ZIKIWA zimebaki saa chache kabla ya kuchezwa kwa mchezo wa ligi kuu
ya soka Tanzania bara unaozikutanisha Mbeya City Fc na Tanzania
Prison,maandalizi kuelekea mchezo huo uliopangwa kuchezwa kwenye
uwanja wa Sokoine jijini hapa yamekamilika.
Akizungumza mbele ya wana habari muda mchache uliopita, afisa
habari wa City, Dismas Ten, amesema kuwa maandalizi ya kikosi chake
kuelekea mchezo huo uliopangwa kuchezwa jumamosi hii saambamba na
michezo mingine mitano itakayorindima kwenye viwanja tofauti tayari
yamekamilika na kinachosubiliwa na dakika 90 hiyo kesho.
“Kesho ni siku ya mchezo, kwetu sisi huu ni mchezo
muhimu kwa sababu tunahitaji kushinda ili tuendelee kuwa kwenye nafasi
za juu kwenye msimamo wa ligi, maandalizi ya kutosha yamefanyika kwa
hiyo ni nafasi kwa mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya
kusapoti timu yao,jopo la madaktari wetu limenithibitishia kuwa
Geoffrey Mlawa hatakuwepo uwanjani hiyo kesho lakini nyota wengine wako
kwenye hali nzuri, huu ni msimu ambao City inarudi kwenye zama zake”
alisema.
Kuhusu utulivu na amani uwanjani kwa mashabiki watakaojitokeza
kushuhudia mchezo huo, Ten alisema kuwa watu wanatakiwa kuzingatia
amani kwa sababu mchezo wa soka hukutanisha watu wengi hivyo ni vyema
mashabiki kushangilia timu zao huku wakiwa kwenye hali nzuri ya amani.
“Mashabiki wa City wajitokeze kwa wingi, wasiwe na
shaka ya utulivu kwa sababu ulinzi utakuwepo wa kutosha, amani mchezoni
ni jambo jema hivyo kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake kuhakikisha
tunashangilia timu yetu vizuri katika kuhanikiza ushindi huku tukiwa na
wingi wa amani” alimaliza.
City inakutana na Prison huu ukiwa ni mchezo wa 7 kwenye mfululizo wa
mechi za ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara huku rekodi zikionyesha kuwa
City imepata ushindi mara 2, Prison wakishinda mara 3 na mara 1 timu
hizi zikienda sare, Kiungo Peter Mapunda ndiye mchezaji anashika rekodi
ya kufunga bao la kwanza kabisa kwenye mechi zilizokutanisha timu hizi
mbili akifunga bao hilo kwenye mchezo wa duru ya kwanza msimu wa
2013/14 kwenye ushindi wa 2-0, misimu itatu iliyopita.

0 Comments