Na Beatrice Lyimo na
Eleuteri Mangi-MAELEZO, Dodoma
Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amehitimisha Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi na
Mbili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Mjini Dodoma.
Akihitimisha Bunge,
Waziri Mkuu ameainisha mambo mbalimbali ambayo yamefanyika wakati wa Mkutano
huo ikiwa ni pamoja na mijadala mbalimbali inayohusu miswada ya sheria
iliyosomwa kwa mara ya kwanza, mara pili na kwa mara ya tatu.
Waziri Mkuu amesema
kuwa mijadala ya mkutano huo ilikuwa ya uwazi na hoja zilizotolewa zililenga
katika kuleta maendeleo nchini.
“Nawapongeza sana
wabunge wote kutokana na michango yenu mizuri na yenye tija hatua ambayo
ilibidi mara kadhaa vikao vyetu kuendelea hadi usiku ikiwa ni nje ya muda wa
kanuni za Bunge” amesisitiza Waziri Mkuu.
Katika kuhitimisha
mkutano huo, Waziri Mkuu amebainisha baadhi ya matukio mbalimbali yaliyotokea
nchini ikiwemo janga la tetemeko la ardhi, shughuli za bunge, mwenendo na mwelekeo
wa hali ya uchumi, mwenendo wa ukusanyaji mapato ya Serikali, mpango wa
Serikali kuhamia Dodoma, hali ya upatikanaji wa chakula nchini, maboresho
katika tasnia ya Ushirika, Sekta ya elimu, suala la uhakiki wa vyeti kwa
watumishi, kuimarisha usafiri wa anga, hali ya amani na utulivu nchini pamoja
na suala la michezo nchini.
Akizungumzia kuhusu
janga la tetemeko la ardhi lililotokea mikoa ya Kanda ya Ziwa, Waziri Mkuu
ametoa wito kwa wananchi, Sekta binafsi na Jumuiya za Kimataifa kuendelea
kushirikiana na Serikali katika kusaidia waathirika wa tetemeko hilo.
“Serikali inaendelea
kukusanya michango kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali, waliotayari
kuchangia wanaweza kutumia akaunti ya maafa iliyofunguliwa benki ya CRDB yenye
namba 0152225617300 kwa jina la Kamati ya Maafa Kagera na kwa njia ya simu
michango hiyo inaweza kutumwa pia kupitia M-pesa 0768-196669, Airtel Money 0682-950009
na Tigo pesa 0718-069616” amesisitiza Waziri Mkuu.
Kwa upande wa
mwenendo na mwelekeo wa hali ya uchumi nchini, Waziri Mkuu amesema kuwa kwa
ujumla hali ya uchumi nchini inaridhisha na inaendelea kuimarika.
Kwa mujibu wa Benki
Kuu ya Tanzania (BOT) hali ya uchumi umeimarika ambapo pato la Taifa lilikua
asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kwa mwaka 2015, ukuaji huo unatoka
na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, huduma za mawasiliano, utangazaji na
huduma za intaneti na kuongezeka kwa uchimbaji wa madini.
Katika suala la
ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa mwezi Julai na Agosti, Waziri Mkuu amesema
kuwa takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi hicho mapato yanayokusanywa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalikuwa shilingi Trilioni 2.168
ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi trilioni 2.113 ikiwa ni sawa
na ongezeko la asilimia 103 ya lengo la Serikali.
Waziri Mkuu amesema
kuwa, katika mpango wa Serikali kuhamia Dodoma ni dhamira ya Serikali ya Awamu
ya tano ya kukamilisha mchakato na ahadi ya Serikali ya kuhamia katika Mji wa Makao
Makuu Dodoma ambapo utekelezaji wake utakuwa wa awamu sita.
Vilevile katika sekta
ya Kilimo, Waziri Mkuu amesema kuwa hali uzalishaji na upatikanaji wa chakula
nchini umefika tani 16,172,841, ambapo Serikali imetoa ruzuku za pembejeo za
kilimo kwa ajili ya mazao ya chakula hususani mahindi, mpunga na mtama, kwa
upande wa mazao ya biashara ruzuku hiyo hutolewa katoka mazao ya korosho,
pamba, chai, kahawa na alizeti.
Pia Serikali itafanya
marekebisho ndani ya tume ya maendeleo ya Ushirika na kuchukua hatua za kinidhamu
kwa watakao bainika na ubadhirifu wa mali za ushirika.
Katika Sekta ya
Elimu, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Serikali imeamua walimu wapya
watakaoajiriwa wapangiwe vituo vya kazi moja kwa moja na kwa kuzingatia maeneo
yenye upungufu wa walimu.
Kuhusu uhakiki wa vyeti
vya watumishi, Waziri Mkuu amesema kuwa, Serikali inaendelea na zoezi la
uhakiki wa vyeti vya watumishi na kuwaagiza wagurugenzi wa halmashauri kuandaa
vituo maalum ambavyo vipo jirani na vituo vya kazi ili kuwapunguzia watumishi
gharama na adha wakati wa zoezi hilo.
Katika kuboresha
usafiri wa anga nchini, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imenunua ndege mbili aina ya Dash
8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja zitakazotumika kutoa huduma za
usafiri wa anga kwa soko la ndani na chi jirani.
Hata hivyo Waziri
Mkuu amesema kuwa vyombo vya usalama na ulinzi nchini vimeendelea kulinda na
kudumisha amani na utulivu nchini kwa manufaa ya ustawi wa nchi ili kufanikisha
lengo la kukuza uchumi na kuondoa umaskini.
Aidha, Waziri Mkuu
ameipongeza Timu ya Taifa ya Vijana Serengeti Boys kwa kuiwakilisha vyema Tanzania
katika mashindano ya Kimataifa.
Mbali na hayo Waziri
Mkuu Majaliwa amepokea michango mbalimbali iliyotolewa na Kampuni ya Caspian
shilingi milioni 100, Ofisi ya Taifa ya Takwimu shilinhi milioni 1.6 na kampuni
ya Bordar Ltd shilingi milioni 20 kwa ajili ya waadhirika wa tetemeko
lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

0 Comments