Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
...........................................................
MADEREVA wa matipa ya mchanga
,wanaotumia barabara kuu ya Dar es salaam –Morogoro, wamefanya mgomo baridi ,kulalamikia
wakala wa barabara (TANROADS)mkoani Pwani,unaowakamata kutokana na kutofunga
mchanga vizuri na kuwapiga faini ya sh.500,000.
Madereva hao waliweka mgomo
huo katika eneo la Tamco ambapo ndipo watendaji wa wakala huo walikuwa wakiwasimamisha
kwa ajili ya kukagua wale waliojaza mchanga hali inayosababisha kuchafua miundombinu
ya barabara.
Dereva Martine Magari na
Emmanuel Shao,walisema ni kweli wapo madereva wasiofunga vizuri maturubai ya
magari yao lakini tatizo kubwa ni kukosa elimu ya kufunga kwa ubora .
Shao aliziomba idara ama
mamlaka husika kutoa elimu juu ya sheria mbalimbali kwani inakuwa sio rahisi
kuelewa sheria zote zinazotungwa bila kupatiwa elimu ya kutosha.
“Unaona fuso dogo kama
lile,huwezi amini ni sh.500,000 kikweli ni kubwa ,sasa unakuta tunalalamika
kutokana na kwamba hatujui lolote kuhusu sheria zao”
“Halafu hatujafundishwa
kufunga hooks wanavyotaka wao wakala wa barabara,kila mtu anaufungaji wake lakini
endapo watatuelewesha vizuri haina shida .
"Sasa wao wanapanda juu ya gari na
kuchokonoa chokono matokeo yake ndio
inakuwa shida ,mchanga unamwagika”alisema Shao.
Magari aliutaka wakala huo
kukagua kwa macho na sio kupekenyua maturubai kwa kuingiza mikono kwani kwa kufanya
hivyo ni lazima mchanga mwagike .
“Madereva pia wamekasirika
kwa hilo huwezi kukagua hadi uingize mikono ,kwakuwa mikono inasababisha
mchanga kumwagika halafu unatozwa hela yote hiyo”alifafanua Magari.
Kwa mujibu wa kaimu meneja
TANROADS mkoani Pwani,injinia Yudas Msangi,alisema wapo kwenye operesheni ya kukagua
magari ,kwa kufuata sheria ya barabara ya mwaka 2007 namba 13 kifungu namba 46C,
inayokataza kuchafua barabara .
Alieleza kuwa hakuna anaewaonea
madereva hao ,kwani wanatambua vilivyo kuhusu sheria hiyo na mara kwa mara huwa
wakielimishwa kuacha tabia ya kuzembea kufunga mchanga vizuri.
Injinia Msangi
alisema,wanatoa muda hadi jumatatu ijayo zoezi hilo litaendelea ili kudhibiti
uchafuzi huo wa miundombinu ya barabara.
Alisema wanatakiwa wasijaze
mchanga kwakuwa unaathiri matairi ya magari mengine yanayopita,kusababisha
ajali ,kufukia mifereji na kufuta alama za barabarani na hatimae kuipa mzigo
wakala huo.
Injinia Msangi alisema
lengo ni kuacha kumwagwa mchanga na kufunga matipa ya mchanga kwa ubora ili
kuepusha matatizo na kuiondolea hasara TANROADS.
Aliwataka madereva wa
matipa ya mchanga kuacha kudharau sheria zilizopo ili kuepuka migongano isiyo
na tija.
Awali kamanda wa usalama
barabarani,Abdi Issango ,alifika eneo la tukio na kuzungumza na madereva hao ,uongozi
wa tanroads mkoa,akiwemo kaimu meneja,msaidizi wake pamoja na meneja wa
barabara mkoa mama Urio.
Alisema ni kweli madereva wengi
wamekuwa hawafungi vizuri mchanga kwa kutumia kifungio(hooks)kwenye maturubai
ili kuzuia mchanga usimwagike.
Hata hivyo kamanda Issango,alisema
kwa kushirikiana na wakala wa barabara mkoani humo,wameamua kutoa muda ili
kurekebisha mapungufu yaliyopo ambapo kuanzia jumatatu atakaekiuka maelekezo
yaliyotolewa atalipa faini ya sh.500,000.
Akizungumzia kiwango cha
faini kinacholalamikiwa,alieleza kila idara ina sheria zake, kwa usalama
barabara ukikiuka sheria adhabu yake ni sh.30,000 lakini kwa Tanroads ni
500,000 na kutoingia kwenye mizani faini
zake huwa ni mil.2 .
Baada ya kamanda huyo
kuzungumza na pande hizo mbili ,madereva hao walitawanyika na kuridhia
maelekezo waliyopatiwa sambamba na kukubaliana kuanza kwa zoezi hilo wiki
ijayo.