Katikati ni Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu L. Nchemba (Mb) Akisisitiza jambo wakati akijibu
maswali ya waandishi wa habari kuhusu zoezi la kusajili watumishi wa Uma nchi
nzima. kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angellah J. Kairuki
(Mb) na kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Projest
Rwegasira
Baadhi ya waandishi wa Habari nchini wakisikiliza kwa
makini ufafanuzi unaotolewa na Mawaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora; kuhusu usajili wa Vitambulisho vya Taifa kwa watumishi wa Umma
zoezi linaloendelea nchi nzima
Baadhi ya waandishi wa Habari walioshiriki mkutano wa
tathmini ya mwenendo wa Usajili Vitambulisho vya Taifa kwa watumishi wa Umma;
mkutano uliofanyika ukumbi wa Kambarage, jengo la Hazina Dodoma
Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu L. Nchemba (Mb) akiweka saini kitabu cha wageni
alipotembelea ofisi za Usajili za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa mkoani
Dodoma, kukagua shughuli za usajili Watumishi wa Umma kabla ya kuzungumza na
waaandishi wa habari kutoa tathmini ya mwenendo wa zoezi hilo.
Waziri akipokea maelezo ya namna shughuli za usajili
zinavyo ratibiwa na ofisi ya usajili Wilaya ya Dodoma Mjini ; alipofanya ziara
ya ukaguzi na kukutana na viongozi na watumishi wa Umma waliofika kupata huduma.
...............................................................................................
Serikali imewataka
watumishi wote nchini walioajiriwa na Serikali, yakiwemo mashirika ya Dini na
Taasisi nyingine ambazo haziko kwenye
orodha ya malipo ya mishahara ya Serikali lakini zinapata ruzuku kutoka
Serikalini; kuwa wamesajiliwa katika zoezi
la Vitambulisho vya Taifa kwa Watumishi wa Umma linaloendelea kote
nchini, kufikia Oktoba 31, 2016.
Agizo hilo limetolewa na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Angellah J. Kairuki (Mb)
alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, katika mkutano wa pamoja
ulioitishwa kati ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Waziri ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Bi Kairuki amesisitiza;
“waajiri na watumishi watakaoshindwa kutekeleza zoezi hili watachukuliwa hatua
stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo”
Akifungua mkutano huo
uliolenga kutoa tathmini ya mwenendo wa
zoezi linaloendelea la Usajili wa Vitambulisho vya Taifa kwa Watumishi wa Umma
lilioanza nchi nzima tangu Oktoba 03, 2016, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
Mh. Mwigulu L. Nchemba (Mb) amesema mpaka sasa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imefanikiwa kusajili zaidi ya asilimia 50% ya
watumishi wote nchi nzima na baadhi ya mikoa kukamilisha usajili kwa zaidi ya
asilimia 95%. Ameutaja mkoa wa Geita kuwa mkoa unaoongoza kwa kufanya vizuri
katika zoezi hilo
Amesema pamoja na kuwepo
kwa changamoto mbalimbali zilizokwamisha zoezi hilo kukamilika kwa wakati
uliopangwa; Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, wameamua kuongeza muda wa kukamilisha zoezi hilo kwa wiki
mbili zaidi hadi Oktoba 31, 2016.
Amewataka watumishi
kuondokana na upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya watumishi kwamba zoezi hilo
limelenga kuhakiki vyeti na badala yake wajitokeze kwa wingi kusajiliwa kwani
Serikali imelenga kuunganisha taarifa za mfumo wa mishahawa wa Serikali na NIDA,
ili mbali na kutatua tatizo la watumishi hewa; kupitia mfumo huu wa
kielektroniki unaomtambua mtu kwa alama zake za kibaiolojia kuwa na maslahi
mapana kwa taifa na kwa watumishi; kwa kuunganisha mifumo mingine ya Serikali
ukiwemo mfumo wa Kodi, mifuko ya Hifadhi za Jamii, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya
Juu, Bima ya Afya, Uhamiaji, RITA Na Benki ili kutoa manufaa mapana kwa
mtumishi.
Amelipongeza Jeshi la
Wananchi wa Tanzania kwa kuwezesha kusambazwa kwa vifaa vya usajili nchi nzima,
Ofisi ya Rais TAMISEMI, Taasisi na Mashirika yote ya Serikali waliojitoa
kufanikisha zoezi la Usajili.
Kupitia zoezi la Usajili
Watumishi wa Umma, Tayari NIDA imefungua ofisi za usajili nchi nzima, ngazi ya
Wilaya kusogeza karibu zaidi huduma inayotolewa kwa wananchi. Kwa mujibu wa
Waziri Mwigulu Pindi zoezi la usajili
watumishi litakapokamilika usajili wa wananchi utaanza mara moja nchi nzima
kwani zoezi la usajili vitambulisho vya Taifa limelenga kila mwananchi, Mgeni
anayeishi kihalali nchini na Mkimbizi.





0 Comments