Mtumishi wa Umma atakayeshindwa kuwasilisha
cheti cha elimu na taaluma au “Index
number” ya mtihani ili zihakikiwe na Baraza
la Mitihani la Taifa (NECTA), itakapofika tarehe 1 Machi, 2017atakua kajiondoa
kazini mwenyewe.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J.
Kairuki (Mb) alibainisha hayo
mwishoni mwa wiki wakati akifungua mkutano wa Watendaji Wakuu wa Wakala za
Serikali jijini Dar es salaam.
“Watendaji Wakuu ninawaomba msimamie uhakiki wa
vyeti ili watumishi wenu wafanye kazi kwa sifa stahiki” Waziri Kairuki
alisisitiza.
Aliongeza Serikali ilisitisha ajira mpya ili
kupisha zoezi la kuondoa Watumishi hewa, zoezi ambalo limefika ukingoni na siku
za karibuni ajira zitarudishwa.
Waziri Kairuki aliwataka Watendaji Wakuu kuweka
mikakati ya kuepuka watumishi hewa na kusimamia kwa dhati kwasababu jambo hilo
limeumiza na kupoteza rasilimalifedha nyingi za Serikali.
Alisema anatambua kuna Wakala zenye upungufu wa
Watumishi hivyo zinaingia gharama kubwa za kuajiri wafanyakazi wa mikataba,
hata hivyo alielekeza kila Mtendaji Mkuu ajiridhishe kwa kuandaa taarifa ya
mahitaji halisi ya Watumishi.
Waziri Kairuki, pamoja na hilo alielekeza
Wakala zenye Watumishi wa mikataba zifanye tathmini na kuhakiki kama kweli watumishi
hao wanahitajika kwa kuwa eneo hilo ni moja ya maeneo yenye ajira za mashaka
kwa baadhi ya Taasisi.
Waziri Kairuki aliongeza kuwa yapo malalamiko
kuhusu suala la maadili na uwajibikaji yanayozigusa Wakala za Serikali.
Aliainisha masuala hayo ni pamoja na Watumishi hewa, taarifa chafu za
Watumishi, matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za Umma, kutosimamia
ipasavyo utekelezaji wa mifumo ya utendaji kazi na wakati mwingine kutotekeleza
majukumu ya msingi ya wakala.
Alifafanua kuwa amegundua kupitia taarifa
mbalimbali kuwepo kwa changamoto ya
mawasiliano hafifu kati ya Wizara mama na Wakala zilizo chini yao ambapo
taarifa kutoka katika Wakala hazichambuliwi inavyostahili na hata
zinapochambuliwa na wizara mama, hazitoa mrejesho kwenda katika Wakala.
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi Dkt.
Laurean Ndumbaro alizitaka Wakala za Serikali kuimarisha eneo la ufuatiliaji na
tathmini ili kuimarisha utendaji kazi na kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na
Watanzania.
Alisema
matarajio ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha Wakala za Serikali zinapunguza
utegemezi kwa Serikali kwa kujitegemea kimapato kutokana na vyanzo vyake vya
ndani hasa kwa Wakala zinazoingiza mapato makubwa kutokana na huduma zinazotoa.
Serikali ilianzisha Wakala kwa lengo la
kuzifanya vyombo vya kutekeleza majukumu kwa niaba ya Serikali kwa tija na
ufanisi zaidi, pia kupunguza urasimu na hivyo kutoa huduma bora kwa wakati kwa
wananchi.
Imetolewa na Kitengo cha
Mawasiliano, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

0 Comments