Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa Manispaa ya
Kigamboni jijini Dar es salaam akiwa katika ziara ya wialaya ya
Kigamboni Januari 3, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wa wialya ya
Kigamboni baada ya kuwasili wilayani humo kwa ziara ya siku moja.
.............................................................................................................
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha fedha
zote zilizotengwa kwa ajili ya posho mbalimbali zisizokuwa za kisheria
zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.
Ametia agizo hilo leo
(Jumanne, Januari 3, 20017) wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya
Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.
“Kuanzia sasa marufuku Wakurugenzi
kutoa posho zisizotambulika kisheria zikiwemo za mazingira magumu, kujenga
uwezo na vitafunwa katika halmashauri zenu na badala yake fedha hizo zitumike
kwenye miradi ya maendeleo,” amesema.
Agizo hilo litawezesha
Jiji la Dar es Salaam kuokoa sh bilioni 130 zilizokuwa zitumike na Halmashauri
na Manispaa za jiji hilo, ambazo kwa sasa zitaingizwa kwenye miradi na shughuli
za maendeleo.
Aidha, Waziri Mkuu
amewataka watumishi wa umma nchini kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuacha kutumia
fedha kinyume cha utaratibu na watakaobainika Serikali haitosita kuwachukulia
hatua kali za kisheria.
“Katika halmashauri zetu
kila mtumishi anashiriki katika ukusanyaji wa mapato hadi walinzi, lakini
mwisho wa siku vitafunwa huliwa na wachache wanaojiita wakubwa huku wengine
wakisikilizia kwa nje. Jambo hili haliwezekani,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesisitiza
kwamba Mkurugenzi yeyote atakayebainika kulipa posho hizo baada ya siku ya
leo atakuwa amejifukuzisha kazi.
Aidha, ameagiza fedha
zilizokuwa zikitolewa kwa madiwani kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo
zisitolewe moja kwa moja kwa madiwani na badala yake zipelekwe kwenye kata husika na zifuatiliwe
matumizi yake.
Hata hivyo, Waziri Mkuu
amezionya halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa kila fedha zinayopelekwa
kwenye halmashauri hizo inatumika kama ilivyokusudiwa na atakayebainika kutumia
kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Pia amewataka watumishi
wote wa umma nchini kuwajibika ipasavyo na kuhakikisha wanawatumikia vyema
mwananchi ikiwa ni pamoja na kuepuka vishawishi na kujiingiza kwenye vitendo
vya rushwa na ufisadi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa siku tatu kwa watumishi 10 wa halmashauri
hiyo ambao wamehamishiwa kutoka wilaya ya Temeke wawe wameripoti katika
Manispaa hiyo, vinginevyo watakuwa wamejifukuzisha kazi.
Awali Mkuu wa Wilaya ya
Kigamboni Bw. Hashim Mgandilwa wakati akiwasilisha taarifa ya wilaya hiyo kwa
Waziri Mkuu, alisema hadi sasa asilimia 98 ya watumishi waliotakiwa kuhamia
kwenye halmashauri hiyo wameripoti isipokuwa 10 na hakuna taarifa zozote juu
yao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
JUMANNE, JANUARI 3, 2017


0 Comments