Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza viongozi
wote wa Serikali walioalikwa kuhudhuria sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa
Uhuru kitaifa zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba, 2016 katika Wilaya ya Bariadi
Mkoani Simiyu kutohudhuria sherehe hizo na wale ambao walishalipwa fedha ya
posho na safari kwa ajili hiyo wazirejeshe
Taarifa
iliyotolewa leo tarehe 12 Oktoba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam na Katibu
Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Rais Magufuli ametoa maagizo
hayo ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kubana
matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali nyingi katika shughuli za
maendeleo ya nchi.
Viongozi
waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za kwenda Bariadi ni pamoja na Wakuu wote
wa Mikoa, Wakuu wote wa Wilaya, Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za
Mitaa, Mameya na Wenyeviti wote wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na
Wilaya pamoja na watumishi ambao huambatana nao wakiwemo madereva na wasaidizi
wao ambao kwa idadi hufikia takribani 1,500.
Kwa
kuwa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na Maadhimisho ya
Siku ya Kumbukumbu ya Muasisi wa Taifa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere aliyefariki dunia miaka 17 iliyopita, agizo hilo limewataka
Viongozi wote wa Mikoa na Wilaya kubaki katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea
utaratibu wa jinsi ya kuienzi siku hiyo.
Aidha,
Rais Magufuli ameagiza Wilaya zote ambazo zimefanya vizuri katika shughuli za
maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa
rasmi katika siku ya kilele cha Mbio za Mwenge na kwamba zawadi zilizoandaliwa
zitapelekwa kwa wahusika kwa utaratibu utakaoelekezwa na Mamlaka inayohusika
kutoa zawadi hizo.
Hata
hivyo Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa
Taifa, Viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu na Wilaya zake pamoja na
wananchi wote wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi na kushiriki katika sherehe za kuzima
Mwenge wa Uhuru siku hiyo ya tarehe 14 Oktoba, 2016.
Mgeni
Rasmi katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru atakuwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar
es Salaam
12
Oktoba, 2016