Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Equator SUMAJKT kilichopo Ruvu Mkoani Pwani, Robert Mangazeni akizungumza na waandishi wa habari waliokwenda kutembelea na kujua hatua ilipofikia ujenzi wa kiwanda cha kuunganisha matrekta pamoja na kutengeneza magari ya zimamoto.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
......................................................................................................
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
KAMPUNI ya equator SUMAJKT iliyoko Ruvu, mkoani Pwani, kwa mara ya kwanza itaanza kuunganisha matrekta ya farmtrac hapa nchini baada ya kuingia mkataba wa uhawilishaji teknolojia na kampuni inayotengeneza matrekta hayo ya Escort ya India.
Kupitia makubaliano hayo equator SUMAJKT itaweza kuunganisha matrekta kwa ajili ya soko la Tanzania na masoko ya bara la Afrika kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari, waliokwenda kutembelea kiwanda hicho, mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo Robert Mangazeni alisema awali matrekta yalikuwa yakiletwa kutoka India.
Alisema lakini baada ya makubaliano hayo kampuni hiyo haitaleta tena matrekta hapa nchini badala yake yataunganishwa katika kiwanda hicho cha kampuni ya Equator SMJKT.
" Hatujawahi kuwa na kiwanda wala karakana za kutengeneza matrekta hapa nchini, yanapohabirika hutengenezwa kiwango cha chini na mafundi wasio na ujuzi,"
"Mara nyingi yakishindikana huegeshwa na kutelekezwa baada ya kushindwa kufanya Kazi, kwa mara ya kwanza equator SUMAJKT tutafanya Kazi hiyo, tunayetengeneza pia kuyahudumia yanapoharibika, "alisema Mangazeni.
Alisema matrekta hayo watayauza wakulima kupitia wakala wao kwa bei nafuu lakini pia watakopesha wakulima walipe kidogo kulingana na uwezo wa kila mtu ili kusaidia waweze kulima kilimo chenye tija na kupata kipato na faida.
Aidha Mangazeni alisema kiwanda hicho kinatarajia kuanza kazi rasmi mwezi novemba.
Alielezea kuwa mbali na kazi yaykuunganisha matrekta pia kiwanda hicho kitaunganisha mabasi, na magari mbalimbali, pia zana za kilimo.
" Tunatarajia kushirikiana na viwanda vya ndani kwa ajili ya kuzalisha vipuli mbalimbali vya magari, matrekta na zana za kilimo, tunategemea kushirikiana na kampuni ya Automech, kiwandacha TATC- Nyumbu, SIDO, UDSM na vingine.
Alisema wataalamu kutoka nje kwa ajili ya ufungaji wa mitambo wameshafika na hatua za awali za ujenzi wa majengo ya kiwanda hicho na usimikaji wa mitambo na vifaa zimeshaanza.
Mangazeni alisema hadi sasa zimeshatumika kiasi cha sh.bil 2,ambapo hadi kukamilika kwake mwishoni mwa mwezi novemba kinatarijia kutumia bil.3.
Kampuni ya equator SUMAJKT ni ubia kati ya shirika la uzalishaji mali la JKT (SUMAJKT) na kampuni ya equator Automech ambayo ni ya watanzania wakiwamo wastaafu kutoka jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania (JWTZ).


0 Comments