*Asema atafuatilia ajue kwa nini kuna tozo kwenye maghala
ya Serikali
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali haitavumilia kuona mamia ya vijana waliofaulu mitihani ya darasa la
saba na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanabaki nyumbani eti kwa kuwa
hakuna madarasa ya kutosha.
“Serikali haitaridhika kuona vijana
waliofaulu vizuri wanashindwa kwenda kidato cha kwanza. Halmashauri zilijua tangu
mapema ni wanafunzi wanaenda shule za msingi kwa hiyo inataka kuona wote
waliofaulu wanakwenda sekondari kwa asilimia 100,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana wakati
akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Lndi mara baada ya kupokea
taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo wilayani Nachingwea. Waziri Mkuu
amewasili wilayani Nachingwea akiwa njiani kuelekea Ruangwa kwa mapunziko ya
mwisho wa mwaka.
Amesema Serikali ya awamu ya tano
imedhamiria kutoa elimu ya bure kwa kila mtoto sasa iweje watoto wengine
wanafaulu na wanashindwa kujiunga na elimu ya sekondari. “Tumesema elimu ni
bure hakuna sababu ya kufanya wengine wasiende shule wakati azma ya Serikali ni
kutoa elimu ya bure. Hakikisheni wote wanaingia katika chaguo la kwanza,”
amesema.
Amewataka Wakuu wa Wilaya na
Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo zimefaulisha wanafunzi lakini hazina madarasa
na madawati ya kutosha warudi mezani na kujipanga upya ili kuhakikisha
wanafunzi wote waliofaulu wanapangwa na kuanza na wenzao katika chaguo la
kwanza kwani wakisubiri chaguo la pili wanakuwa wamechelewa.
“Kama tumepokea vijana wengi kwenye
udahili wa kidato cha kwanza, ni dhahiri kuwa ,tutapata Vijana wengi
watakaomaliza kidato cha nne. Sote tunajua kuna agizo la kila tarafa kuwa na
sekondari moja ya kidato cha tano na sita, nataka utekelezaji wa agizo hili
usimamiwe kuanzia sasa.”
“Tafuteni moja kati ya shule kwenye
tarafa zenu na ipandishwe hadhi kwa kuwekewa miundombinu inayotakiwa ya bwalo, jiko,
mabweni, mifumo ya maji, madarasa na vyoo vya kutosha,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema atafuatilia ili abaini ni kwa nini
taasisi ya maghala ya Serikali inadai tozo kwa wakulima wanaohifadhi mazao
kwenye maghala hayo.
Waziri Mkuu amesema atapitia sheria
ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ili kuona kama inaruhusu tozo hizo na kuangalia
sheria gani inawaruhusu kutoza kodi. Alihoji inakuwaje taasisi ya Serikali inatoza
tozo kwenye maghala ambayo yamejengwa na wananchi.
Akitoa mfano
kuhusu ghala la Liwale, Waziri Mkuu amesema: “Kuna viagency vimeanzishwa kazi
yao ni kutoza mapato tu. Inakuwaje kunakuwa na taasisi imekaa tu na kuanza
kutoza tozo kwa wananchi wanaotumia facility za Serikali. Sheria ya kutoza tozo
imetokana na nini na hizo zinakwenda kwa nani, je srikali imeanza kufanya
biashara?,” alihoji.
“Nimepata
taarifa kuwa walikuja kuzuia mazao yasitoke hadi wao walipwe, hapana huu siyo
utaratibu. Ni kwa nini tuwanyang’anye fedha wale waliojenga ghala? Wao
walijenga ghala kutokana na ubunifu halafu unasema unawapa sh. 7/- kwa kilo
wakati wewe umetoza sh.25/- kwa kilo moja. Hapana hilo halikubaliki,” amesisitiza.
Waziri Mkuu
amesema kama Serikali inaruhusu kuwepo kwa tozo hizo kwa jambo ambalo wananchi
wamelibuni wenyewe, basi ilipaswa kudai kodi na hiyo kodi ilitakiwa kukusanywa
na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na siyo vinginevyo.
Waziri Mkuu
amesema atafuatilia wakala mbalimbali walioanzishwa kwenye wizara kwani kuna
nyingine zinafanya kazi ambazo zilistathili kufanywa na idara kwenye wizara
mama.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, DESEMBA 27, 2016.
0 Comments