Hapa ni Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Picha na Maktaba
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
.....................................
BODI ya barabara mkoani Pwani ,imewatahadhalisha
wafanyabiashara na wananchi wa Mailmoja,Mji wa Kibaha,ambao wamejenga
kwenye eneo la hifadhi ya barabara ,kuanza kubomoa kwa hiari ,kabla ya
novemba 23.
Imesema wakala wa barabara (TANROADS )ilishawaandikia
barua watu waliojenga kwenye eneo la hifadhi ya barabara umbali wa mita
60 kwa kila upande wa barabara kuu ya Morogoro kuanzia Kiluvya -Tamco
kwa kipindi kirefu sasa.
Akizungumza katika kikao cha bodi ya barabara mkoani
Pwani,mwenyekiti wa bodi hiyo mkoani humo,mhandisi Evarist
Ndikilo,alisema wakala huo utaanza kubomoa eneo la mita 60 badala ya 120
zilizoelezwa awali.
Alieleza kuwa ni wakati wa jamii kukubali mabadiliko hayo
ambayo yapo ndani ya sheria ili mji wa Kibaha uweze kuwa katika
mpangilio mzuri.
Mhandisi Ndikilo alisema kipindi cha nyuma wananchi
walipinga kufanyika kwa bomoabomoa lakini walishindwa kesi walizofungua
hivyo kwasasa ni vyema wakapisha maeneo hayo bila shuruti.
"Tanroads ikifika novemba 23 mwaka huu itavunja eneo la Mailmoja na haiwezi kurudi nyuma"
"Lengo letu ni halmashauri ya Mji kuwa manispaa hivyo moja
ya vigezo ni kupanga Mji huu ,wananchi watuelewe na wote tunahitaji
kupanga Mji wetu alifafanua mwenyekiti huyo .
Alieleza kuwa kutokana na sintofahamu ya hifadhi ya mita
120 ama mita 60 kila upande hadi hapo wizara ya ujenzi itakapotoa
ufafanuzi hivyo wakala huo utaanza kubomoa upana wa mita 60.
Mwenyekiti huyo ambae pia ni mkuu wa mkoa wa Pwani,
mhandisi Ndikilo,alisema wananchi waanze kufunga virago na hakuna
mjadala kuhusiana na hilo.
Nae mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Jennifer
Omolo alisema soko la sasa litahamia eneo la Sagulasagula na fedha zipo
na tangazo la kumpata mkandarasi limeshatoka.
Alisema soko la Sagulasagula linatarajia kukamilika mwezi wa 12 mwaka huu.
Hata hivyo ,Jennifer alielezea kuwa wafanyabiashara
wanaofanya biashara kwenye eneo la Mailmoja wawasiliane na halmashauri
kupata maeneo pembezoni mwa soko la Sagulasagula kwa ajili ya kujenga
mabanda yao.
Jennifer aliwaomba wafanyabiashara hao kuanza kuwasiliana na halmashauri ili waanze kuchukua maeneo na kuajenga mapema.
Pia alisema maeneo ya Mailmoja yaliyo ndani ya hifadhi ya
barabara yatabomolewa lakini stend itaendelea kufanya kazi hadi hapo
itakapojengwa stend mpya .
Jennifer alisema endapo zoezi la bomoa bomoa litafanyika
itawasaidia halmashauri kupanga Mji na kuwa na kujenga mabanda ya
kupumzikia abiria eneo la stend ya sasa.
Meneja wa Tanroads mkoani Pwani, Tumaini Sarakikya alisema
awali zoezi hilo lilikuwa lifanyike mwezi agost lakini muda uliongezwa
hadi mwezi novemba na kudai wapo watu wengine walishawekewa alama ya X
tangu mwaka 2004 .
Alisema katika kipindi hicho chote zoezi hilo halikufanyika ila kwasasa ndio linatarajiwa kutekelezwa na hawawezi kurudi nyuma.
Sarakikya alisema wananchi walikwenda mahakamani ambapo walishindwa kesi.
Anasema kwa mujibu wa sheria ya barabara ya mwaka 1932 na
kufanyiwa marekebisho 1958 kifunga na 52 na marekebisho ya sheria ya
barabara na 13 ya mwaka 2007 .
Taratibu za sheria za usimamizi wa barabara kifunga na 30
(b) eneo la hifadhi ya barabara,mita 120 sawa na futi 400 kwenda kila
upande kutoka katikati ya barabara ni marufuku kufanya maendelezo yoyote
katika eneo hilo.