NAHODHA
wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, John Bocco
‘Adebayor’, amewatakia mashabiki wa timu hiyo kheri ya mwaka mpya ‘2017’
unaoanza leo saa 6.00 usiku huu huku akiwashukuru kwa sapoti yao
waliyoionyesha mwaka huu.
Bocco ametoa kauli hivi karibuni mara baada ya kumalizika kwa mchezo
uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) dhidi ya Tanzania Prisons
walioifunga bao 1-0, huku akifanikiwa kutupia bao hilo pekee
lililorudisha morali ndani kikosi hicho baada ya kutofanya vizuri kwenye
mechi mbili za ufunguzi wa mzunguko wa pili walipocheza ugenini na
African Lyon (0-0) na Majimaji (1-1).
“Kwanza tunawashukuru mashabiki wetu kwa uvumilivu waliouonyesha, kwa
sapoti waliotupa katika kipindi chote kigumu tulichopitia, kama
wachezaji na timu kwa ujumla tunawaomba waendelee kuwa na moyo huo huo
na pia tunawatakia kheri ya mwaka mpya (2017) na wamalize mwaka huu
vizuri, tuendelee kuwa pamoja ili kuisaidia timu yetu iweze kufanya
vizuri,” alisema Bocco wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz
Bocco ambaye ameipatia mafanikio makubwa Azam FC kwa mabao yake
muhimu tokea timu hiyo ikiwa madaraja ya chini hadi kupanda Ligi Kuu
mwaka 2008, aliendelea kusema kuwa wamepitia changamoto nyingi sana kwa
mwaka huu unaoisha huku akidai kuwa wamejifunza kupitia hayo na
wanachoangalia kwa mwaka mpya ni kuipeleka mbele zaidi timu hiyo ili
kufikia mafanikio.
“Changamoto zilikuwepo nyingi na ni sehemu ya maisha, sisi kama timu
tunajua mpira unachangamoto zake na tumezipokea kama binadamu na sisi
wachezaji changamoto iliyokuwa katika kazi yetu haikuwa ndogo na
tunamshukuru Mungu kwa kuweza kutusaidia tumeweza kupigana nazo na
hatukuweza kukata tamaa, kikubwa tunachofanya hivi sasa ni kuangalia
mbele zaidi ili kuipatia timu mafanikio kwa mwaka unaokuja,” alisema.
Azam FC mbali na kuwa bingwa mtetezi wa michuano ya Klabu Bingwa ya
Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), inamaliza mwaka huu ikiwa
imefanikiwa kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho
Afrika mwakani pamoja na taji la Ngao ya Jamii baada ya kuichapa Yanga
kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90
za mchezo huo uliofungua pazia la ligi msimu huu.
Ujio wa Mapinduzi Cup
Wakati kikosi cha timu hiyo kikielekea mchana wa leo Jumamosi
visiwani Zanzibar kwenda kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, Bocco
amesema kuwa wao kama wachezaji wanaenda kushindana na hatimaye kurejea
na ubingwa wa michuano hiyo.
“Mashindano ya Mapinduzi si mageni kwa Azam FC, michuano hiyo si
mepesi ni migumu, sisi kama wachezaji tunaenda kushindana naamini ni
sehemu moja ya msimu huu ambayo tukiweza kuchukua kombe itakuwa ni
faraja kwa klabu na mashabiki wetu pamoja na sisi wachezaji, tukitoka
huko hata tukirudi kwenye ligi tutakuwa na morali nzuri ya kuendeleza
ushindi kwenye ligi, michuano ya FA na Kombe la Shirikisho Afrika,”
alimalizia Bocco.
Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola kinachosisimua
mwili na kuburudisha koo pamoja na Benki ya NMB, inaenda huko ikiwa na
kumbukumbu nzuri ya kulitwaa taji hilo mara mbili (2012,2013), ambapo
itaanza kufungua dimba Jumatatu ijayo kwa kuvaana na Zimamoto saa 10.15
jioni.
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii wapo Kundi B pamoja na timu nyingine za Yanga na Jamhuri.

0 Comments