Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama akifyeka wakati wa kufanya usafi ambapo mkoa wa Pwani uliadhimisha kilele cha mbio za mwenge na kumuenzi hayati mwalimu Nyerere kwa kufanya usafi kituo cha afya Mkoani.
(picha na Mwamvua Mwinyi)
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo akichoma uchafu moto Mara baada ya kufanya usafi katika kituo cha afya mkoani ikiwa ni kumuenzi hayati mwalimu Nyerere tangu afariki dunia miaka 17 iliyopita.
Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama akizungumza baadhi ya watumishi na watendaji wa mkoa na wilaya ya Kibaha katika kituo cha afya Mkoani baada ya kufanya usafi kumuenzi hayati mwalimu Nyerere na kilele cha mbio za Mwenge.
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza na baadhi ya watumishi na watendaji wa mkoa na wilaya ya Kibaha katika kituo cha afya Mkoani baada ya kufanya usafi kumuenzi hayati mwalimu Nyerere na kilele cha mbio za Mwenge.
...................................................................
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
VIONGOZI wa mkoa wa Pwani na wilaya ya Kibaha,wameungana pamoja kufanya usafi katika kituo cha afya mkoani,ikiwa ni kumuenzi baba wa Taifa ,hayati mwalimu Nyerere ambae alipenda kuhifadhi mazingira ya nchi.
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo,alisema wameamua kufanya usafi wa mazingira kuenzi azma ya mwalimu aliyoiweka mwaka 1960 baada ya uhuru ambapo alieleza anataka nchi ipambane kikamilifu na maadui watatu ikiwemo maradhi.
Aidha alisema wiki ijayo anatarajia kukutana na mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha na mkuu wa wilaya ya Kibaha kuweka mipango endelevu ya kuweka mji huo safi wakati wakijiandaa mji huo kuwa manispaa.
Mhandisi Ndikilo alisema moja ya vigezo vya mji kuwa manispaa ni lazima uwe safi na wenye mpangilio mzuri wa miundombinu ya majengo na barabara hivyo kuna kila sababu ya kuweka mji katika muonekano bora.
Alieleza kuwa wapo baadhi ya watu wanahofia na tishio la kubomolewa nyumba zao hivyo hawawezi kujenga mji huku wakijia watavunjiwa nyumba na kupata hasara.
Mhandisi Ndikilo aliwatoa hofu hiyo wananchi hao na kudai wiki ijayo watafanya mkutano mkubwa na kuwapa wananchi maelekezo ya serikali kwa namna walivyokubaliana na wizara ya ujenzi na baada ya hapo hakutakuwa na tamko jingine la kuwafanya watu wavunje maeneo yao na kuishi kwa sintofahamu.
Aliitaka jamii kujenga tabia ya kuwa wasafi na kuweka mazingira bora ili kuepukana na magonjwa mbalimbali yanayotokana na uchafu na magonjwa ya matumbo na mlipuko.
Pia aliwaasa vijana kuchota busara na mshikamano kutoka kwa hayati baba wa taifa ili hali kujifunza kutoka kwa kiongozi huyo wa kipekee.
“Tusome machapisho yake,tufuatilieni hotuba zake ili kuendelea kumuenzi na kuyasimamia vilivyo yale aliyoyaamini ikiwemo amani,upendo na mshikamano”alisema mhandisi Ndikilo.
Mhandisi Ndikilo,aliwataka vijana ambao wamekuwa wakiingia katika vishawishi vya namna moja ama nyingine kujaribu kuchezea amani na utulivu kuacha mara moja kwa faida yao na taifa kijumla..
Hata hivyo aliwaomba viongozi wa wilaya,mkoa,watumishimwatendaji na wananchi mkoani humo kuendelea kumuenzi mwalimu Nyerere kwa vitendo iwapo kila mara kwa kukumbuka yale aliyoyapigania na kuyakemea .
Aliwaonya baadhi ya watumishi na watendaji kuachana na tabia ya kuomba rushwa katika majukumu yao ya kazi kwani kwa kufanya hivyo ni kujipalia makaa ya kuwajibishwa endapo watabainika.
“Daima tuendelee kumkumbuka daima kwa uongozi wa mfano na wa kuigwa na mataifa mengine,kwani alifanya mengi na kukemea,rushwa ni namba moja,tukatae rushwa,tujitume na kupenda kufanya kazi”
“Alipinga pia ubaguzi wa kibabila,udini na kusema watanzania wote ni kitu kimoja hivyo haipaswi kubaguana kwa rangi ama mahala ulipotoka”alisisitiza .
Mkuu wa wilaya ya Kibaha,Assumpter Mshama alisema kila mtanzania ana wajibu wa kumuenzi hayati baba wa taifa kwa vitendo kwa kulinda na kuheshimu mazuri aliyoyaacha na kupinga aliyokuwa akiyapinga.
Alisema tayari alishaagiza maeneo yote ya wilaya yahakikishwe yanasafishwa na kusafisha vichaka vyote vilivyokaribu na maeneo ya ofisi mbalimbali.
Assumpter alisema kikubwa wanahitaji mji uwe safi kuanzia katika maofisi na kwenye maeneo yanayozunguka nyumba za watu,kila nyumba kuwa na chanja ya kuanikia vyombo na kujenga vyoo vya kudumu.
Aliwashukuru wananchi kwenda kasi na kupokea maagizo hayo vizuri na sasa maeneo mengi yapo safi licha ya zoezi la kujenga vyoo vya kudumu kutoenda vizuri.
Baba wa taifa alifariki dunia octoba 14,1999 katika hospitali ya mtakatifu Thomas mjini London uingereza hivyo kufikisha miaka 17 sasa tangu kifo chake.
0 Comments