Random Posts

VIONGOZI WA SERIKALI WASHAURIWA KUTUMIA NDEGE ZA ATC

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu akionyesha mfano wa hati ya safari ya kuelekea Mwanza kupitia Shirika la ndege la Tanzania (ATCL), kushoto kwake ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akipokea maoni kutoka kwa wasafiri wanaotumia usafiri wa anga katika uwanja wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNIA) wakati alipokagua utoaji wa huduma uwanjani hapo.
  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu akiongea na waandishi wa habari kabla ya kufanya ziara ya kikazi mkoani Mwanza kupitia Shirika la ndege la Tanzania (ATCL), leo jijini Dar es salaam.

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akipokea maoni kutoka kwa wasafiri wanaotumia usafiri waa anga katika uwanja wa kimataifa wa Julius Nyerere wakati alipotembelea kukagua huduma zitolewazo uwanjani hapo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la ndege Tanzania (ATCL) Eng. Ladislaus Matindi  akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wakati alipotembelea Uwanja wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNIA) kukagua huduma zitolewazo uwanjani hapo.
................................................................................................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muunngano wa Tanzania Bi Samia Suluhu  amewasihi viongozi wa serikali na  wananchi kutumia ndege za Shirika la Ndege Tanzania(ATC) ili kudumisha uzalendo na kuchangia pato la shirika hilo kwa lengo la kuhimili ushindani na kukuza uchumi wa nchi.

Ametoa rai hiyo jijini Dar es salaam alipopewa hati ya kusafiria kupitia ndege za shirika hilo wakati akisafiri na ujumbe wake kuelekea mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi.

“Napenda kutoa wito kwa viongozi wa Serikali na wananchi kwa ujumla kutumia ndege zetu ili shirika letu lifanye kazi vizuri zaidi, kufanya hivi kutaongeza pato na kukuza uchumi wa nchi ”, amesema Makamu wa Rais.

Ametanabaisha kuwa kwa kutumia ndege za Shirika la ATC kwa safari za ndani Serikali itaokoa fedha nyingi zinazotumika kwa kukodi ndege za mashirika binafsi.

“Mimi na ujumbe tumeamua kusafiri na ndege za shirika la ndege Tanzania kutokana na kubana matumizi, gharama tuliyotumia  kwa safari hii ni shilingi  Milioni saba na laki sita ambapo tungekodi ndege binafsi tungetumia milioni arobaini”, amefafanua Makamu wa Rais.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amempongeza Makamu huyo kwa kitendo cha uzalendo alichokionyesha na kutaka viongozi wengine wa Serikali na wananchi kwa ujumla kuiga mfano huo ili kuliinua shirika hilo na kuongeza uchumi.

“Nampongeza Makamu wa Rais kwa kuamua kutumia ndege za Shirika hili kwa safari za ndani, kitendo hiki kimeonesha nia ya dhati ya serikali ya kulifufua shirika hili, naomba wananchi nao waendelee kutumia ndege za shirika hili katika safari zao za ndani kama alivyofanya Makamu wa Rais”, amesema Waziri Mbarawa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Mhandishi Ladislaus Matindi ameahidi kuboresha huduma katika shirika hilo ikiwemo mifumo ya kukatisha tiketi ili kurahisisha utoaji wa huduma na kuvutia wateja wengi kwa lengo la kurudisha hadhi ya shirika.
“Tumeshaanza mchakato wa kuweka mfumo mpya  wa kukatisha tiketi ikiwemo kwa njia ya kielektroniki kupitia tovuti ya shirika hili ambapo mteja hatalazimika kufika kwenye ofisi zetu”, amesema Mhandis Matindi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Post a Comment

0 Comments