Mkazi wa Kilindi,
Tanga Angela Basso , aliyetembea kwa miguu kwa muda wa siku 21 pamoja na Watoto wake Janeth Peter (9) na
Happy Peter (7) kuja Mkoani Dodoma kuonana na Waziri mkuu ili kupeleka
malalamiko yake ya kudhulumiwa mashamba yake ya hekari 30 na kuchomewa nyumba .
........................................................................................
MKAZI wa Kilindi mkoani
Tanga, Angela Basso, akiwa na watoto wake wawili Happy(7) na Janeth
Peter(9), amelazimika kutembea kwa mikuu kwa siku 21 hadi mkoani Dodoma kwa
lengo la kumuona Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili amsaidie kurudishiwa hekari 30
za mashamba yake aliyozoporwa.
Basso alifika mjini Dodoma akiwa na
watoto wake hao, ambapo alisema aliona ni vyema kwenda Dodoma kuonana na Waziri
Mkuu kutokana na kuporwa mashamba na kuchomewa nyumba yake katika kijiji cha
Kwendigole wilayani Kilindi na wanaume wawili ambao waliojitokeza kwa nyakati
tofauti wakidai ni maeneo yao.
Alisema alipita hatua zote
zinazotakiwa kuomba mashamba, ambapo awali alipatiwa hekari 10 na kijiji
na akazifanyia shughuli za kilimo na kujenga nyumba yake ya kuishi, lakini
baada ya kwenda kujifungua alikuta mazao yamefyekwa na yeye kutakiwa kuondoka
kwenye eneo hilo.
Mwanamke huyo alisema baada ya
kunyang’anywa alifikisha malalamiko yake kuanzia uongozi wa kijiji hadi
wilayani na baadaye akapatiwa eneo jingine la hekari 20, lakini alijitokeza mtu
mwingine na kudai eneo hilo ni mali ya kanisa, licha ya kumiliki kihalali eneo
la Hembekali.
“Nilikwenda kushtaki kwa serikali ya
kijiji, kata na baadaye kwenda kwa mkuu wa wilaya ambako iliamuliwa nirudishiwe
mashamba yangu, lakini hawakufanya hivyo mwisho wa siku nikafukuzwa kabisa
kuishi kwenye eneo hilo,” alisema Basso
Mwanamke huyo alisema baada ya kutimuliwa alianza kuishi maisha yake kituo cha
mabasi Muheza na baadaye alifukuzwa kituoni hapo kwa madai watu hawaruhusu
kulala ama kuishi hapo na ndipo akaamua kuanza safari ya Dodoma baada ya
kusikia Waziri Mkuu amehamia Dodoma.
Akisimulia machungu ya safari yake,
Basso alisema akiwa njiani walikuwa wakila mahindi ya kukaanga na maji ya
kunywa na kulala porini muda mwingine giza linapowakuta katikati ya pori.
“Naomba kusaidiwa jamani nimeanza kufuatilia tangu mwaka 2012 lakini bila
mafanikio jambo ambalo limechangia familia yake kusambaratika kutokana na
kukosa pa kuishi huku watoto wangu hawa wakikosa elimu kwa
kutangatanga,”alisema Mwanamke huyo
Basso aliomba Serikali itende haki
ili yeye aweze kupata haki yake ya kurejeshewa mashamba yake na kurudi katika
eneo hilo ili watoto wake wawili wapate nafasi ya kusoma.
Mwanamke huyo alisema kwa sasa
amekuwa kama mkimbizi kutokana na kukosa hana mahali pa kuishi huku mumewe naye
akiikimbia familia yake baada ya kuporwa ardhi hiyo ambayo ilikuwa kama kitega
uchumi chao.


0 Comments