Wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM Mji wa Kibaha, wakimsikiliza katibu wa chama hicho Kibaha Mjini, Abdallah Mdimu.
(picha na Mwamvua Mwinyi)
........................................................................................
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Chama Cha Mapinduzi (CCM)Kibaha mjini,mkoani Pwani,kimesema wakati chama kikielekea kwenye chaguzi mbalimbali ,wanaCCM wajipange kuchagua wagombea wanaokubalika na wananchi na wawajibikaji.
Aidha kimesema ushindi mkubwa uliopatikana katika uchaguzi mdogo uliopita uwe somo kuwa chaguzi bila rushwa inawezekana .
Mwenyekiti wa chama hicho mjini Kibaha, Maulid Bundala, alisema hayo katika kikao cha halmashauri kuu ya CCM mjini hapo, kilicholenga kumpongeza Ramadhani Bogas kwa kushinda udiwani kata ya Misugusugu.
Alisema matokeo ya ushindi huo nchini,ni mafunzo tosha ndani ya chama.
"Wakati tukielekea kwenye uchaguzi wa chama kuanzia ngazi ya chini, tunapaswa kuweka watu wanaokubalika katika jamii, wenye moyo wa kufanya kazi "
"Tubadilike wakati wa kubeba mizigo umepitwa ,tuchague wenye kukipenda na kuweza kukitumikia chama pasipo kununua uongozi "alisema Bundala.
Kwa mujibu wa katibu wa CCM Mjini Kibaha, Abdallah Mdimu,kama chaguzi zote zingekuwa zinafanyika hivyo basi CCM itaendelea kushika dola miaka mingi ijayo.
Alisema uchaguzi huo ulikuwa mwepesi kwani wagombea waliowekwa walikubalika na wananchi.
Mdimu alisisitiza umoja ,mshikamano na kuondoa makundi ambayo wakati mwingine husababisha kuvuruga upatikanaji wa ushindi.
Katibu mwenezi wa CCM Mkoani Pwani, Zainab Gama, alimpongeza Bogas kwa ushindi aliokipatia chama .
Zainab alimuomba diwani huyo, kusimamia ilani ya chama cha mapinduzi na kutembelea wananchi ili kujua kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Kwa upande wake Bogas, alishukuru jumuiya zote na chama kijumla kupigana kwa umoja kupata ushindi huo.
"Nawashukuru wananchi wote bila kujali itikadi za kisiasa kwa kunipigia kura, naomba tufanye kazi kwa lengo la kupiga hatua kimaendeleo "alisema Bogas.
Katika uchaguzi mdogo kata ya Misugusugu Ramadhani Bogas (CCM) alipata kura 1,307, Gasper Ndakidemi (Chadema) 926 na CUF 56.

0 Comments