Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
.............................................
BAADA ya mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,kutoa agizo la kukamatwa kwa uongozi wa kampuni ya ALPHA CHOICE LTD na KAASAL COMMODITIES LTD kutokana na kukiuka mkataba wa mnada wa korosho msimu huu ,makampuni hayo yamelipa kiasi cha fedha ili kujinasua katika agizo hilo..
Viongozi wa makampuni hayo wameanza kulipa fedha ambayo walidaiwa kushindwa kulipa kwa wakati zaidi ya sh.bil 5.794 za mnada huo.
Mhandisi Ndikilo,akizungumza na waandishi wa habari juu ya jambo hilo alisema,viongozi hao wamelipa baadhi ya fedha ambazo walikuwa wakidaiwa na wakulima wanyonge wa korosho mkoani hapo.
Alieleza kampuni ya ALPHA CHOICE ltd imekamilisha malipo ya kiasi cha sh.bil .4,202,514,402 ilizokuwa ikidaiwa.
Aidha kwa upande wa kampuni ya KAASAL COMMODITIES ltd imelipa sh.mil.342,200,768 ambapo awali ilikuwa ikidaiwa bil.1,591,608,288.
Mhandisi Ndikilo alisema kwamba kwasasa kampuni ya KAASAL COMMODITIES bado inadaiwa kiasi cha sh.bil.1,298,407,520 huku ikiahidi kumalizia deni hilo desemba 19 mwaka huu.
Kufuatia kampuni hiyo kushindwa kukamilisha deni lake zuio la kusafirisha korosho zake za Mtwara lipo pale pale na litaendelea hadi hapo itakapokamilisha deni .
Hata hivyo kutokana na kampuni ya ALPHA CHOICE ltd kulipia deni lake mkuu wa mkoa huyo ameiruhusu kuchukua korosho zilizokuwa kwenye maghala na kusafirisha.
Mhandisi Ndikilo,alizikumbusha kampuni hizo na nyingine zinazonunua korosho mkoani Pwani,kuheshimu mikataba ya ununuzi wa korosho inayowekwa.
“Nazishukuru kampuni hizo kwa kutii agizo langu na kulitekeleza kwa muda mfupi lakini haifai kushurutishwa kwa mambo ambayo yanakwenda kimikataba namna hii’
“Haipaswi kuvutana wakati sheria na taratibu zinajulikana,hawa wakulima wanatumia nguvu zao kupambana na umaskini sasa ikitokea watu wachache wakawahujumu inakuwa haina tija katika mustakabali mzima wa maisha yao”alisema mhandisi Ndikilo.
Wiki iliyopita mkuu wa mkoa wa Pwani,aliyakalia kooni makampuni hayo mawili kwa kuamuru viongozi wa kampuni hizo wakamatwe na kufunguliwa mashtaka kwa kushindwa kufuata makubaliano ya mkataba wa mnada wa mwaka huu .
Sambamba na agizo hilo alimuomba mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego kuzuia korosho zilizonunuliwa na makampuni hayo hadi pale watakapolipia korosho walizonunua mkoani Pwani.
Taratibu za makubaliono ya minada zinamtaka mnunuzi akishinda zabuni aandae malipo ndani ya siku saba.
0 Comments