*Aja nchini kwa dharura kutoka masomoni Uingereza ili kumuwahi Waziri Mkuu
.......................................................................................................................
MBUNGE wa jimbo la Arumeru Mashariki, Mheshimiwa
Joshua Nassari amepongeza na kusifu jitihada kubwa zianazofanywa na Serikali ya
Awamu ya Tano katika kuwaletea maendeleo wananchi wa maeneo mbalimbali nchini
wakiwemo wa jimbo lake.
Kufuatia
hatua hiyo Mheshimiwa Nassari ameahidi kushirikiana bega kwa bega na Serikali ili
kuhakikisha maendeleo yanakuwa endelevu.
Mheshimiwa
Nassari ametoa pongezi hizo leo (Jumapili, Desemba 18, 2016) mbele ya Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa katika majumuisho ya ziara yake ya siku 10 ya
kikazi mkoani Arusha.
Mbunge
huyo ambaye alilazimika kuja nchini kwa dharura akitokea masomoni nchini Uingereza
ili kumuwahi Waziri Mkuu, amesema ameridhishwa na hatua za utatuzi wa migogoro
ya ardhi zinazochukuliwa na Serikali.
Amesema
ziara ya Waziri Mkuu mkoani Arusha, imesaidia kutibu majeraha na makovu makubwa
yalitokana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana."Kama kuna kiongozi
ambaye hawezi kuunga mkono jitihada hizi za kuwaletea maendeleo watu wetu, atakuwa
na matatizo,” amesema.
Ameongeza
kuwa kitendo cha Waziri Mkuu kuweka mikakati ya kushughulikia migogoro ya ardhi
iliyodumu kwa miaka mingi ni ushahidi tosha kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria
kuwasaidia wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa
Nassari amesema mwaka 1952 wazee wa Meru walimtuma mtu kwenda Uingereza kuomba
uhuru wa wananchi wa Arumeru ili waweze kujitawala na kumiliki ardhi yao kutoka
kwa wakoloni.
Amesema
wazee hao walichukua uamuzi huo baada ya kuchoshwa na vitendo vya unyanyasaji
vilivyokuwa vinafanywa na wakoloni dhidi yao. Lakini miaka 55 imepita tangu
nchi ipate Uhuru bado migogoro na mateso hayo yapo.
Hivyo
amempongeza Waziri Mkuu kwa kuamua kuitafutia ufumbuzi changamoto ya ardhi
wilayani Arumeru jambo ambalo litawawezesha wananchi kupata ardhi kwa ajili ya
kuendesha shughuli zao za kimaendeleo zikiwemo za kilimo na ufugaji.
Waziri
Mkuu jana (Jumamosi, Desemba 17, 2016) alifanya ziara katika wilaya ya Arumeru ambapo
alisema Serikali itawanyang’anya ardhi wamiliki wote wa mashamba makubwa
wilayani Arumeru ambao hawajayaendeleza kwa sababu wamekiuka mkataba wa
umiliki.
Alisema
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi
atakuja mkoani Arusha kwa ajili ya kufanya mapitio ya mashamba yote makubwa
ambayo hayajaendelezwa na kuyarudishwa Serikalini.
“Tufanya mapitio ya kila shamba ili kujua
linamilikiwa na nani na alipewa lini na tangu alipokabidhiwa amefanya nini.
Shamba lisiloendelezwa litarudisha kwa wananchi. Kama mtu ameshindwa kupata
mtaji kwa muda wa miaka 10 atapata leo,” amesema.
Amesema
Serikali haiko tayari kuona wananchi wakinyanyaswa kwa kukosa ardhi ya kilimo
kwa sababu ya watu wachache kumiliki maeneo makubwa bila ya kuyaendeleza..
"Ninataarifa
kwamba hapa Arumeru kuna baadhi ya wawekezaji wanamiliki mashamba makubwa na hawajayaendeleza.
Wengine wanakodisha kwa wananchi ili kujipatia fedha kinyume na mikataba yao ya
umiliki. Hatutawavumilia,” alisema.
Alisema
wilaya ya Arumeru inaongoza kwa migogoro ya ardhi na maeneo mengi yametwaliwa
na mtu mmoja mmoja na baadhi yao wamekuwa wakilitumia vibaya Jeshi la Polisi
kwa kuwanyanyasa wananchi wanaokatiza au kulima kwenye maeneo hayo, ambapo
aliwataka polisi kuacha tabia hiyo mara moja.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, DESEMBA 18, 2016.
0 Comments