Na Mwamvua Mwinyi,Soga
......................................
MBUNGE wa Kibaha
Vijijini,Hamoud Jumaa ,ameungana na wakazi wa kata ya Soga kumkataa meneja anaesimamia
eneo la mwekezaji Mohammed Interprises ,Amir Mndeme, anaedaiwa kutishia amani
watu ,kudharau serikali na kujitia mungu mtu.
Aidha wameitaka serikali ifanye
uchunguzi wa kina na kuangalia upya umiliki wa eneo la mwekezaji huyo ambalo
lina ukubwa wa hekta 20,000 na kusababisha wananchi kupungukiwa na maeneo ya kujishughulisha ikiwemo kilimo.
Akizungumza katika mkutano
wa wananchi ,katika kijiji cha Soga,Jumaa alisema mgogoro baina ya wananchi
kata ya Soga na Mohammed Interprises umedumu kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Alisema mgogoro huo umefikia
pabaya kwani vijana 16 wamekamatwa na polisi kwa madai ya kuchimba mchanga
kwenye eneo la mwekezaji hali iliyosababisha wananchi kuifunga ofisi ya
serikali ya kijiji kwa siku mbili kutokana na kutokuwa na imani nayo.
Jumaa alieleza kufuatia
kutokea kwa matukio hayo alilazimika kwenda eneo la tukio ambapo wananchi
walisema hawafungui ofisi hiyo hadi viongozi wa wilaya ama mkoa wafike
kusikiliza kilio chao.
“Mgogoro huu kwasasa unakua
na kuhofia kupoteza amani iliyopo,imefikia hatua ya meneja wa MO kutumia polisi
kunyanyasa wananchi na upande wa wananchi kuweka chuki nae”
‘Tangu aletwe meneja mpya
bwana Mndeme, amekuwa akitishia amani na kutumia nguvu za pesa kunyanyasa
wananchi.Mameneja hapa wameshakuja zaidi ya sita lakini meneja huyu amekuwa
kero kubwa”alisema Jumaa.
Mndeme amekuwa akikataza
watu kukatisha katika eneo lake,kuchimba mchanga kwenye machimbo ya mchanga
ambayo anadai yapo kwenye eneo hilo na kupelea kuwanyima uhuru wananchi.
“Machimbo hayo ni ya asili
,vijana wanajitafutia kipato lakini yeye anakataza watu wasichimbe na kutumia
polisi kuwakamata ambapo juzi walikamatwa vijana 16 ”alisema Jumaa.
Jumaa alisema hatua
zichukuliwe haraka pamoja na mwajiri Mohammed inteprises amwondoe meneja wake
ili kurejesha amani kwa jamii.
Nae mtendaji wa kata ya
Soga, Betram Mfalamagoha,alisema septemba 20 baadhi ya polisi walioambatana na
Mndeme walienda kuwakamata vijana 16 ,waliokuwa wakichimba mchanga kwenye machimbo
ya mchanga.
Alisema kijana mwingine
aligongwa na gari la mikopo kisha, askari polisi walikwenda na kuendelea
kumpiga kijana huyo licha ya kuwa amegongwa na sasa yupo Tumbi hospital kwa
matibabu.
Wakazi wa kata hiyo,
akiwemo Hussein Maro,Ramadhani Rashid ,Iddi Muhunzi na mwenyekiti wa kijiji cha
Kipangege Shomary Mwinshehe ,walisema wamechoshwa na tabia anazozifanya meneja
Mndeme.
Walisema baadhi ya polisi wamewekwa
mkononi kwani wamekuwa wakitumika na meneja huyo kwenda kuwakamata wananchi na
kuwashurutisha bila kosa.
Mzee Omary Kibwana ,alisema
anaimani na serikali kuwa itaangalia suala hilo kwa kina ili kuleta suluhisho
la mgogoro huo wa kipindi kirefu.
Mkuu wa kituo cha polisi
Kibaha,Emmanuel Bondo ,alisema kazi yao ni kulinda amani kwa watu wote bila
kupendelea.
Kamanda Bondo alisema
,kutokana na malalamiko aliyofikishiwa atayafanyia kazi na kuahidi kushirikiana
na wananchi hao pale patakapokuwa na tatizo.
Nae mkuu wa wilaya ya
Kibaha ,Assumpter Mshama alifika katika eneo hilo na kutoa agizo kuwa meneja
Mndeme aondoke kuanzia sasa na mwajiri wake atafute meneja mwingine.
Alisema hakuna jeuri zaidi
ya serikali na serikali haiwezi kumvumilia mtu mmoja ambae anatishia maisha ya
watu na kuwajengea hofu ya kuishi.
Assumpter alieleza hakuna
mungu mtu zaidi ya wananchi na sasa yeye ndie atakuwa saizi yake huyo meneja
anaetikisa kata nzima kwa pesa zake.
Aliomba wananchi
wasibuguziwe na kuwataka polisi wasiwe wepesi wa kuhongwa kitu kidogo kwa ajili
ya kuwakandamiza wananchi.
Assumpter alitoa pole kwa
kijana aliyegongwa na gari la mikopo
kisha kupigwa tena na polisi kwa madai ya kuingia kwenye eneo la MO, na
kuongeza kuwa amesikitishwa na vitendo vya meneja huyo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema
kuanzia sasa Mndeme aondoke,na kuwaasa wananchi wasifanye fujo wala maandamano
bali watulie na serikali ipo kwa ajili yao.
Mndeme alipatikana kwa njia
ya simu na kusema hawezi kuzungumzia suala hilo kutokana na vitisho ambavyo
ameshaanza kuvipata,na baada ya kujibu hayo alikata simu.
Baada ya mkutano huo
wananchi waliamua kutoa magogo na makuti waliyofunga kwenye ofisi ya serikali
ya kijiji ambayo waliifunga kutokana na sakata hilo.
0 Comments