Na Is-haka Omar, Zanzibar.
.........................................
ZAIDI ya shilingi milioni 43
zimetumika kununua vifaa mbali mbali vya
Jimbo la Chumbuni Zanzibar, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Viongozi
wa jimbo hilo kwa wananchi katika
Kampeni za Uchaguzi uliopita.
Akisoma Risala katika hafla
fupi ya kukabidhi vifaa hivyo, Abrahman Abass alisema vifaa hivyo vimetolewa na
viongozi wa jimbo hilo ambao ni Mbunge, Mwakilishi na Madiwani.
Alivitaja vifaa vilivyotolewa kuwa
ni Gari moja aina ya Canter, Dawa za binadamu kwa ajili ya vituo vya Afya vya
jimbo hilo pamoja na jezi za mpira wa miguu kwa timu za jimbo zenye usajili wa
ZFA.
Alisema tangu viongozi hao
waingie madarakani kwa kipindi cha miezi 14 kwa mbunge na miezi minane kwa
Mwakilishi na Madiwani tayari
wameshatumia zaidi ya milioni 205 katika utekelezaji wa miradi mbali mbali
ndani ya jimbo hilo.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa
wananchi mbali mbali wa Chumbuni, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar Vuai Ali Vuai aliwasihi wafuasi wa Chama hicho na wananchi kwa ujumla kuunga
mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na viongozi hao.
Alisema endapo wananchi wa
Jimbo la Chumbuni wataendelea kushirikiana na viongozi wao vizuri jimbo hilo litakuwa miongoni mwa majimbo ya kuigwa
kimaendeleo hapa nchini.
Vuai ambaye pia ni Mlezi wa Jimbo hilo
alisema Chama hicho kwa
sasa kinahitaji viongozi imara na wabunifu wenye uwezo wa kutekeleza kwa
vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2015/2020 bila ya kusukumwa kwa lengo la kutatua changamoto
zinazowakabili wananchi.
“ Suala la maendeleo halina
Chama wala kabila kwani misaada inayotolewa na viongozi wetu wa jimbo hili na
mengine naamini wanaonufaika ni wananchi wote na sio Wana CCM pekee, hivyo
tuwaunge mkono juhudi zao na kuthamini na kutunza vifaa wanavyotoa ili viweze
kudumu kwa muda mrefu.
Pia wananchi nakukumbusheni kuwa
juhudi hizi ni matunda ya Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyofanywa na wazee wetu
kwa lengo la kutuweka huru ili tujitawale na kutengeneza miundombibu imara ya maendeleo ya nchi yetu.”, alifafanua Vuai
na kuwataka viongozi hao kuendelea kutoa misaada mbali mbali ya kimaendeleo
kadri hali za kiuchumi zitakavyoruhusu ili wananchi waweze kunufaika na fursa
hizo.
Aidha alipongeza viongozi hao
kwa utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho kwa wananchi na kuongeza kuwa
wametekeleza kwa vitendo matakwa ya Katiba ya CCM.
Hata hivyo aliwasihi vijana, wanawake na wazee wa
jimbo hilo kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi ya
Zanzibar yaliyofanyika mwaka 1964.
Pamoja na hayo alitoa ahadi ya
shilingi milioni moja kwa Vikundi mbali mbali vya ujasiriamali vya jimbo hilo
ili ziweze kuwasaidia katika harakati zao za kimaendeleo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo
hilo, Ussi Salum Pondeza “Amjadi” alisifu ushirikiano uliopo baina yake na
viongozi wengine wa Jimbo hilo na kuahidi kuwa wataendelea kuwatumikia wananchi
kwa ufanisi zaidi.
No comments:
Post a Comment