Na Shamimu Nyaki-WHUSM
............................................
“Mkataa kwao ni mtumwa”ni msemo ambao una maana kwamba
binadamu ni lazima ujikubali katika kila hali ambayo unakutana nayo katika
mazingira yoyote yale na usikubali binaadamu mwingine akakutawala au
akabadilisha mtazamo wako kwa manufaa yake bali kubali kupokea mawazo
yanayoweza kuboresha kile unachokiamini.
Na
ndivyo alivyofanya Baba wa Taifa letu
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kutumia Kiswahili kama utambulisho wa Mtanzania
popote pale atakapokuwa.
Katika
Historia Lugha ya Kiswahili ilianza takriban miaka 800-1000 iliyopita katika mazingira ya Vituo vya Biashara Ukanda
wa Pwani ambako Wafanyabiashara kutoka Uarabuni, Uajemi na Uhindi walikutana na
wenyeji Waafrika.
Lugha kuu ya Kimataifa ya Biashara wakati huo
ikiwa ni Kiarabu ambapo kutokana na
muingiliano wa watu lugha mpya ilijitokeza wakati wenyeji wa Pwani waliokuwa
wasemaji wa Lugha za Kibantu walipopokea maneno mengi hasa ya Kiarabu katika
mawasiliano yao.
Kiswahili kilikuwa na lahaja nyingi kutokana
na lugha mbalimbali za Kibantu zilizochangia matumizi tangu Karne ya 19 ambapo Kiswahili kilianza kuenea Barani Afrika kwa njia ya
Biashara.
Ni katika kipindi hiki ambapo Mwalimu Nyerere alikuwa katika harakati za kudai Uhuru
wa Tanganyika ndipo alipoamua kutumia lugha ya Kiswahili kama chombo muhimu cha kuwaunganisha watanzania wote kupigania na kudai Uhuru.
Mara baada
ya Uhuru mwaka 1961, Kiswahili kilitangazwa kuwa Lugha ya Taifa. Ambapo Waziri Mkuu wa kwanza wakati ule aliagiza
kuwa Kiswahili kitumike katika shughuli zote za Umma.
Na katika
kutekeleza Agizo hilo, tarehe 10 Desemba
1962, Rais wa Tanganyika wakati huo
akiwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitoa Hotuba ya
Jamhuri kwa Lugha ya Kiswahili. Katika
utetezi huo, hatua ya kwanza ya Mwalimu Nyerere ilikuwa ni usisitizaji wa
matumizi ya Kiswahili kama lugha asilia ambayo raia wa Tanganyika walipaswa
kutumia ili kuelewana ifaavyo, na kuondoa uwezekano wowote wa mafarakano
yanayohusiana na mitafaruku ya kimatamshi.
Na kwa kuweka mfano wa
hatua hiyo, Rais Nyerere alihutubia katika hafla zote rasmi kwa lugha ya
Kiswahili, hivyo basi kuhakikisha kuwa kila raia wa Tanganyika; aliyekuwa na
kisomo au la; alimwelewa, pamoja na mikakati ambayo Serikali yake ilipaswa
kuweka.
La kutia moyo ni kuwa,karibu
asilimia 95 ya wakazi asilia wa Tanganyika, ni wenye asili ya Kibantu, hivyo
mazingira ya usisitizaji wa uzingatiaji wa Kiswahili kuwa lugha unganishi ya
jamii hizo yalifaa.
Hatua ya pili kwa Rais
Nyerere ilikuwa ni upitishaji wa Azimio la Arusha la 1967, aliposema kuwa, “ni
mfumo wa 'Ujamaa’ pekee ambao ungefikia lengo kuu la uuganishaji wa Watanzania
wote”.
Katika hotuba yake,
kiongozi huyo alisisitiza kuwa, ni kupitia kwa Ujamaa pekee, ambapo Waafrika
wangeweza kupambana na falsafa kandamizi za kibepari, akiurejelea mfumo wa
ujima, ambao unawiana moja kwa moja na ujamaa endelevu.
Mwalimu Nyerere pia
alikwepa matumizi ya falsafa ya kikomunisti, hasa kutoka mataifa ya Urusi na
Uchina, kwani yalihusishwa na ukandamizaji wa haki za binadamu.Badala yake,
alisisitiza mfumo wa demokrasia asilia, uliotambua ushiriki wa kila mwanakijijji
bila shaka, mafanikio ya ujamaa yaliendelea kujitokeza kwani kadri vijiji hivyo
vilivyoendelea kukua, kiwango cha elimu kiliendelea kuimarika nchini Tanzania.
Kwa mfano, kwa wakati
mmoja, Tanzania iliorodheshwa nchi iliyokuwa na kiwango kikubwa cha kisomo
barani Afrika (asilimia 83) pamoja na mafanikio makubwa katika sekta ya afya.
Hili liliashiria kuwa,
hakujikita pekee katika uongozi wa kisiasa, lakini katika utetezi wa Kiswahili,
kwani baadhi ya vitabu vyake aliviandika
kwa Kiswahili ili kuwafaa wananchi na kuwafungua macho Watanzania kuhusu ilikokuwa
ikielekea nchi yao.
Kutokana na mchango
huo, ni wajibu wa viongozi wetu wa kisiasa kutambua kwamba mchango wao katika
kuitetea lugha ndiyo utakaowafanya kukumbukwa na vizazi vijavyo.
Uzalendo wa Mwalimu
Nyerere unapaswa kuwa mwanga kwa viongozi wote wa Kiafrika kufahamu kwamba
kutumia Kiswahili ni wino wa kuandika historia.
Mwalimu Nyerere
atakumbukwa kwa kuwa miongoni mwa Waafrika wa kwanza kutafsiri kazi za
Kiingereza kwa Kiswahili.
Juhudi hizo zimeendelea kuonekana kwani
Januari
1967 Agizo jingine lilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais wakati huo Mheshimiwa
Rashidi Mfaume Kawawa kwamba, Kiswahili kitumike katika shughuli zote za
Kiserikali na Kitaifa.
Kuanzia hapo Kiswahili kikawa kinatumika katika
shughuli zote za Nyanja zote hapa nchini
na kimeimarisha mahusiano ya
makabila na kuifanya Nchi ionekane kama ina kabila moja
badala ya makabila takriban 120. Kiswahili kimekuwa Nguzo Imara ya Mshikamano,
Amani, Utulivu na Upendo miongoni mwa Watanzania.
Ama kwa hakika juhudi hizi zimezaa matunda kwa
Watanzania kutokana na umoja uliotakana na juhudi za mwalimu katika kueneza
matumizi ya lugha yetu na ni kutokana na juhudi za viongozi wote wa nchi hii wanavyohimiza kutumia
lugha hii.
Kudhihirisha hilo Rais wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya
Kikwete katika hotuba yake kwanza aliyoitoa Bungeni baada ya
kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Disemba 2005 alisema
“Lugha ya Kiswahili imeanza kupata umaarufu Afrika na duniani”.
Umoja wa Afrika umekubali Kiswahili kuwa moja ya lugha zake kuu. Aidha Nchi za
Kanda ya Maziwa Makuu zimekubali kutumia na kuendeleza lugha ya Kiswahili.
“Serikali
ya Awamu ya Nne itahakikisha kuwa juhudi hizi zinaendelezwa na kuhakikisha kuwa
lugha ya Kiswahili inakua nje ya mipaka ya Afrika”.Alisema Mhe. Kikwete.
Hizi ni jitahada kubwa sana zilizofanywa na ambazo
zinaendelea kufanywa na Serikali katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakuwa
kwa kiasi kikubwa.
Kipo
chombo Muhimu kilichopewa dhamana ya kuendeleza na kukuza lugha hii kwa ubora
zaidi ambacho ni Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ambalo lipo chini ya Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
liliundwa chini ya sheria namba 27 ya Bunge ya mwaka 1967 kukuza na kuendeleza
matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika Tanzania,kushirikiana na taasisi nyingine
ndani ya Jamhuri ya Muungano ambazo zinahusika na kukuza Kiswahili na
kuratibu kazi zao,kukuhamasisha matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika shughuli
rasmi na za umma.
Mafanikio
haya ya matumizi ya Kiswahili yamesaidia sana kukuza na kuendeleza lugha ya
Kiswahili kwani Hata Rais wa Awamu ya Tano Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli yupo
mstari wa mbele katika kutumia lugha hii ya Kiswahili katika hotuba zake na
dhifa mbalimbali za Kitaifa Mfano ni wakati alipokutana na Waziri Mkuu wa India
Mhe.Narendra Modi tarehe 29 mwezi Agosti 2016.
Watanzania
wote tunapaswa kujivunia juhudi hizi na tuwe mstari wa mbele kuendelea
kukitumia Kiswahili kama utambulisho wetu ili kueneza utamaduni wa nchi yetu.

0 Comments