Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango na Ujumbe kutoka Serikali ya Denmark ukiongozwa na Waziri wa Nchi-Sera, Bw. Martin Hermann, walipokutana kwa mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, Mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nchi anayehusika na masuala ya Sera, Bw. Martin Hermann (kulia) akiwa na ujumbe wake wakati wa mazungumzo kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (hayupo pichani), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam, ambapo nchi hizo zimekubaliana kuendeleza ushirikiano utakaojikita katika masuala ya uwekezaji na biashara kwa faida ya pande zote mbili. Kushoto ni Balozi wa Denmark hapa nchini Bw. Einar Jansen.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto), akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na ujumbe kutoka nchini Denmark, ukiongozwa na Waziri wa nchi anayeshughulikia Sera, Bw. Martin Hermann, (hayupo Pichani) walipokutana Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James, wakifuatilia kwa umakini mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Waziri wa Nchi anayeshughulika na masuala ya Sera wa Denmark, Bw. Martin Hermann (hawapo pichani), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nchi anayehusika na masuala ya Sera kutoka Denmark, Bw. Martin Hermann (kushoto) akimkabidhi Dkt. Mpango, nyaraka za kampuni zinazoonesha nia ya kuwekeza Tanzania katika Sekta ya Gesi na Mafuta wakati akiongoza ujumbe wa nchi hiyo katika mazungumzo kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kulia), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (katikati) akiangalia nyaraka alizokabidhiwa na Waziri wa Nchi wa Serikali ya Denmark anayehusika na Sera, Bw. Martin Hermann, wakati wa mazungumzo kati yao yaliyojikita katika masuala ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James na kulia kwa Waziri Dkt. Mpango, ni Naibu Katibu Mkuu Dkt. Khatib Kazungu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa pili kushoto) akiwa na wageni wake kutoka Serikali ya Denmark wakiongozwa na Waziri wa Nchi anayehusika na Sera, Bw. Martin Hermann (kushoto), baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati yao ambapo masuala kadhaa yamejadiliwa ikiwemo kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kijamii hususan katika uwekezaji na biashara, mazungungo yaliyofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto) akipeana mkono wa shukurani na mgeni wake kutoka Serikali ya Denmark, Waziri wa Nchi anayehusika na Sera, Bw. Martin Hermann (kushoto), baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati yao yaliyogusa Nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii hususan katika uwekezaji na biashara, mazungunzo yaliyofanyika makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto) akiwasindikiza wageni wake kutoka nje ya jengo la Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya ujumbe wa Serikali ya Denmark na Tanzania uliolenga kuimarisha uhusiano katika masuala ya uwekezaji na biashara.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM)
....................................................................
Na Benny Mwaipaja,
WFM, Dar es salaam
SERIKALI ya Denmark
imeahidi kuwashawishi wawekezaji wakubwa kutoka nchini humo kuja kuwekeza hapa
nchini katika sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Viwanda, Bandari, Gesi na Mafuta.
Ahadi hiyo
imetolewa Jijini Dar es salaam na Waziri wa Nchi wa Serikali ya Denmark
anayeshughulikia Sera, Bw. Martin Hermann, alipokutana na kufanya mazungumzo na
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Makao Makuu ya Wizara hiyo.
Bw. Hermann alielezea
kufurahishwa kwake na namna Serikali ya Awamu ya Tano ilivyojipanga kuwatumikia
wananchi wake kwa kuwaletea maendeleo ya haraka ya kiuchumi pamoja na
kuimarisha uwajibikaji, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, na kusema kuwa
nchi yake inaunga mkono juhudi hizo.
Alisema kuwa nchi
yake itasaidia juhudi hizo kwa kuzishawishi kampuni kubwa zenye mitaji na uwezo
wa kiteknolojia kutoka sekta binafsi ili zije ziwekeze hapa nchini na hivyo
kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi.
Amesisitiza pia umuhimu
wa serikali kuwekeza juhudi kubwa katika kuendeleza kilimo kwa kuwa sekta hiyo
inaweza kuchochea na kutoa mchango mkubwa na wa haraka wa ustawi na maendeleo
ya wananchi.
Aidha, Bw.
Hermann, ambaye aliambatana na Balozi wa Denmark hapa nchini, Bw. Einar Jensen,
amesifu utendaji mzuri wa Rais Mhe. Dkt. John Magufuli katika mapambano dhidi
ya vitendo vya ufisadi ikiwemo rushwa na kuishauri Serikali kuweka mfumo wa
vita hiyo utakaokuwa endelevu.
Kwa upande wake
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alisema Serikali inathamini
mchango mkubwa wa Denmark katika kukuza uchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla
kwa kusaidia miradi ya maendeleo na ushauri wa kisera.
“Katika kipindi
cha zaidi ya miaka 50 ya uhusiano kati ya nchi hizi mbili tumeshuhudia Serikali
ya Denmark ikichangia maendeleo yetu katika nyanja zinazokwenda sambamba na
vipaumbele vya maono ya mipango yetu ya maendeleo katika sekta za fedha,
miundombinu, kilimo, afya na elimu”alisisitiza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango aliishauri
nchi hiyo kwamba mwelekeo wa uhusiano huo sasa uwe katika kushirikiana kiuchumi
kwa kuhamasisha uwekezaji na biashara kati ya pande hizo mbili.
Alifafanua kuwa
amejaribu kutafuta takwimu za kiwango cha uagizaji na uingizaji wa bidhaa kati
ya Tanzania na Denmark lakini cha kusikitisha hakuna biashara hiyo jambo ambalo
amesema inabidi lilisisitizwe katika mfumo mpya wa ushirikiano kwa kuwa kuna
fursa nyingi zinazoweza kusaidia pande zote mbili kiuchumi.
Alisisitiza kuwa
mwelekeo huo ni muhimu utiliwe mkazo sambamba na jitihada za Serikali za
kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini huku akitoa
wito kwa kampuni za Denmark zilizopo hapa nchini pia kuvuta kampuni nyingine
kutoka nchini mwao kuja kuwekeza Tanzania.
Dkt. Mpango, amewakaribisha
wawekezaji hao kuwekeza katika katika sekta za ufugaji wa samaki, ujenzi wa
viwanda vya kuchakata samaki, ufugaji wa ng’ombe wa kisasa na viwanda vya
kusindika nyama na maziwa, hatua itakayo saidia kukuza mitaji, kuongeza tija
katika sekta hizo na ajira kwa kundi kubwa la vijana.
Kuhusu ushauri
uliotolewa na Waziri wa nchi wa Denmark anaye shughulikia Sera, Bw. Martin
Hermann wa kujenga mfumo endelevu wa kupambana na rushwa na ufisadi, Dkt.
Mpango amesema kuwa Serikali imeanzisha mahakama maalumu ya mafisadi ambayo
anaamini ni moja ya ujenzi wa mifumo hiyo endelevu ya kupambana na vitendo
hivyo.
0 Comments