Ziara ya Mfalme wa Morocco nchini Tanzania
Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini kuanzia tarehe 19 hadi 23 Oktoba, 2016.
Madhumuni
ya ziara hiyo ni kukuza zaidi uhusiano kati ya Tanzania na Morocco
hususan katika masuala ya kiuchumi na kibiashara kwa faida ya nchi hizi
mbili na watu wake.
Vilevile,
Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco atatumia fursa ya ziara hiyo
kutembelea Zanzibar na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya
kujionea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Hata
hivyo, ziara hiyo ambayo imejikita zaidi katika kukuza ushirikiano wa
kiuchumi na kibiashara haitaathiri msimamo wa Tanzania katika mgogoro
unaoendelea kati ya Morocco na Sahara Magharibi.
Msimamo
wa Tanzania ambao umekuwa ukisimamiwa na Awamu zote za uongozi
zilizopita na Awamu hii, upo sambasamba na ule wa Umoja wa Afrika (AU)
unaoutaka Umoja wa Mataifa (UN) ambao ndio wamepewa jukumu la kusimamia
mgogoro huo, kuongeza kasi katika kuutatua na kupata suluhu ya kudumu ya
mgogoro huo.
Tarehe
20 Oktoba, 2016 Mhe. Mfalme Mohammed wa VI atakutana kwa mazungumzo ya
faragha na Mhe. Rais Magufuli Ikulu yakifuatiwa na mazungumzo rasmi
kati yao na wajumbe waliofuatana nao.
Mhe. Mfalme Mohammed VI pamoja na kutembelea Tanzania, pia atatembelea Rwanda, Ethiopia na Kenya.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 13 Oktoba, 2016.
0 Comments