
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Askofu Mkuu wa kanisa la
EAGT, Dkt. Brown Mwakipesile kabla ya kupokea msada wa shilingi milioni
10 uliotolewa na kanisa hilo kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani
Kagera. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye makazi ya Waziri Mkuu
jijini Dar es salaam Desemba 22, 2016.
............................................................................................................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea fedha taslimu sh. milioni 10 kutoka
Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) zikiwa ni msaada kwa
ajili ya watu waliopatwa na maafa kutokana na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Makabidhiano ya mchango huo yamefanyika leo mchana (Alhamisi, Oktoba 22,
2016) kwenye Makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi mchango huo, Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dk. Brown
Mwakipesile amesema kanisa hilo limeona lina wajibu wa kuisadia Serikali kuwapunguzia
machungu watu waliopatwa na maafa kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea
mkoani Kagera, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17.
“Tumeona ni vema kanisa la EAGT lishiriki kuisadia Serikali kuwafariji
wananchi waliopata maafa kutokana na tetemeko hilo. Tumeona ni wajibu wetu kwa
sababu waliopatwa na maafa ni watu wetu wote. Tunawaombea wote waliopatwa na
shida waweze kupata nafuu mapema zaidi,” amesema.
Askofu Mkuu Dk. Brown ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa
kusimamia vema suala hilo tangu lilipotokea hadi sasa na kuongeza kuwa
wanamuomba Mwenyezi Mungu awape nguvu viongozi wa Serikali ya awamu ya tano ili
waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo.
“Ukiacha hili la tetemeko, tumeona jinsi Serikali ilivyosimamia vizuri suala
la madawati hadi sasa kuna baadhi ya maeneo wamevuka hadi malengo. Tunamshukuru
Mheshimiwa Rais Magufuli na Serikali nzima kwa kusimamia jambo hilo vizuri,”
amesema.
Amesema kanisa hilo linatoa shukrani nyingi kwa Mheshimiwa Rais Dk. John
Pombe Magufuli kwa jitihada zinazofanywa na Serikali yake kukabili mambo
mbalimbali yanayowagusa wananchi walio wengi.
Akitoa shukrani kwa Baba Askofu Mwakipesile na viongozi wa kanisa hilo
aliombatana nao, Waziri Mkuu ameahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo
inafikishwa Kagera kwa walengwa. “Nawashukuru sana kwa jinsi mlivyoguswa na
kuamua kuwachangia wenzetu waliopatwa na maafa, tutahakikisha inawafikia
walengwa,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema anawashukuru sana viongozi wa dini zote kwa jinsi wanavyoisadia Serikali
kuwahudumia wananchi kupitia sekta mbalimbali. “Tunatambua juhudi zinazofanywa
na taasisi za dini zote kuunga mkono juhudi za Serikali, tunafarijika mno na
tunawashukuru sana,” ameongeza.
Amemuomba
Askofu huyo pamoja na viongozi wengine wa dini wawaombee kwa Mungu viongozi
waliopo madarakani ili awape hekima na busara na awawezeshe kuwaongoza vema Watanzania.
Tetemeko
hilo la ardhi liliharibu miundombinu ya barabara, shule, zahanati na kujeruhi watu
440. Pia lilisababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika
hali hatarishi na 9,471 zikipata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315
wakihitaji misaada mbalimbali.


0 Comments