Random Posts

MTANZANIA ATEULIWA KUSHAURI SEKRETARIETI YA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI


Pichani Luteni Kanali Joseph Bakari (kushoto) akimkabidhi Katibu Mkuu wa Baraza hilo Kanali Dorah Mamby Koita zawadi maalum (plaque) kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis A. Mwamunyange alipowasili rasmi katika Sekretarieti ya Baraza hilo.
 Pichani Kanali Bakari akiwa Meja akivisha Nishani na aliyekuwa Rais wa Baraza  hilo Meja Jenerali Gianni Gola (Italia) kwa kutambua mchango wake katika michezo huko Suriname Paramaribo Amerika ya kusini mwaka 2008.


Waamuzi vijana katika Kituo cha kukuza na kuendeleza michezo cha Twalipo Youth Sports Foundation katika mazoezi.
...................................................................................................................

Sekretarieti ya Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (Conseil International du Sport Militaire/International Military Sports Council -CISM),yenye Makao yake makuu Jijini Brussels Nchini Ubelgiji, imepata nguvu mpya baada ya Mtanzania Luteni Kanali Joseph Peter Bakari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuteuliwa kushikizwa kwenye Sekretarieti ya Baraza hilo kama  Mshauri/ Msaidizi wa Mkurugenzi wa Idara ya Michezo ya Baraza hilo (Advisor/ Special Assistant to the CISM Sports Director). Katika utekelezaji wa majukumu yake  Kanali Bakari anakuwa  chini ya Mkurugenzi Kanali  Carlos Eduardo kutoka Brazil.

Akiongea siku ya kumkaribisha rasmi, Katibu Mkuu wa Baraza hilo Kanali Dorah Mamby Koita kutoka Guinea alisema” Sekretarieti imepokea kwa furaha uteuzi na hatimaye ujio wa Kanali Bakari, kwani binafsi anamfahamu katika utendaji wake kazi hususani kuendeleza na kukuza vipaji vya watoto katika michezo, (Mwaka 2008 nchini Suriname Paramaribo Bodi ya wakurugenzi ya Baraza hili ilimtunikia Nishani  (CISM Order of Merit) iitwayo The Grand Knight kwa kutambua moyo wa kujitolewa, bidii, uaminifu na uadilifu katika kuenenda sambamba na malengo ya CISM katika kuendeleza michezo.) Hivyo ni dhahiri kuwa atakuwa msaada mkubwa katika Baraza hilo Kimataifa”.

Aliongeza kuwa Tanzania imefanya vyema kumshikiza Kanali Bakari kwani hapa ataongeza  uzoefu zaidi ambao atautumia katika kuendeleza tasnia ya michezo Jeshini na kwa Taifa kwa ujumla kutokana na ukweli kuwa Sekretarieti hiyo inaundwa na maafisa wenye uzoefu na taaluma za hali ya juu katika tasnia ya michezo, utimamu wa mwili na viungo na ambao wanatoka kwenye mataifa ambayo yamepiga hatua kubwa katika maendeleo ya michezo kama vile Brazil, Ujerumani, Uhispania n.k”.

Akitoa neno la shukrani Kanali Bakari alisema kuwa amefarijika sana kuwa miongoni mwa watendaji katika Baraza hilo. Aidha, alilishukuru JWTZ na Taifa kwa ujumla kwa kumpa dhamana hiyo ya kimataifa. “  Kwa uwezo wa Mungu ,ni matarajio yangu kuwa nitafanya  kazi kwa weledi mkubwa na moyo wa kujituma ili niweze kuitendea haki nafasi na fursa niliyopewa kwa manufaa ya  Baraza hilo,  JWTZ na nchi yangu ya Tanzania kwa ujumla”. Alisema.

Kanali Bakari ni muasisi wa program ya kukuza na kuendeleza vipaji katika michezo ya Twalipo Youth Sports Foundation inayosimamiwa na JWTZ. Programu hiyo pamoja na kuendeleza vipaji pia ni program ya kwanza nchini kutoa mafunzo ya uamuzi katika mpira wa miguu. Waamuzi hao vijana kwa sasa wanatumika kuchezesha mashindano mbalimbali hadi ngazi ya Ligi Kuu. Frank Domayo wa Azam na Yohana Mkomola wa Serengeti Boys ni miongoni mwa matunda chanya ya programu hiyo.

“CISM” ( International Military Sports Council/ Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani  ni moja kati ya Shirikisho kubwa duniani linalojishughulisha na michezo anuai (multdisplinary).Baraza hilo  linaloundwa na majeshi ya nchi wanachama  134, Tanzania ikiwemo.

Dhima Kuu ya Shirikisho hilo ni kutumia michezo kama njia/zana ya kueneza amani duniani badala ya vita. Hivyo kupitia Shirikisho hilo nchi wanachama zinaaswa na kupewa wito  kuwa yale waliyokuwa wanayafanya katika uwanja wa vita sasa wayafanye katika viwanja vya michezo.

 Shirikisho hilo huandaa mashindano mbalimbali ya michezo. Kwa mwaka huandaa zaidi ya mashindano 20 ya dunia (World Championships), mashindano ya Mabara na kikanda katika michezo zaidi ya 30. Masuala yahusiyo uongozi,  uamuzi, ualimu,  tiba na katazo la matumizi ya nguvu za kusisimua misuli katika michezo ni miongoni mwa mambo muhimu yanayosimamiwa na shirikisho hilo.

Kanali Joseph  Bakari anakuwa ni Mtanzania wa Kwanza kuteuliwa katika sekretarieti ya  Baraza hilo. Anajiunga na waafrika wengine Kanali Dorah Mamby Koita kutoka Guinea na  Kanali Abdulraheem Belo kutoka Nigeria.
Ni matarajio ya wapenda michezo kuwa Kanali Bakari atatoa uwakilishi uliotukuka huko Brussels. Kila la heri!!!