Random Posts

MWAKYEMBE AMPONGEZA MAKONDA KWA MPANGO WA KUWASAIDIA WANANCHI WA DAR ES SALAAM KUPATA MSAADA WA HUDUMA ZA KISHERIA NA HAKI ZAO KWA WAKATI

 Waziri wa Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe amemtembelea mkuu wa mkoa wa Dar es salaam na kumpongeza kwa kitendo chake cha kuwasaidia wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kupata huduma za msaada wa kisheria na mpango wa kujenga mahakama 20 mpya ili kuhakikisha huduma za upatikanaji wa haki kwa wananchini zinaimarika na kupatikana kwa wakati.
 Waziri Dkt Mwakyembe ametoa pongezi hizo alipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda ofisini kwake jijni Dar es salam wakati viongozi wa Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria walipomtembelea ili kumpongeza na kuuunga mkono jitihada  za Mkuu wa Mkoa katika kuhakikisha wananchi wa Dar es salaam wanapata haki zao kwa wakati.
 “Mhe Mkuu wa Mkoa nimekuja hapa hii leo na timu yangu kukupongeza na kukuonyesha kwamba tunakuunga mkono na tuko pamoja kuhakikisha upatikanaji haki na huduma za masaada wa kisheria kwa wananchi vinapatikana kwa wakati,” alisema Dkt Mwakyembe na kuongeza kuwa kitendo cha kusikiliza matatizo ya wananchi na kuwasaidia kama ulivyofanya ni cha aina yake na kwa hilo mimi binafsi na viongozi wenzangu tunakupongeza sana na nikuhakikishie kwamba tunakuunga mkono na tuko pamoja katika hili,” alisema Dkt Mwakyembe


Akizungumza katika kikao hicho Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria Prof Sifuni Mchome amesema wizara imenufaika sana na ziara ya Mkuu wa Mkoa ambayo ilimpatia fursa ya kusikiliza kero na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi na kuonyesha kuwa wanachi wengi wanahitaji msaada wa huduma za kisheria ili kupata haki zao kwa wakati.
 Amesema ziara hiyo imesaidia kuangalia utendaji wa eneo la sekta ya sheria na utoaji haki kwa ujumla kufuatia malalamiko mengi yaliyotolewa na wananchi na kubaini kuwa hitaji la msaada wa huduma za kisheria kwa wananchi wa mkoa wa Dar es salaam pia ni kubwa kama ilivyo mikoani na hivyo ni muhimu kulizingatia.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akizungumza katika kikao hicho amesema uongozi wa mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo  wanatarajia kujenga Mahakama mpya 20 kuanzia mwaka 2017 ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa mahakama mkoani humo kwakuwa mkoa una mahakama za mwanzo 12 wakati mahitaji halisi ni mahakama 102. 
Mhe Makonda amesema uamuzi wa kujenga mahakama hizo unaenda sambamba na mpango wa kujenga vituo vya polisi katika kila kata ambao ulisaidia kugundua kuwa ili haki itendeke tena kwa wakati kwa wananchi watakaopelekwa katika vituo hivyo vya polisi ni lazima kuwe na mahakama zaidi ili kufanikisha mpango wa upatikanaji haki kwa wakati .

Ameiomba Wizara kupitia Mahakama ya Tanzania kuwapatia maeneo kjama wanayo na vigezo vya namna mahakama zinavyotakiwa kuwa kama vipo ili kujenga mahakama zitakazokidhi viwango na hivyo kuwafanya watendaji wa mahakama hizo kutoa huduma bora kwa wananchi.

Amesema ziara aliyoifanya mkoani hivi karibuni ilimpatia fursa ya kusikiliza kero za wananchi na kugundua kuwa wananchi wengi wanakabiliwa na changamoto ya kutopata haki kwa wakati na uelewa mdogo wa namna ya kupata haki zao hali ambayo inawasababisha wengi wao kukosa haki zao kwa wakati na kuongeza kuwa kama kiongozi ameamua kulivalia njuga suala hilo ili kuwapunguzia wananchi kero hiyo.


Amesema mpaka sasa anao vijana 35 ambao ni wahitimu wa degree ya Sheria ambao wamepatiwa mafunzo maalum na mwanasheria wa mkoa na atawasambaza vijana hao katika wilaya zote za mkoa ili kuwahudumia wananchi kwa kuwaptia msaada wa huduma za kisheria na hivyo kuwaondolea changamoto ya kupeleka mahakamani kila kitu na pengine hata kukosa haki zao kwa kutojua namna ya kushughulikia mambo yao kwa mujibu wa sheria.

Post a Comment

0 Comments