Beki wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC,
Shomari Kapombe, akimiliki mpira mbele ya Abdallah Kheri, wakati wa
mazoezi ya mwisho ya timu hiyo leo asubuhi kujiandaa na mchezo wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es
Salaam dhidi African Lyon kesho Jumapili.
Mshambuliaji wa Azam FC, Yahaya Mohammed, akifumua shuti wakati wa mazoezi hayo.
Wachezaji wa Azam FC wakifanya mazoezi ya kusafa wakati wa mazoezi hayo.
Kipa wa Azam FC, Aishi Manula, akiokoa mchomo kwenye mazoezi ya timu hiyo.
..............................................................................................................................
Category:
Team:
Azam FC
BAADA
ya maandalizi ya takribani wiki tatu, hatimaye Klabu Bingwa ya Afrika
Mashariki na Kati Azam FC, kesho inatarajia kufungua pazia la mzunguko
wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kukipiga dhidi ya
African Lyon, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam saa
10.00 jioni.
Azam FC itaanza ngwe hiyo ikiwa na nguvu mpya kabisa baada ya kufanya
usajili mzuri kwenye dirisha dogo la usajili, kwa kuongeza sura mpya
tano pamoja na kumrejesha winga wake, Enock Atta Agyei, aliyekuwa kwa
mkopo Medeama ya Ghana ilipomsajili, na sasa ataanza kuonekana katika
mechi za ligi mara baada ya kutimiza miaka 18 Januari 5 mwakani.
Wachezaji wapya watano waliosajiliwa na Azam FC kwenye dirisha dogo
ni beki Yakubu Mohammed (Aduana Stars, Ghana), kiungo mkabaji raia wa
Cameroon, Stephan Kingue Mpondo (Coton Sports, Cameroon), winga Joseph
Mahundi aliyerejea nyumbani (Mbeya City, huru) na washambuliaji Samuel
Afful (Sekondi Hasaacas, Ghana), Yahaya Mohammed (Aduana Stars, Ghana).
Kikosi cha Azam FC kilichomaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kikiwa
nafasi ya tatu kwa pointi 25 tofauti ya pointi 10 dhidi ya vinara Simba
(35), kimeonekana kurejea na ari ya juu na morali kubwa kuelekea
mzunguko wa pili kutokana na kiwango bora na hali ya kupambana
wanayoonyesha kwenye maandalizi mazoezini.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz
mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben
Hernandez, alisema wamejiandaa vema kuelekea mchezo huo pamoja na
mzunguko wa pili wa ligi kiujumla kutokana na nguvu mpya walizoziongeza
kikosini.
“Kiufupi raundi ya pili tumejiandaa na timu inanguvu mpya ya
wachezaji tuliowasajili ambao hawakuwepo raundi ya kwanza hata mazoezi
jinsi yanavyoendelea na jinsi wachezaji wanavyoonekana tunaamini kwa
raundi ya pili tutaanza katika mazingira mazuri kuliko ambavyo tulikuwa
tukifanya mzunguko wa kwanza,” alisema.
Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, alisema kuwa
wanaingia kwenye raundi ya pili wakijua kuwa kutakuwa na ushindani
mkubwa, lakini amekipanga kikosi chake kufanya vizuri huku akiwaambia
mashabiki wa Azam FC waendelee kuisapoti timu hiyo.
“Mashabiki waendelee kutusapoti tunajua kwa namna tulivyokuwa
tukicehza mzunguko wa kwanza ilikuwa ni ngumu kwao, lakini si kwa wao tu
bali ilikuwa kwa watu wote, kwa kile ambacho naweza kuwaambia wajaribu
kutuvumilia, mpira tutakaokuwa tunacheza na matokeo tutakayokuwa
tunayapata mzunguko wa pili, wenyewe watakuwa wakiyapenda na hawatajutia
kabisa kuchagua na kuisapoti Azam FC,” alimalizia.
Rekodi zao (Head To Head)
Agosti 21 mwaka huu, timu hizo zilikutana katika mchezo wa raundi ya
kwanza, uliokuwa ni wa tano kihistoria kukutana kwenye ligi, ambapo
uliisha kwa matokeo ya sare ya bao 1-1, Lyon ikitangulia kufunga kupitia
kwa Hood Mayanja kwa mpira wa kona wa moja kwa moja kabla ya nahodha
John Bocco ‘Adebayor’, kufunga bao zuri la kusawazisha mwishoni mwa
mtanange huo.
Mpaka sasa katika mechi hizo tano walizokutana, Azam FC imeshinda mara tatu, Lyon mara moja huku mchezo mmoja wakienda sare.
Katika mechi zote hizo, Azam FC ndio iliyofunga mabao mengi zaidi
ikitupia saba katika lango la wapinzani wao hao, huku Lyon yenyewe
ikitingisha nyavu za matajiri hao mara nne tu.




0 Comments