Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Jumatatu Januari mbili, 2017 amemaliza ziara yake ya
siku mbili Mkoani Kagera kwa kuwatembelea baadhi ya wananchi walioathiriwa na
tetemeko la ardhi pamoja na kukagua baadhi ya miundo mbinu iliyoathiriwa na
tetemeko hilo na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo ya shule ya
sekondari ya Ihungo Omumwani iliyobomolewa
na tetemeko la ardhi la Septemba 10,2016.
Mara baada ya
ukaguzi huo Rais Dkt Magufuli akazungumza na wananchi wa Mkoa huo wa Kagera
katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ihungo na kuagiza kuvunjwa kwa kamati
ya maafa ya Mkoa huo iliyokuwa ikiratibu utoaji wa misaaada na kufanya tathmini
ya athari ya tetemeko hilo.
''Kila kitu huwa
kina mwanzo na mwisho wake ukiwa na harusi huwa kuna kamati ya
harusi,ukishamaliza kufunga ndoa kamati ya harusi huwa inavunjwa,na ukiwa
kwenye msiba huwa kuna kamati ya msiba na msiba mkishazika kamati ya mazishi huvunjwa,kamati
ya maafa ya Kagera huu ni mwezi wa tano na inawezekana hata kwenye kamati huwa
wanalipana posho,sasa nataka hii kamati nayo iishe,yalishapita yamepita''
Aidha Dkt Magufuli
amewataka wote walioahidi kuchangia katika kamati ya tetemeko la ardhi ya mkoa
wa Kagera ambao bado hawajatekeleza ahadi zao ambazo ni jumla ya shilingi
bilioni nne nukta tano wakamilishe ahadi hizo ili ziweze kumalizia miundombinu
ya Serikali iliyoathiriwa na tetemeko hilo.
Ameongeza kuwa
wale wote wanaoendelea kuguswa kusaidia wapeleke michango yao moja kwa moja kwa
wananchi badala ya kuipeleka serikalini kwa kuwa hakuna mchango mwingine
utakaopokelewa katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Pia Rais Dkt
Magufuli ameagiza shule ya Sekondari ya Omumwani iliyokuwa inamilikiwa na Jumuia
ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi CCM imilikiwe na Serikali kutaka wanafunzi
wote wanaosoma katika shule hiyo kutolipa ada kama zilivyo shule nyingine za
serikali.
Dkt Magufuli
ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kagera kupunguza utitiri wa kodi katika zao la
kahawa ili bei ya zao hilo ipande na kuwanufaisha wakulima
Balozi wa
Uingereza hapa Nchini Bi Sarah Cooke ambaye nchi yake imechangia kiasi cha shilingi
bilioni sita kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Ihungo, amempongeza
Rais Dkt Magufuli na serikali yake kwa jitihada za kupambana na rushwa suala
ambalo nchi yake ya Uingereza inalipa kipaumbele sambamba na kutoa elimu bila
malipo jambo linalowawezesha watoto wengi wa kitanzania kupata elimu bure
Jaffar
Haniu
Naibu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kagera.
02 Januari,
2017
0 Comments