Random Posts

RC NDIKILO ABAINI WANAFUNZI HEWA 89 SHULE YA SEKONDARI KILANGALANGA

WANAFUNZI wa shule ya sekondari Kilangalanga wilaya ya Kibaha Vijijini mkoani Pwani wakionekana kumsikiliza mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza shuleni hapo.

 (Picha na Mwamvua Mwinyi)

..................................................................................................................

Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, amefanya ziara ya kushtukiza katika shule ya sekondari ya Kilangalanga na kubaini wanafunzi hewa 89 na upotevu wa fedha za serikali zaidi ya sh.mil 30 .
Aidha ametoa siku saba ya kufanyika uchunguzi kwa mkuu wa shule hiyo, afisa elimu halmashauri ya Kibaha na mkoa na atakaebainika kuhusika na udanganyifu huo atachukuliwa hatua zinazostahili.
Hayo yalijiri katika ziara yake ya kushtukiza aliyoifanya shule ya sekondari Kilangalanga na Ruvu Station zilizopo Mlandizi.
Mhandisi Ndikilo, alisema fedha hizo zimedaiwa kupotea kwa kipindi  cha mwaka mmoja baada ya kubainika  uwepo wa jumla ya wanafunzi hewa  89 wa bweni shuleni hapo.
Alieleza kuwa fedha hiyo ni ile inayotolewa na serikali kupitia mpango wake wa elimu bure nchini kwa shule za sekondari na msingi.
"Shule hii imekuwa ikipewa pesa zaidi tofauti na idadi halisi ya wanafunzi 219 wa kidato cha tano na sita huku takwimu ambayo imekuwa ikipelekwa hazina ni wanafunzi 308"alifafanua.
Alieleza lengo kuu la ziara yake ni kuhakiki uhalisia wa idadi ya  wanafunzi kama ina uwiano na  takwimu  anazopelekewa ofisini na watumishi wa idara ya elimu.
Mhandisi Ndikilo alisema kuwa kasoro nyingine aliyobaini ni tofauti ya idadi ya wanafunzi wa O level ambao takwimu za ofisi ya elimu ya mkoa  inasema wapo wanafunzi 784 huku ya mkuu wa shule ikieleza wapo wanafunzi 829 ikiwa na tofauti ya wanafunzi 45.
Akiwa shule ya sekondari Kilangalanga alimuomba mkuu wa shule hiyo, Albert Mabiki ampatie taarifa ya wanafunzi waliopo  shuleni hapo na kugundua takwimu kukinzana na aliyopatiwa na idara ya elimu mkoa.
Mhandisi Ndikilo alilazimika kuomba  apatiwe Vitabu vya mahudhurio ya wanafunzi na kumtaka mkuu huyo wa shule awaite wanafunzi  wote wasimame nje ya madarasa yao na kuwafanyia uhakiki.
Alitoa rai kwa walimu mkoani hapo kutojiingiza kwenye mchezo wa kuongeza idadi ya wanafunzi na endapo watabainika hatowafumbia macho.
"Msijihusishe kabisa na mchezo huo, ni kama wizi, epukeni kushirikishwa na walimu wakuu kuongeza idadi atakaehusika atawajibishwa "alibainisha.
Nae mkuu wa shule ya sekondari ya Kilangalanga, Albert Mabiki, akijielezea alisema, fedha zilizozidi walizilipia madeni ya shule.
Kufuatia majibu hayo, mkuu wa mkoa mhandisi Ndikilo alisema ni kinyume na utaratibu na kuhoji kwanini hakusema mapema kama wanaopokea kiasi kikubwa cha fedha.

Post a Comment

0 Comments