Random Posts

NDIKILO- JAMII ISHIRIKIANE NA POLISI KUPAMBANA NA UHALIFU PWANI

MKUU wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,akizungumza jambo,wakati wa sherehe ya kuwaaga baadhi ya wastaafu wa jeshi  la  polisi mkoani humo.

(picha na Mwamvua Mwinyi)
............................................................................................................................

Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

MKUU wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo ,amewataka wananchi kushirikiana na jeshi  la  polisi ,kuwafichua watu wasio wema ili kupambana na uhalifu mbalimbali ikiwemo mauaji,uporaji na kitumia silaha.

Aidha ametoa rai kwa jeshi la polisi mkoani Pwani,kufanya kazi kwa uadilifu ili kuhakikisha wanasimamia jukumu lao la ulinzi wa raia na mali zao.

Mhandisi Ndikilo ,aliyasema hayo,wakati wa sherehe ya kuwaaga wastaafu wa jeshi hilo, ambao wamestaafu kazi kwa mujibu wa sheria baada ya utumishi wao jeshini kukoma.

Alisema kuwa kila mmoja ndani ya jamii ana jukumu la kushirikiana na polisi katika kutoa taarifa yoyote yenye lengo la kufichua wahalifu pasipo kuwaachia askari pekee.

Mhandisi Ndikilo ,alieleza kwamba polisi wanawajibu wa kulinda raia na mali zao lakini jamii inawajibu wa kujenga umoja wa kutoa taarifa pale kwenye utata ama kushuku kama kuna watu ama matukio yanayotishia amani.

"Askari wanapaswa kukabiliana na makundi ya uhalifu wanaotumia silaha ili kwa wale wanaofikiri wanaweza kuvunja sheria ndani ya mkoa wakomeshwe"
"Na nyie wananchi tusaidieni kushirikiana na vyombo vya dola kupambana na majambazi,waporaji na watumia silaha  kwani kwa kufumbia macho mambo haya  huleta madhara makubwa" alisema mhandisi Ndikilo.

Hata hivyo mhandisi Ndikilo, aliwasisitiza polisi kuwadhibiti wauzaji na watumiaji dawa za kulevya, wavunja sheria za usalama barabarani na wanaosafirisha binadamu mkoani hapo.

Alihimiza amani na utulivu hasa nyakati hizi  za kuelekea kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka.
“Endapo mkoa utakuwa na amani na utulivu na polisi kukabili uhalifu mtavutia wawekezaji katika kipindi hiki cha kuielekeza Pwani na nchi kuwa ya viwanda,” alisema mhandisi Ndikilo.
Alisema kuwa ofisi yake itashirikiana bega kwa bega na jeshi la polisi katika mapambano dhidi ya uhalifu ili kuufanya mkoa kuwa salama na kuwavutia wawekezaji.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Boniventure Mushongi alisema wastaafu hao wawe mabalozi wazuri kwa kuishi kwa utii na nidhamu waliyolelewa walipokuwa wakifanya kazi kwenye jeshi .
Nae mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia kamishna Msaidizi Athuman Mwambalaswa alisema,askari waliopo kazini wanapaswa kupokea maelekezo wanayopewa na viongozi wao.
Alifafanua kuwa amefanya kazi kwa kipindi cha miaka 42 na hakuwahi kuwa mtovu wa nidhamu ambapo sasa anaona fahari kumaliza muda wa kulitumikia jeshi bila ya kuwa doa.
Mstaafu mwingine Rajab Msangi aliwaasa askari kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea bali wasome alama za nyakati katika kulitumikia Taifa.
Msangi aliwataka askari kufanya kazi kwa kasi iliyopo ili kutekeleza kauli mbiu ya Serikali ya Hapa Kazi Tu ili kufanikisha kuleta maendeleo ya nchi kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments