Meneja
wa Karakana ya Dar es Salaaam ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia
(TAZARA), Eng. Timothy Kayani, akimwonyesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa vipuri vya treni vilivyotengenezwa katika
karakana hiyo jijini Dar es Salaam, alipotembelea karakana ya Mamlaka hiyo kuona
utendaji wake.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akimsikiliza mmoja wa
wataalam wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), akimweleza namna wanavyosimamia mafuta yanayotumika kwenye
treni za Mamlaka hiyo, alipowatembelea jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akiangalia behewa la
treni lililofanyiwa ukarabati na kukamilika katika karakana ya Mamlaka ya Reli
ya Tanzania na Zambia (TAZARA), alipotembelea karakana hiyo jijini Dar es
Salaam.
Meneja
wa Karakana ya Reli Dar es Salaaam ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia
(TAZARA), Eng. Timothy Kayani, akifafanua namna behewa la treni linavyoanza
kufanyiwa ukarabati kwa Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto) katika
karakana hiyo, wakati Waziri huyo alipotembelea kuona utendaji wake. Wa pili
kushoto ni Meneja wa TAZARA Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Fuad Abdalla.
Mtaalam
wa mifumo ya Tehama wa Kampuni ya Qmax Bi. Jenirose Jabakila akimweleza Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, namna mfumo
walioutengeneza wa kufatilia treni inapokuwa njiani unavyofanya kazi, wakati
alipotembea Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa
wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), alipotembelea
mamlaka hiyo kuona utendaji kazi.
Picha
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.
..............................................................................................
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa
Makame Mbarawa amesema Serikali haitamvumilia mtumishi
yoyote ambaye ataendelea kuisababishia hasara Mamlaka ya Reli ya Tanzania na
Zambia (TAZARA) kwa kuendelea kuihujumu na kusababisha mamlaka kujiendesha kwa
hasara.
Profesa Mbarawa
ameyasema hayo leo wakati alipotembelea Tazara, kuangalia utendaji ambapo
amebaini matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na Serikali na kuahidi kuchukua
hatua stahiki.
“Ninafahamu kuna watu
10 hapa ambao wao ni chanzo kikubwa cha matumizi mabaya ya fedha na miongoni
mwao wapo Watanzania na Wazambia, nawahakikishia kuwa kila atakayetumia vibaya
fedha zinazotolewa na Serikali hatutamvumilia kwenye Serikali hii’, amesema
Prof. Mbarawa.
Profesa Mbarawa
amesema kumekuwa na idadi kubwa ya watumishi ambao hawana tija na kuagiza menejimenti ifanye uhakiki na
kubaini mahitaji halisi ya Watumishi na watakaobainika kuzidi wahamishiwe ofisi
ya tazara Mkoa wa Dar es Salaam.
Aidha Prof. Mbarawa
ameuagiza uongozi wa Tazara Makao Makuu kuacha mara moja kutumia mtandao ya
kampuni binafsi kutuma taarifa za Ofisi na kuagiza kuanza kutumia mtandao wa Kampuni
ya Simu Tanzania (TTCL) mara moja.
‘Nikirudi tena hapa
sitaki kuona mnatumia mitandao wa Kampuni binafsi kutuma taarifa za kiofisi
ninawaomba muhakikishe mnatumia mtandao
wa TTCL’ amesisitiza Prof. Mbarawa.
Kwa upande Meneja wa
TAZARA Mkoa wa Tanzania, Bw. Fuad Abdalla amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa
kuwa mkoa umejipanga vizuri kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa na Mamlaka
inajiendesha kibiashara.
‘Kama mkoa tumekuja na
mikakati mizuri ya kutumia mifumo ya Tehama kama njia ya udhibiti wa mapato, kama ulivyona hivi sasa
tunakamilisha mfumo wa Tehama tunaoutumia kufatilia treni kila inapoondoka
kwenye Stesheni ya Makao Makuu Dar es Salaam na mfumo huu ukikamilika
tutawaashawishi na wenzetu wa Zambia kutumia mfumo huu ili tuweze kudhibiti
upotevu wa mapato’ Amesisitiza Bw. Fuad Abdalla.
Bw. Fuad ameongeza
kuwa pamoja na mifumo mipya ya Tehama Tazara inaendeleza kwa kasi ukarabati wa
mabehewa ya abiria na mizigo ili kuongeza tija na kuiwezesha Mamlaka kupata
faida.






0 Comments