awe ametumikia 1/3 ya kifungo chake;
v) Awe ameonesha tabia na mwenendo mzuri kwa muda wote aliokaa gerezani na;
vi)
Asiwe na pingamizi la kimahakama la kukataliwa kunufaika na utaratibu
wa Parole chini ya Kifungu cha 67 cha Sheria ya makosa ya Jinai.
UAMUZI WA BODI ZA PAROLE UNAVYOFANYIKA HAPA NCHINI
Kimsingi
mfungwa anapoingia gerezani kwa mara ya kwanza hujulishwa kuhusu haki
zake ikiwemo haki ya kuingizwa kwenye mpango wa Parole kama ana sifa
kulingana na kosa lake na muda wa kifungo chake gerezani.
Mfungwa
mwenye sifa ya kuingizwa kwenye mchakato wa Parole anapotimiza 1/3 ya
kifungo chake, Afisa Parole hukusanya taarifa mbalimbali zinazomuwezesha
kujadiliwa katika Bodi za Parole; Taarifa hizo ni maoni kutoka kwa
wazazi/ndugu zake, maoni ya mwathirika wa uhalifu, nakala ya hukumu,
hati ya kifungo, maoni kutoka uongozi wa kijiji anachotarajia kwenda
kuishi na maoni/taarifa kutoka Kituo cha Polisi kilichomkamata na pia
matokeo ya uchunguzi wa alama zake za vidole kuhusu kumbukumbu zake za
uhalifu. Taarifa hizi zote huwa ni kwa ajili ya kudumisha usalama wa
jamii na wa mfungwa mwenyewe anufaikapo kwa Parole.
Baada
ya Taarifa hizi zote kukamilika kila mfungwa anayependekezwa kunufaika
na Parole hufunguliwa jalada (Prison Form. 64) kwa ajili ya kutunza
kumbukumbu zake pamoja na taarifa za tabia na mwenendo wa mfungwa.
Mchakato wa kumjadili mfungwa huanzia katika Kamati za Urekebishaji ya
Gereza. Kamati hiyo hupitia taarifa hizo na kutoa maoni na mapendekezo
kwenda Bodi ya Parole ya Mkoa. Bodi ya Parole ya Mkoa hupitia maoni na
mapendekezo hayo na baada ya uchambuzi wa kina, hutoa mapendekezo yake
kwa Bodi ya Taifa ya Parole kupitia kwa Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya
Parole.
Sekretarieti
ya Taifa ya Parole ina jukumu la kuratibu shughuli zote za Bodi. Hivyo
hupokea taarifa za wafungwa waliopendekezwa au kutopendekezwa kunufaika
na Parole kutoka katika Bodi za mikoa. Huchambua taarifa hizo na kuandaa
taarifa ya kila mfungwa kwa ajili kujadiliwa na Bodi ya Taifa ya
Parole.
Bodi
hiyo kwa kutumia taaluma mbalimbali walizonazo wajumbe wake na nyadhifa
zao hufanya uchambuzi wa kina wa mawasilisho hayo na kutoa uamuzi wa
mfungwa anufaike au asinufaike na Parole. Uamuzi wa Bodi ya Taifa ya
Parole huwasilishwa kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa
uamuzi wa mwisho kwa mujibu wa Kifungu cha 6(4) cha Sheria ya Bodi za
Parole Na. 25 ya mwaka 1994 (Sura ya 400 R. E 2002).
Mheshimiwa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi hupitia taarifa za kila mfungwa na
kutoa uamuzi wa mwisho wa kukubaliwa au kukataliwa kunufaika kwa mpango
wa parole. Uamuzi huo huwasilishwa kwa Katibu wa Bodi ya Taifa ya Parole
ambaye ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Tanzania.
Itaendelea...... !.
MWANDISHI WA MAKALA HII NI AFISA NGAZI YA JUU WA JESHI LA MAGEREZA, KWA MAONI NA USHAURI - 0754 871084, lucasmboje@yahoo.co.uk or mbojelucus@gmail.com
