Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi katika Wizara ya
Elimu Sayansi na Teknolojia, Sarah
Mlaki, akimkabidhi cheti cha kumaliza darasa la saba mhitimu Mercygracious
Tolla wa Shule ya Msingi ya Macedonia kwenye mahafali ya tano
ya shule hiyo iliyoko Tabata Segerea jijini Dar es Salaam.
.............................................................................
Hussein
Makame-MAELEZO
SERIKALI
imesema itawachukulia hatua stahiki wale wote watakaobainika kwa sababu moja au
nyingine kuhusika na matukio ya moto yaliyotokea mkoani Arusha hivi karibuni.
Hayo
yamesema na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Simon Msanjila
katika mahafali ya tano ya Shule ya Msingi ya Macedonia iliyopo Tabata Segerea
jijini Dar es Salaam yaliyofanyika mwishoni mwa wiki.
Akizungumza
kwa niaba ya Prof. Msanjila ambaye alialikwa kuwa mgeni rasmi, Mkurugenzi wa
Elimu ya Msingi wa wizara hiyo Sarah
Mlaki alikuwa akijibu kilio
cha Mkuu wa shule hiyo aliyelaani matukio hayo ya moto kuendelea kujitokeza
huko mkoani Arusha na maeneo mengine.
Alisema
mbali na kuwachukulia hatua wahusika, Serikali imechukua hatua mbalimbali
kudhibiti majanga ya moto katika shule zetu za sekondari za bweni nchini.
“Serikali
imechukua hatua mbalimbali kudhibiti majanga ya moto katika shule zetu za
sekondari za bweni.Tutachukua hatua stahiki kwa wale ambao watabainika kwa
sababu moja au nyingine wanahusika na majanga hayo”, alisema Mkurugenzi Mlaki.
Mkurugenzi
huyo aliongeza kuwa Serikali pia imejipanga kuboresha miundombinu ya shule zake
ili watoto Watanzania wapate haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Kwa
upande mwingine, Mkurugenzi Mlaki alisema soko la vitabu vya kiada
vinavyotumika katika shule za msingi
nchini limevamiwa na watu mbalimbali na Serikali inafahamu kuwa kuna vitabu
vingine havina ubora unaostahili kwa matumizi ya shule.
Hata
hivyo, Mkurugenzi Mlaki alisema Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania
(TEA) imepewa dhamana ya kuandaa vitabu vya kiada ili wanafunzi wote kutumie
vitabu hivyo bila ya kuwa na tofauti katika elimu inayotolewa.
“Kwa
kweli soko la vitabu limevamiwa na watu mbalimbali na tunafahamu kuna vitabu
vingine havina ubora stahiki, lakini Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania
(TEA) imepewa dhamana ya kuandaa vitabu vya kiada (text book) ili wanafunzi
wote waweze kutumia vitabu hivi pasiwe na tofauti katika elimu inayotolewa”
alisema Mkurugenzi Mlaki.
Aliongeza
kuwa anaamini kwamba tatiz hilo litatatuliwa kadri siku zinavyokwenda kwa kuwa
taasisi husika tayari inalishughulikia suala hilo kulingana na uzito wake.
Katika
mahafali hayo jumla ya wanafunzi 53 wa shule hiyo walihitimu na wanatarajia
kufanya mitihani ya taifa ya darasa la saba mwaka huu, wakiwemo wanafunzi 24
wanaume na wanawake 29.
Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo Shukuru Mbwire alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2009,
imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya darasa la saba na la nne ambapo
ilianza na wanafunzi 70 lakini hadi sasa ina wafanuzi 782.
Alisema
katika matokeo ya mitihani ya kitaifa ya darasa la saba shule hiyo imekuwa
ikifanya vizuri mwaka hadi mwaka ambapo katika mitihani ya mwaka 2015 shule
hiyo ilipata wastani wa daraja A na kushika nafasi ya 3 kati ya shule 56
kiwilaya, nafasi ya 28 kati ya shule 534 kimkoa na kitaifa ilishika nafasi ya
219 kati ya shule 16,096.
“Kwa
miaka yote hiyo shule ilifaulisha wanafunzi kwa asilimia 100 ambapo watoto wote
walifanikiwa kujiunga na shule za Sekondari za vipaji maalum na zile za
kawaida” alisema Mbwire.
Katika
risala ya wanafunzi wa shule hiyo, wahitimu walitangaza kumuunga mkono
kaulimbiu ya Rais John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu na kuwataka Watanzania
wafanye kazi kwa bidii ili kulikomboa Taifa na umasikini.

