WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali tayari imeshalipa sh. bilioni 722.7
kati ya sh. bilioni 964.2 za madeni ya michango ya jumla ambayo Serikali
inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini.
Ametoa
kauli hiyo leo (Alhamisi, Oktoba 20, 2016) wakati akifungua Mkutano wa Sita wa wadau wa NSSF
ulioanza leo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Arusha
na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 600.
Amesema
sekta hiyo imekua kwa asilimia 15 kutoka sh. trilioni 8.9 mwaka 2015 hadi kufikia
sh. trilioni 10.2 mwaka 2016. “Hadi kufikia Juni 2016, takwimu zinaonesha idadi
ya wanachama imeongezeka na kufikia milioni 2.1. Rasilmali za mifuko zimefikia
shilingi trilioni 10.28 na mafao yaliyolipwa kwa kipindi cha mwaka kinachoishia
Juni 2016 ni shillingi trilioni 2.93. Michango ya wanachama kwa mwaka ni
shilingi trilioni 2.15 uwekezaji katika nyanja mbalimbali umefikia kiasi cha
shilingi trilioni 9.29,” ameongeza.
Waziri
Mkuu pia amemuagiza Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Prof. Godius Kahyarara awaandikie
barua waajiri wote wanaodaiwa na shirika hilo na kuwataka wawasilishe fedha
wanayodaiwa mara moja na wale ambao hawatalipa ndani muda utakaowekwa
wafikishwe mahakamani na yeye apewe taarifa.
“Kumekuwepo na changamoto ya muda
mrefu ya baadhi ya waajiri kutolipa michango kwa wakati hali inayoleta usumbufu
mkubwa kwa wanachama hasa wanapofikia muda wa kustaafu. Suala hili
halikubaliki, hivyo natoa maelekezo kwa waajiri wote nchini waheshimu sheria na
wawasilishe michango yao kwa wakati,” amesisitiza.
Mbali ya kuwabana waajiri, Waziri
Mkuu pia amewataka wanunuzi wa nyumba za shirika hilo na wapangaji wote
wanaodaiwa wakamilishe malipo yao na wasipofanya hivyo ndani ya muda uliopangwa
wafikishwe mahakamani.
“Nimeambiwa pia lipo tatizo la
wadaiwa wa nyumba yaani wanunuzi na wapangaji. Suala hili lilitolewa maelekezo
na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu. Nataka
nisisitize kuwa watu wote walionunua nyumba za NSSF na bado hawajakamilisha
malipo na wale waliopanga lakini hawalipi kodi wanatakiwa kulipa haraka au
wakabidhi nyumba hizo kwa NSSF ziuzwe kwa watu wengine, vinginevyo nao
wafikishwe mahakamani.”
Akizungumzia utendaji wa shirika
hilo, Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa shirika hilo na Bodi ya Wadhamini
kwa uamuzi wake wa kuwekeza kwenye uzalishaji wa sukari nchini. Amesema kiwanda kitakachojengwa, kinatarajiwa kutoa ajira
zaidi ya 100,000 kwa Watanzania na hivyo kuongeza wanachama katika mfuko wa
NSSF.
“Nimefurahishwa na uamuzi wa NSSF na PPF kuungana ili
kukabiliana na tatizo la sukari nchini. Tumeelezwa hapa kuwa mashirika haya
yatashirikiana kujenga Kiwanda cha Sukari kitakachozalisha tani 200,000 kwa
mwaka. Kiwanda hicho kitajengwa katika eneo la Mkulazi lililopo mkoani Morogoro,”
amesema.
Mapema, akielezea utendaji kazi wa shirika
hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof. Godius
Kahyarara alisema limeboresha mafao ya wanachama wake kutoka sh. 80,000 hadi
sh. 100,000 kwa mwezi.
Alisema limeanza
kufanya upembuzi yakinifu wa kujenga nyumba za watumishi Dodoma ili kuendana na
uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma. “Upembuzi bado unaendelea lakini
tumeshabaini kuna uwezekano wa kujenga nyumba 200 hadi 300 mkoani Dodoma,”
alisema.
Kuhusu uwekezaji
kwenye ujenzi wa Daraja la Mwalimu Nyerere lililopo Kigamboni, Dar es Salaam,
Prof. Kahyarara alisema uwekezaji huo unalipa kwa sababu makusanyo ya tozo kwa
watumiaji yamefikia asilimia 109. “Tuna uhakika kwamba fedha tulizowekeza
zitarudi,” amesisitiza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amepokea msaada wa tani 45
za saruji ambazo ni sawa na mifuko 900 yenye thamani ya sh. milioni 15 kwa
ajili ya waathirika wa tetememo la ardhi mkoani Kagera. Amepokea msaada huo
kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Prof. Samuel Wangwe.
Akiwasilisha
msaada huo, Prof. Wangwe alisema wameguswa na tatizo lilitokea mkoani Kagera na
wameamua kutoa mchango ili kusaidia juhudi za Serikali kukabiliana na maafa
hayo. Pia alisema wamekamilisha ahadi yao ya madawati 6,000 yenye thamani ya
sh. milioni 400 ambayo waliitoa awali.
Waziri
Mkuu aliwashukuru kwa misaada hiyo na kuwahakikishia kwamba itafikishwa kwa
walengwa.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI,
OKTOBA 20, 2016.
