![]() |
| ........................................................................................................................................ |
Na Eleuteri Mangi,
MAELEZO, Dodoma
Watumishi wa Umma 1,663
kutoka Wizara, Idara zinazijitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za
Mikoa, na Mamlaka za Serikali za Mitaa wamechukuliwa hatua za kinidhamu baada
ya kubainika kusababisha watumishi hewa 19,629 hadi Oktoba 25, 2016.
Waziri ya Nchi, Ofisi
ya Rais, anayeshughulikia Utumishi na Utawala Bora Angella Kairuki amesema hayo
leo Bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mainda Hamad Abdallah (Mbunge
wa Viti Maalum) alilohoji hatua zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya watumishi
wanarudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Akifafanua idadi
hiyo, Waziri Kairuki amesema kuwa idadi ya watumishi waliochukuliwa hatua za
kinidhamu kutoka Wizara mbalimbali ni 16, Idara zinazijitegemea na Wakala za Serikali
watumishi tisa, Sekretarieti za Mikoa watumishi sita na Mamlaka za Serikali za
Mitaa watumishi 1,632.
Waziri Kairuki amesema
kuwa watumishi hao wameisabishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 19,
huku Halmashauri ya Kinondoni ikiwa na watumishi hewa 107 ambao waligharimu Serikali
sh. bilioni 1.29, Kishapu watumishi 73 wamesababisha hasara ya kwa kugharimu sh.
milioni 543 na kuonya kuwa waajiri waendelee kuchukua hatua za haraka na
kudhibiti uwepo wa watumishi hewa ili kuipunguzia Serikali kuingia hasara kubwa
badala ya kuwahudumia wananchi.
Aidha, Waziri Kairuki
amesema kuwa jumla ya watumishi 638 wamefunguliwa mashtaka polisi, watumishi 50
wanafanyiwa uchunguzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na
watumishi 975 mashtaka yao yamefikishwa kwenye Mamlaka zao za kinidhamu.

0 Comments