Mkuu wa Kituo cha
polisi Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ASP Evarest Makala
akizungumza juzi na wamiliki na madereva wa pikipiki katika warsha
iliyoandaliwa na mamlaka ya udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra).
Mmiliki wa
pikipiki Abubakary Sadik akizungumza juzi mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro
Mkoani Manyara kwenye warsha iliyoandaliwa na mamlaka ya udhibiti usafirishaji wa
nchi kavu na majini (Sumatra).
Wamiliki na
madereva wa pikipiki za kubeba abiria (bodaboda) wa Mji mdogo wa Mirerani
Wilayani Simanjiro Mkoani manyara, wakiwa katika warsha iliyoandaliwa juzi na mamlaka
ya udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra).
..........................................................................................................
Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya
Simanjiro Mkoani Manyara, Mhandisi Zephania Chaula amewataka wamiliki na madereva
wa pikipiki za kubebea abiria (bodaboda) kujiandaa kulipia mapato kupitia
leseni ya usafirishaji wa abiria.
Mhandisi Chaula
aliyasema hayo mji mdogo wa Mirerani, akizungumza na wamiliki na madereva
wa pikipiki za kubebea abiria (bodaboda) kwenye semina iliyoandaliwa na mamlaka
ya udhibiti usafirishaji wa nchi kavu na majini (Sumatra).
Alisema wanapaswa
kujiandaa na ulipaji wa leseni ya usafirishaji itakayoanza kutozwa hivi
karibuni kwani haikwepeki, hivyo wajipange kwa ajili hiyo ili wachangie mapato
ya nchi, ambayo inalenga kujitegemea.
“Hivi karibuni
tutawapa taarifa ya kuanza kwa zoezi hilo ila sasa subirini kidogo kwani hii ni
serikali ya awamu ya tano inayotaka kujitegemea kupitia mapato ya wananchi na
siyo kuomba misaada nje ya nchi,” alisema Mhandisi Chaula.
Afisa mfawidhi wa
Sumatra mkoani Manyara, Nelson Mmari alisema lengo la kukutana na bodaboda hao
ni kuhakikisha kila mmiliki anakuwa na leseni ya usafirishaji inayotolewa kupitia
halmashauri ya wilaya husika.
Mmari alisema Machi
2009, Bunge lilipitisha sheria ya kuruhusu pikipiki za magurudumu mawili au
mitatu kubeba abiria kwa malipo au kukodisha na iliyoanza kutumika mwaka 2010
hivyo leseni ya usafirishaji inapaswa kulipiwa.
Alisema kila mtu anapaswa
awe na leseni ya usafirishaji wa biashara ya kubeba abiria wa pikipiki ya
magurudumu mawili au matatu na atakayekiuka atatozwa faini ya kati ya sh50,000
au sh100,000 au kufungwa jela miezi sita au mwaka.
Alisema mkuu wa
wilaya ya Simanjiro aliwaelewesha vizuri wamiliki na madereva wa bodaboda kuwa
wajiandae na zoezi la ulipaji wa leseni ya usafirishaji kwani zoezi hilo
linatarajia kuanza hivi karibuni kwenye eneo hilo.
Kwa upande wake,
mkuu wa askari polisi wa usalama barabarani wa mkoa wa Manyara, Mary Kipesha,
alisema wanasubiri taarifa ya mkuu wa wilaya hiyo ili waanze zoezi la ufuatiliaji
ulipaji wa leseni ya usafirishaji kwa bodaboda.
“Tunasubiri
mazungumzo hayo ila mjiandae na ninyi kwani baada ya hapo ndipo tutaanza
ukamataji kwa wale ambao watakuwa hawajalipa leseni ya biashara ya kubeba
abiria kwa wenye bodaboda hapa Mirerani,” alisema Kipesha.



0 Comments