Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mh.
January Makamba akiongea na waandishi wa Habari juu ya Siku ya Kimataifa
ya tabaka la Ozoni. Siku hii huadhimishwa Septemba 16 kila mwaka.
Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mazingira Bw. Richard Muyungi.
(Picha
kwa hisani ya Idara ya Habari Maelezo)
..........................................................................................................................
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
ILIYOTOLEWA NA
JANUARY Y. MAKAMBA (MB.), WAZIRI WA NCHI, OFISI YA
MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA
KATIKA KUADHIMISHA
SIKU YA KIMATAIFA YA HIFADHI YA TABAKA LA OZONI
16
SEPTEMBA, 2016
Ndugu Wananchi,
1. Tarehe 16 Septemba mwaka huu tutaungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha
Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni kama ilivyoagizwa na Mkutano Mkuu
wa Umoja wa Mataifa katika Azimio lake nambari 49/114 la tarehe 19 Desemba 1998
kama kumbukumbu ya tarehe ya kutiwa saini Mkataba wa Montreal (Montreal Protocol - 1987) kuhusu
kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Hewa ya Ozoni angani.
Ozoni ni hewa iliyoko kwenye angahewa ya juu, takribani
kilometa 10 hadi 50 juu ya ardhi. Kazi yake kubwa ni kuchuja sehemu kubwa ya
mnururisho wa mionzi kama “Ultraviolet B”
isifike kwenye uso wa dunia. Ujumbe wa mwaka huu ni “Kuhuisha
Tabaka la Ozoni na Tabia-Nchi kwa pamoja Duniani”. Ujumbe huu umeambatana na Kauli mbiu isemayo “Kukabiliana
na ongezeko la gesi Joto Duniani
HFCs chini ya Itifaki ya Montreal”.
2. Tabaka la Ozoni linapoharibiwa huchangia kuruhusu mionzi
zaidi ya “Ultraviolet B” kufika
kwenye uso wa dunia na hivyo kusababisha kuongezeka kwa magonjwa kama vile saratani
ya ngozi, uharibifu wa macho yaani "mtoto wa jicho" unaosababisha
upofu, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi na kujikunja kwa ngozi. Aidha, madhara
mengine ni kuharibika kwa mimea hasa mazao ya kilimo kutokana na kuathirika kwa
maumbile na mifumo ya ukuaji. Vile vile, baadhi ya kemikali hizi husababisha
kuongezeka kwa joto duniani na hivyo kuchangia katika mabadiliko ya tabianchi.
3. Ili kulinda tabaka la Ozoni, Serikali za mataifa
mbalimbali zilikubaliana kuunda Mkataba wa Vienna (Vienna Convention) wa
Hifadhi ya Tabaka la Ozoni mwaka 1985. Mkataba huu unasisitiza ushirikiano
katika utafiti, usimamizi na ubadilishanaji wa taarifa za hali ya Tabaka la Ozoni
kutokana na kupungua kwa matumizi yake. Vile vile ulianzishwa Mkataba wa Montreal
(Montreal Protocol) unaohusu udhibiti wa kemikali zinazomong'onyoa Tabaka la
Ozoni na Mkataba huu ulipitishwa tarehe
16 Septemba, 1987. Lengo kuu la Mkataba huu ni kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa
kudhibiti utengenezaji na matumizi ya kemikali zinazoharibu Tabaka hili.
4. Hadi sasa Mkataba wa Montreal umepata mafanikio makubwa
ya kupunguza zaidi ya kiasi cha asilimia 98 (takribani tani 1.8) ya uzalishaji
wa matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Hewa ya Ozoni. Punguzo hilo
la matumizi ya kemikali hizi limechangia katika juhudi za kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi kwa sababu baadhi ya kemikali zinazomong’onyoa tabaka
la Ozoni pia husababisha kuongezeka kwa joto duniani. Kwa mfano, kiasi cha
kemikali kilichoondolewa katika matumizi ni takriban tani bilioni 135 za hewa
ukaa na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na ongezeko la
joto duniani na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, matokeo ya tafiti
yanathibitisha kwamba kiwango cha kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni angani
kinaendelea kupungua na inakadiriwa kuwa iwapo jitihada za utekelezaji wa
Mkataba huu zitaendelea, Tabaka la Ozoni litarudi katika hali ya kawaida
ifikapo katikati ya karne hii.
5. Ili kufanikisha utekelezaji wa Mkataba wa Montreal, mwaka
1996 Serikali iliandaa na kutekeleza Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya
kemikali hizi. Mikakati ya kitaifa ndani ya Programu hii ni pamoja na:
i) Kujenga uwezo wa Taasisi zinazosimamia utekelezeji wa
Mkataba;
ii) Kuweka takwimu za kemikali hizo;
iii) Kutoa elimu kwa wadau na kwa umma wa Watanzania kuhusu
umuhimu wa Tabaka la Ozoni na hatari zinazolikabili;
iv) Kusambaza habari kuhusu kemikali na tekinolojia mbadala;
v) Kubadilisha tekinolojia katika viwanda vinavyotumia
kemikali haribifu;
vi) Kutoa mafunzo yanayolenga kuimarisha ujuzi katika sekta
ya kuhudumia viyoyozi na majokofu;
vii) Kuimarisha mbinu za upunguzaji wa matumizi ya kemikali
husika kwa kuanzisha mtandao wa kunasa, kusafisha na kurejeleza vipoza joto;
viii) Kuhamasisha na kuhimiza matumizi ya kemikali na
tekinolojia mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni; na
ix)
Kuweka
taratibu za kudhibiti uingizaji na matumizi ya kemikali zinazodhibitiwa na
Mkataba wa Montreal.
6. Hatua hizi zimewezesha Tanzania kuondosha kemikali hizi
kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa na Mkataba. Kwa mfano, Viwanda vitatu
vilivyokuwa vinatumia kemikali haribifu vimebadilisha teknolojia hiyo. Aidha,
wafanyabishara wengi ambao ni wauzaji wa kemikali husika wamekuwa na uelewa
mkubwa na hivyo biashara ya kemikali mbadala imeendelea kukua mwaka hadi mwaka.
7. Chini ya Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya
kemikali haribifu, Serikali iliandaa Mpango wa Usimamizi wa Vipozi (Refrigerant Management Plan) ambao
utekelezaji wake umefanyika kama ifuatavyo:
i.
Kuandaa
Kanuni za Usimamizi wa Kemikali Zinazomong’onyoa Tabaka la hewa ya Ozoni na zilianza
kutumika tarehe 7 Desemba 2007;
ii.
Jumla
ya mafundi mchundo wa viyoyozi na majokofu 500 wamepatiwa mafunzo kuhusu njia
bora za kuhudumia vifaa hivyo bila kuathiri Tabaka la hewa ya Ozoni;
iii.
Kusambazwa
kwa Vitambuzi vya kemikali hizi vipatavyo 18 kwa ajili ya usambazaji katika
vituo vilivyo mipakani mwa nchi yetu;
iv.
Mashine
20 za kunasa na 5 za kunasa na kurejeleza gesi chakavu zimenunuliwa na kusambazwa kwa
karakana 20 na Vituo vitano vya Kikanda vya kunasa na kusafisha gesi chakavu za
Majokofu na Viyoyozi katika vyuo vya VETA vya Mwanza, Chang’ombe - Dar es
salaam, Kigoma, Mbeya na Mkokotoni-Zanzibar;
v.
Mtambo
wa kunasa na kurejeleza kemikali umewekwa katika Kituo cha Tanzania cha Uzalishaji
Bora na Tekinolojia Endelevu (Cleaner
Production Centre for Tanzania);
vi.
Utekelezaji
wa Mpango wa Kusimamia Usitishaji wa Matumizi ya Kemikali hizi (Terminal Phase-out Management Plan
(TPMP).
vii.
Jumla
ya maafisa forodha na wasimamizi wa sheria 172 wamepatiwa mafunzo kuhusu
udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la hewa ya Ozoni.
viii.
Hadi
sasa Tanzania imeweza kupunguza zaidi ya tani 216 sawa na asilimia 86 ya kiasi
cha matumizi ya kemikali hizi cha mwaka
1999.
8. Hapa nchini maadhimisho haya yatafanyika kwa njia ya
uelimishaji umma kuhusu Tabaka la
Ozoni, faida zake, madhara ya kuharibika kwa Tabaka hili na matumizi salama ya
bidhaa zenye kemikali rafiki kwa Tabaka la ozoni. Hivyo kupitia kwenu
wanahabari naamini elimu hii itaendelea kutolewa kwa jamii ya Watanzania ili
kuongeza ushiriki wao katika kutekeleza jukumu hili muhimu la kulinda sayari
hii. Makala zimeandaliwa ili muweze kuzitumia katika kuwafikishia Wananchi
elimu hii muhimu.
9. Ni muhimu tuzingatie kwamba juhudi za kila mmoja wetu
zinatakiwa ili kupunguza na kuondosha madhara katika Tabaka la Ozoni
yanayosababishwa na bidhaa tunazonunua na kutumia majumbani au sehemu za
biashara. Natoa wito kwa kila mwananchi kushiriki katika kuhifadhi Tabaka la
Ozoni kwa kuzingatia mambo yafuatayo:
i.
Kuepuka
kuingiza nchini gesi zilizopigwa
marufuku na vifaa vinavyotumia gesi haribifu kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika (mitumba) na ambavyo vinatumia
vipoozi aina ya R11 na R12.
ii.
Kuingiza
nchini vipoozi mbadala na rafiki kwa
tabaka la Ozoni kama vile R22, R134a,
R407, R404 na R717.
iii.
Kununua bidhaa zilizowekwa nembo rasmi isemayo “Ozone
friendly” yaani “sahibu wa Ozoni” au “CFC-free”
ikiashiria haina wala haikutengenezwa na kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni.
iv.
Kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani ama vifaa vya
kuzima moto vyenye kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni aina ya “CFCs” na
“halon”. Pata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mafundi ama
mamlaka zinazohusika.
v.
Kuepuka matumizi ya
kemikali aina ya “Methyl bromide”
kufukizia udongo, na badala yake kutumia mbinu mbadala na salama pamoja na
mbinu tungamanishi za udhibiti wa wadudu waharibifu yaani “integrated pest management”.
vi.
Mafundi
wa majokofu na viyoyozi wahakikishe
kuwa wananasa na kutumia tena vipoozi (refrigerants)
kutoka kwenye viyoyozi, na majokofu wanayohudumia badala ya kuviachia huru visambae
angani. Aidha, mafundi watoe elimu kwa
wateja wao juu ya njia rahisi za kutambua uvujaji wa vipoozi kutoka katika
majokofu na viyoyozi wanavyotumia.
10. Nawatakieni maadhimisho mema ya Siku ya Kimataifa ya
Hifadhi ya Tabaka la Ozoni.
JANUARY Y. MAKAMBA (MB.)
WAZIRI
WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS
MUUNGANO NA MAZINGIRA


0 Comments