![]() |
| ............................................................................................................... |
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
Mbunge wa jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete,ameitaka jamii hususan vijana kujenga tabia ya kujitolea kuchangia damu ili kusaidia kuokoa maisha ya watu wenye mahitaji hayo katika vituo vya vya afya na hospitali mbalimbali.
Aidha amewahamasisha wanananchi kupima afya zao mara kwa mara kwa lengo la kujua maradhi yanayowakabili na kupatiwa matibabu mapema kabla ya magonjwa kukua na kuleta madhara .
Ridhiwani aliyasema hayo huko Chalinze katika kampeni ya kuchangia damu salama iliyotambuliwa kama " changia damu salama kwa mama na mtoto"ambapo alikuwa ni mgeni rasmi katika kampeni hiyo.
Alisema tatizo la damu ni kubwa na kuna umuhimu wa kuchangia pamoja na kupima afya kila wakati ili kuweza kujikinga ama kutibu magonjwa mapema kabla ugonjwa haujakua.
“Tujitolee damu ndugu zangu kuwa wenye mahitaji ni ndugu zetu,'mama zetu, watoto wetu na watanzania wenginw wenye mahitaji”
“Licha ya kuwa mgeni rasmi lakini siwezi kuja kuangalia watu wakichangia damu wakati mimi mwenyewe ninayo damu ya kutosha kuchangia" ,na nashukuru nimefanikiwa kuchangia kifuko kimoja cha damu”alisema Ridhiwani.
Hata hivyo alieleza kuwa takwimu zinaonyesha kuwa watoto chini ya umri wa miaka mitano mkoani Pwani wako kwenye hatari ya kupoteza maisha kutokana na ukosefu wa damu hivyo kuna kila sababu ya kuokoa maisha ya watoto hao.
Alisema watoto wenye umri huo wamekuwa wakiongoza kwa kukosa damu kutokana kuugua ugonjwa wa malaria lakini pia kucheleweshwa kuwahishwa hospitali mapema.
Ridhiwani alieleza kuwa kundi jingine lililo hatarini ni wakina mama wajawazito ambao nao wamekuwa wakipata tatizo la ukosefu wa damu ama wakihitaji kufanyiwa upasuaji na majeruhi wa ajali.
Katika hatua nyingine mbunge huyo,alikwenda kuangalia hali ya lambo la maji la Pera ambalo limekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa mji wa Chalinze wakati wa shida ya maji.
Ridhiwani alifuatana na mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa chalinze,Hussein Mramba, diwani wa kata ya Pera ,Lekope Lang'wesi, na mwenyekiti wa jumuiya ya wakinamama Esther Laban na viongozi wengine wa kata.
Mbunge alijionea jinsi matope yalivyojaa na ambavyo fedha za Tasaf zilivyotumika na bila mafanikio kuonekana.
Ridhiwani alibali ombi la kwenda kuzungumza na wawekezaji ili kukodi bulldozer litakalosaidia kuchimba lambo upya.
"Ukarabati wa lambo hili unaweza kuwa mwepesi kwa kutumia vyombo vya moto kufukua na kutoa matope na mchanga uliojaa na kulijenga vizuri",mbunge alisema.
Wakati huo huo kufuatilia kuanza kufanyiwa kazi kwa sheria ya Mifugo ya Utambuzi ,( sheria namba 10'/2010) wakina mama wa kifugaji jamii ya kimasai waliamua kutoka makwao na kwenda porini kukusanyika wakifanya mgomo wa kuomba msaada dhidi ya sheria hiyo kandamizi.
Ridhiwani akiambatana na ujumbe huo na mwenyekiti wa chama cha wafugaji walikwenda kukutana nao malengo yakiwa kuwasikiliza kero zao na kushauri .
Katika kikao hicho aakinamama jamii ya kifugaji,walieleza masikitiko yao juu ya sheria inayoelekeza ng'ombe wote katika eneo husika wapigwe chapa na wengine kulalamika hata Ndama wanapozaliwa wanatakiwa kupata vyeti vya kuzaliwa.
Walitaja kero nyingine ni askari sungusungu wanaokama mifugo wakiwa katika maeneo yao ya kuchungwa.
Akijibu kuhusiana na kero hizo ,Ridhiwani alisema atakwenda kushauriana na wenzake bungeni juu ya sheria hiyo ya kupiga chapa .
Aliwaomba wafanye subira ili apate tafsiri kamili ya chapa hizo na alikataa kuamini kuwa chapa hizo zinaletwa kwa sababu serikali inataka kuwanyang'anya wafugaji mifugo yao.
Ridhiwani anaendelea na mikutano na wananchi jimboni hapo kabla hajaelekea dodoma bungeni katika mikutano ya bunge.

0 Comments