TANGAZO KWA UMMA
BENKI YA TWIGA KUANZA KUTOA HUDUMA
NOVEMBA 8, 2016
Kwa mamlaka
iliyopewa kisheria kupitia kifungu namba 58(2) (a) na (b) cha Sheria ya Mabenki
na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu inapenda kuutarifu umma kwamba zoezi
la tathmini ya hali ya kifedha ya Twiga Bancorp Ltd (Twiga) limekamilika; kwa
mantiki hiyo, Twiga itaanza kutoa baadhi huduma za kibenki kwa umma kuanzia
Jumanne tarehe 8 Novemba 2016. Huduma hizo ni pamoja na ukusanyaji wa marejesho
ya mikopo ya wateja. Meneja Msimamizi wa benki hiyo atawajulisha wateja huduma
zitakazotolewa na taratibu za kuzingatia.
Benki Kuu ipo
katika mchakato wa kupitia na kuchambua njia mbadala za kutatua tatizo la mtaji
linaloikabili Twiga Bancorp. Njia inayopewa kipaumbele ni kutafuta mtaji kutoka
kwa wawekezaji wapya, mchakato utakaowahitaji kuchambua hali halisi ya taarifa
za hesabu za Twiga (due diligence). Zoezi hili linatarajiwa kuchukua takribani wiki
tatu na litakapokamilika, Benki Kuu itaingia makubaliano na wawekezaji wapya
kuhakikisha wanaingiza mtaji unaohitajika haraka iwezekanavyo ili shughuli za
kawaida za kibenki ziweze kuendelea.
Benki ya Twiga
itaendelea kuwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu hadi hapo utaratibu wa
kuwamilikisha wawekezaji wapya utakapokamilika.
Benki Kuu ya
Tanzania ilitangaza kuiweka Twiga Bancorp Ltd chini ya usimamizi wake kuanzia tarehe
28 Oktoba 2016 kutoka na upungufu mkubwa wa mtaji unaoikabili.
Benki Kuu ya
Tanzania inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye
amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.
BENKI KUU YA TANZANIA
6 Oktoba 2016

0 Comments