Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka akipima
kipimo cha shinikizo la damu wakati alipotembelea banda la Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya kwenye maonesho ya Wiki ya Vijana yanayoendelea mkoani humo.
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,
Imanuel Amani akitoa elimu kwa wananchi waliofika bandani hapo kujua huduma
zinazotolewa na Mfuko.
Maofisa wa NHIF wakiendelea na kuwahudumia
wananchi waliofika bandani hapo.
Wananchi
wakiendelea na upimaji wa huduma za afya ndani ya banda la NHIF.
Wananchi wakisubiri kupata huduma ya kupima afya
zao.
Huduma za upimaji zikiendelea
Wananchi mkoani Simiyu wakiwa na hamu ya kupata
huduma za upimaji
Wananchi wakijisajili kwa ajili ya kupata huduma
ya upimaji.
..................................................................................................................................
Na Grace
Michael, Simiyu
HUDUMA za
upimaji afya bure zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwenye
Maadhimisho ya Wiki ya Vijana yanayokwenda sambamba na tukio la uzimaji Mwenge
zimekuwa kivutio kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Mfuko unatoa
huduma za vipimo vya shinikizo la damu, kiwango cha sukari, uzito na urefu
lakini pia mwananchi anayepima anapata fursa ya kupata elimu ya namna ya
kujikinga na maradhi yasiyoambukiza kwa kuzingatia mtindo bora wa maisha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti bandani hapo,
wananchi hao wamesema, kitendo kilichofanywa na Mfuko cha kusogeza huduma hiyo
mkoani humo ni nzuri kwa kuwa inawapa fursa ya kujua hali ya afya yao.
“Kwa kweli
niwapongeze sana kwa huduma hii ambayo mnatupima bila ya kutoa gharama yoyote
lakini kitu kizuri Zaidi ni kupata elimu ya namna ya kuishi ili kuepukana na
maradhi ambayo yanaweza kuepukika kwa kuzingatia ushauri wa wataalam ambao leo
tunaupata bila gharama yoyote,” alisema Bw. Maduhu Sita mkazi wa Bariadi.
Akizungumzia
mwitikio wa wananchi bandani hapo ambao wanafika kwa lengo la kupata huduma ya
vipimo, Meneja wa NHIF Mkoa wa Shinyanga na Simiyu Bw. Imanuel Amani alisema
kuwa mwitikio wa wananchi ni mkubwa sana.
“Mwitikio
kwa kweli ni mkubwa sana nah ii inaonesha tu kwamba wananchi wanataka kujua
hali ya afya zao na kwa upande wetu NHIF tupo tayari kuwahudumia hawa wananchi
kwa kadri itakavyowezekana hivyo hata ambao hawajafika hapa waje ili
tuwahudumie,” alisema.
Alieleza
kuwa mbali na upimaji wa afya, Mfuko pia unatumia nafasi hiyo kuwahamasisha
wananchi kujiunga na huduma zake ili wawe na uhakika wa kupata matibabu wakati
wowote. “Kwa sasa NHIF imepanua wigo wake ambapo makundi mbalimbali
yanaruhusiwa kujiunga na huduma zake yakiwemo makundi ya wajasiliamali, watoto,
wanafunzi, watu binafsi hivyo nawaomba wananchi wafike bandani kwetu ili
tuwahudumie,” alisema Bw. Amani.







