Random Posts

MBUNGE RIDHIWANI KIKWETE AMEPONGEZA JITIHADA ZINAZOENDELEA KUBORESHWA MRADI WA MAJI WA WAMI


Na Mwamvua Mwinyi


MBUNGE  wa   jimbo la  Chalinze Ridhiwani  Kikwete  amepongeza  jitihada   kubwa  zinazofanywa na  wataaluma  wa Halmashauri ya  Chalinze  katika  kuboresha  mradi  wa maji wa Wami  ambao utawezesha kuondoa kero ya maji jimboni hapo.

Akizungumza  baada ya  kutembelea  mradi  huo ,Ridhiwani  alisema  mradi  huo ambao  ulianzishwa na aliyekuwa  mbunge  wa jimbo   hilo  Dkt  Jakaya  Kikwete  ambae  ni rais mstaafu  wa awamu ya  nne ni  mmoja kati ya  miradi bora  iliyoleta  ukombozi mkubwa wa  upatikanaji  wa  maji safi na  salama kwa wananchi wa  mji  wa Chalinze .

Hivyo  alisema  lengo la  kufanya  ziara  katika eneo la mradi huo ni  kuona  shughuli mbali mbali  zinazofanywa na wataalam kwa  ajili ya  kuendelea  kuboresha  mradi huo ili kuwawezesha  wananchi  wake  kupata  huduma ya  uhakika ya maji  safi  na  salama .

" Mradi   huu  ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa  jimbo la hili,nichukue fursa ya  kuwapongeza wataalam  wa halmashauri kwa  kazi  nzuri  wanayoifanya  ya  uboreshaji wa mradi huu" alisema  Ridhiwani. 

Alieleza  amefurahishwa na  jitihada  zinazoendelea  kufanywa na  wataalam  wa  Halmashauri hiyo  kuhakikisha  wananchi  wanapata  maji .
Ridhiwani alifafanua  kazi yake akiwa ni mwakilishi  wa  wananchi ni  kuendelea  kuisimamia  serikali  kwa  kuwawakilisha wananchi  wake bungeni.

  Ridhiwani aliwataka  wananchi  kuendelea  kutunza  miundo mbinu ya maji  ili  kuwezesha mradi  huo  kuendelea kuwa  msaada  kwao.

Mradi huo utakapokamilika utakuwa umetatua tatizo kubwa la ukosefu wa maji kwa wananchi hao.

Post a Comment

0 Comments