Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
Mkutano
wa Tano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeishauri Serikali
kutosaini Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi Kati ya Jumuiya ya
Nchi za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU) – (EPA) kwa
kuwa hauna manufaa kwa nchi ya Tanzania.
Ushauri
huo umetolewa leo mjini Dodoma na wabunge wa Bunge hilo baada ya kuujadili
mkataba huo kwa kina kwa kutoa maoni yao ambapo wengi wameunga mkono kutosainiwa
kwa mkataba huo.
Baadhi
ya wabunge waliopata nafasi ya kutoa maoni yao katika mjadala huo ni Mbunge wa
Mtwara Vijijini(CCM) Mhe. Hawa Ghasia amemshauri Mhe. Rais Dkt .John Pombe Magufuli
kutosaini mkataba huo kwa kuwa mkataba huo una hasara nyingi kwa taifa kuliko
faida.
”Kwa
kuzingatia mkataba umeruhusu uingizaji na utoaji wa bidhaa huru na ukizingatia hakuna
nchi hata moja ya Ulaya ambayo Tanzania inapeleka bidhaa zake hivyo mkataba huu
hauna maslahi kwa watanzania”, alisema Mhe. Ghasia.
Ameongeza
kuwa Tanzania sio nchi ya kwanza kutosaini mkataba huo kwani kuna nchi kama Angola,
Nigeria, na Gambia hazijasaini,ameongeza kuwa kama Tanzania itakubaliana na mkataba
huo utaua viwanda pamoja na biashara za Tanzania.
Kwa
upande wake Mbunge wa Nzega Mjini Hussein Bashe amesema kuwa tatizo lililopo
katika mkataba huo ni kutoitambua nchi kama nchi na badala yake kuangalia nchi
zote kwa pamoja hivyo amewashauri wabunge kuhoji kuanzia kwenye kiini cha
tatizo.
“Kwa
kuwa kifungu cha 143 cha mkataba huo kinaruhusu kupeleka marekebisho, naishauri
Serikali yetu ipeleke marekebisho ya kupendekeza kila nchi iingie mkataba
kivyake kulingana na maslahi ya nchi yake”, alisema Bashe.
Aidha,
Mbunge wa Mwibara (CCM) Mhe.Kangi Lugola amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kukataa
kusaini mkataba huo kwani ni miongoni mwa mikataba mibovu kati ya mikataba
iliyowahi kuletwa nchini kutoka katika nchi za Ulaya.
“Kama
tukikubali kusaini mkataba huu nchi hii itakuwa dampo la bidhaa mbalimbali za
ajabu kutoka nje na hivyo kupelekea kushindwa kutimiza dhamira ya nchi ya
kuimarisha viwanda vyetu”, alisema Mhe. Lugola.
Naye,
Mbunge wa Mchinga (CUF) Mhe. Hamidu Bobali amesema kuwa mkataba huo haufai kwa
maslahi mapana ya taifa hili kwani unataka kuondoa ushuru kwa bidhaa
zinazoingia nchini wakati nchi ya Tanzania inaingiza bidhaa nyingi kutoka nje
kuliko kupeleka bidhaa nje ya nchi.
“Kama
tukikubali tukaondoa ushuru wa kuingiza bidhaa kutoka nje basi tutapoteza
mapato mengi yanayotokana na kuwepo kwa bandari pia tunatakiwa tujiulize kama
mkataba umeruhusu uingizaji na utoaji wa bidhaa huru je nchi yetu ina bidhaa
zinazokidhi vigezo vya kuingia katika nchi za Ulaya?” , alihoji Mhe. Bobali.
Mhe.
Bobali ametoa rai kwa Serikali kuileta Bungeni mikataba mikubwa kama ya gesi na
madini kwa ajili ya kujadiliwa kwa kina ili kuepuka kusaini mikataba isiyo na
tija kwa Taifa.

0 Comments