Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil
Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya
Uhuru, Mzalendo na Burudani kutokana na kifo cha Mwanahabari za
michezo, Amina Athumani.
Katika salamu hizo ambazo pia zimekwenda kwa Mwenyekiti wa Chama cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Juma Pinto; Rais
Malinzi ameelezea kushtushwa kwake kwa taarifa za kifo cha ghafla cha
Amina Athumani.
“Niseme tu wazi kuwa tangu kuanza kwa michuano ya mapinduzi, nimekuwa
nikifuatilia taarifa mbalimbali zinazotolewa na wanahabari. Huwa pia
sikosi magazeti ya Uhuru na Mzalendo na kuona byline (jina la mwandishi)
ya Amina. Mpaka matokeo ya fainali zilizofanyika Januari 13, mwaka huu.
“Sasa asubuhi hii nimepata taarifa za kifo chake, ama kwa hakika
zinasikitisha. Ni kifo cha ghafla, ninavyomfahamu binti huyo ni
mchapakazi hodari, na mfano uko wazi kwani katika hali ya ujauzito
alikuwa hakosi kufuatilia habari,” amesema Rais Malinzi.
Kadhalika, Rais Malinzi ametuma salamu hizo za rambirambi kwa familia
ya marehemu Amina Athumani, ndugu, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa
na moyo wa subira wakati huu mgumu wa msiba wa mpendwa wao.
“Binafsi naona ni kama askari Jeshi aliyefia vitani. Naweza kumwita
ni shujaa, lakini ndiyo hivyo tena, huwezi kupingana na mipango ya
Mungu, nimepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa, naomba wenzangu
pia muwe na subira wakati huu mgumu ambao tasnia na Kampuni ya Uhuru
Publications imepoteza mwanahabari mahiri.
Taarifa zinasema Amina alifariki dunia leo Jumapili Januari 15, 2017
akiwa anapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Mnazimmoja, iliyoko
Zanzibar mara baada ya kujifungua jana kwa mtoto ambaye pia alifariki
muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Hadi mauti yanamkuta alikuwa Mwandishi wa magazeti ya Uhuru na
Mzalendo pamoja na gazeti la Burudani linalochapisha mahsusi habari za
michezo na sanaa. Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya marehemu Amina
Athumani mahala pema peponi.
Inna Lillah wa Innaa Ilaihi Rajaajiuun.
Sote wa Mwenyezi Mungu, na kwake tutarejea.
..…………………………………………………………………………..............
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment