Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard
Kalemani, akizungumza jambo wakati wa Mkutano
wake na wananchi wa Kijiji cha Kishuro,Kata ya Ngenge Wilaya ya Muleba,
Mkoa wa Kagera. Dkt.Kalemani amefanya ziara Wilayani humo ya kukagua Mradi
utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili na kueleza mipango ya Serikali
kutekeleza Awamu ya Tatu ya mradi husika.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard
Kalemani, akizungumza jambo wakati wa Mkutano
wake na wananchi wa Kata ya Ngwanseri,wilaya ya Muleba, wakati wa ziara
yake ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhandisi Richard Ruyango,akizungumza jambo wakati wa
ziara ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard Kalema ni kukagua
utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili.Wengine katika picha ni baadhi ya
Viongozi wa Halmashauri hiyo,Wataalam kutoka
Wizara ya Nishati na Madini, REA,TANESCO, na Wakandarasi wanaotekeleza
mradi husika.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard
Kalemani, (Wa tatu kushoto) katika picha
ya pamoja na Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, Prof.Anna Tibaijuka (wa pili
kushoto),Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhandisi
Richard Ruyango,(wan ne kushoto)pmoja na Wataalam kutoka Wizara ya
Nishati na Madini, REA,TANESCO, na Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa REA Awamu ya Pili.
Mmoja wa Wananchi katika akiuliza jambo wakati wa
mkutano wa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.Medard Kalemani(hayupo pichani)
katika Kata ya Ngwanseri.
Wananchi wa Kata za Ngwanseri na Ngenge wakimsikiliza
Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Dkt.Medard Kalemani na ujumbe wake wakati wa
ziara yake a kukagua utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili wilayani Muleba.
Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini Prof.Anna Tibaijuka (kulia) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Dkt.Medard Kalemani ( katikati) mara baada ya kumaliza mkutano wake na wananchi wa Kijiji cha Kishuro. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhandisi Richard Ruyango.
Wananchi wa Kijiji cha Kishuro Wilaya ya Muleba,
wakisoma Jarida la Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakati wakimsikiliza Naibu
Waziri wa Nishati na Madini,Dkt.Medard Kalemani (hayupo pichani) akieleza utekelezaji
wa Mradi wa REA Awamu ya Pili na mipango ya Serikali ya kutekelza REA Awamu ya
Tatu.
.................................................................................................
Na Asteria
Muhozya, Muleba
Imeelezwa kuwa, Serikali imepanga kutumia Nguzo
za Zege katika utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji
Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, unaotarajia kuanza kutekelezwa kuanzia mwezi Januari, 2017 chini ya Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Hayo
yamebainishwa kwa nyakati tofauti na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt.
Medard Kalemani wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa REA Awamu ya Pili katika Kata za Ngenge na
Ngwanseri, Wilayani Muleba Mkoani Kagera, pamoja na kueleza mipango ya Serikali
katika utekelezaji wa mradi husika Awamu ya Tatu.
Dkt. Kalemani
amesema kuwa, lengo la kutumia nguzo
hizo za zege ni kutokana na uimara wake utakaowezesha upatikanaji umeme wa uhakika na kuepuka
kuchomwa na kuongeza kuwa, tayari nguzo hizo zimeanza kutumika katika Mkoa wa
Kilimanjaro.
Akizungumzia
utekelezaji wa REA Awamu ya Pili, amesema Serikali imetekeleza mradi huo kwa
kasi kubwa kutokana na dhamira yake ya
kuhakikisha kuwa, ifikapo mwaka 2025
asilimia 75 ya Watanzania wawe wameunganishwa
na nishati hiyo ambayo ni kichocheo cha shughuli za kiuchumi.
“ REA awamu ya
pili imekamilika kwa kiwango kikubwa. Vipo baadhi ya vijiji havijafikiwa
kutokana na dosari ndogo ndogo lakini tutavikamilisha kuwezesha utekelezaji wa
Awamu ya Tatu. Hata katika Wilaya hii vipo
na tayari nimemwelekeza Mkandarasi kukamilisha kazi hiyo
haraka,”amesisitiza Dkt. Kalemani.
Akielezea
mipango kwa Awamu ya Tatu, amesema kuwa, Serikali imelenga kuhakikisha kuwa,
awamu hiyo inavifikia vijiji vyote ambavyo havikuunganishwa katika Awamu ya
Pili, visiwa vyote, Taasisi mbalimbali, Sehemu zinazotoa Huduma za Kijamii
zikiwemo za Afya, shule na visima vya
maji.
Aidha, alisema
kuwa, kukamilika kwa utekelezaji wa Miradi
Ujenzi wa njia za Kusafirisha umeme wa
Msongo Mkubwa wa kV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga kupitia Dodoma na
Singida kutawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika pamoja na kuchochea uchumi
wa viwanda hususan katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Wakati huo huo,
Dkt. Kalemani ametumia fursa hiyo kuzitaka Halmashauri zote nchini kushirikiana
na TANESCO kuweka utaratibu shirikishi
ambao utawawezesha wananchi kupata huduma za kuunganishiwa nishati hiyo kupitia
utaratibu wa kuanzisha madawati ya TANESCO katika maeneo yatakayotambuliwa ili
kuwawezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi.
“TANESCO na
Halmashauri, pangeni namna ya kuwawezesha wananchi kufikiwa kwa urahisi na huduma za kunganishwa nishati ya umeme. Mkubaliane
kupanga siku maalum ambayo wananchi watahudumiwa. Serikali inataka kila
mwananchi apate umeme, hivyo tuweke utaratibu ambao utarahisisha na kuwezesha
azma hiyo kufikiwa kwa haraka,” amesisitiza Dkt. Kalemani.
Pia, Dkt.
Kalemani amewataka Wakandarasi wote wakati wa utekelezaji wa miradi ya Awamu ya
Tatu kuhakikisha kuwa, wanajitambulisha katika Halmashauri na Mamlaka nyingine
ili waweze kutambulika ili kuepusha udanganyifu.
Vilevile, Dkt.
Kalemani ameitaka TANESCO kuwaidhinisha Wakandarasi wote watakaofanya kazi ya
‘wiring’ katika nyumba za wananchi katika utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu
ikiwemo kutoa orodha zao ili kuwapunguzia wananchi kero ikiwemo kuwaepusha na
utapeli unaofanywa na baadhi ya wasiowaaminifu.
Akizungumzia
Sekta ya Madini, Dkt. Kalemani amewahamasisha wachimbaji wadogo wadogo kujiunga
katika vikundi ikiwemo kujisajiri katika
Ofisi za Madini zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la
kuwawezesha wachimbaji hao kuomba ruzuku kupitia vikundi pindi zinapotolewa na Serikali.
Katika ziara ya
kutembelea Kata hizo, Dkt. Kalemani ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Muleba,
Mhandisi Richard Ruyango, Wataalam
kutoka Wizara ya Nishati na Madini, REA, TANESCO na Wakandarasi wanaotekeleza
mradi wa REA Awamu ya Pili Wilayani humo.








0 Comments