![]() |
JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA NISHATI NA MADINI
|
TAARIFA
KWA UMMA
ZOEZI
LA UOKOAJI WACHIMBAJI 15 WALIOFUKIWA NA KIFUSI KATIKA MGODI WA DHAHABU GEITA LAKAMILIKA
KWA MAFANIKIO
Wizara ya Nishati na Madini inapenda
kuufahamisha umma kuwa, Zoezi la
kuwaokoa wachimbaji 15 waliofukiwa na kifusi
tarehe 26/01/2017 kwenye mgodi wa dhahabu eneo la kijiji cha Mawemeru,
Nyarugusu Wilayani Geita limekamilika kwa mafanikio.
Ajali ya kufukiwa wachimbaji hao
iliyohusisha Watanzania 14 na raia 1 wa China ilitokea kwenye leseni ya
uchimbaji wa Kati wa madini ya dhahabu yenye Namba ML 492/2013 inayomilikiwa na
Bw. Ahmed Mubarak Adam.
Chanzo cha ajali hiyo ilikuwa ni
kuanguka kwa shaft ya mgodi huo na
kufukiwa na kifusi wakati wachimbaji hao wakifanya kazi mgodini chini ya ardhi.
Tukio la uokoaji limefanikiwa leo
tarehe 29/01/2017 ambapo wahanga hao walianza kutolewa shimoni kuanzia saa 5
hadi saa 5:30 asubuhi wote 15 wakiwa hai ingawa walikuwa wamedhoofika kiafya. Aidha, wachimbaji hao wamepewa huduma ya
kwanza katika eneo la ajali na kisha kukimbizwa Hospitali Teule ya Rufaa ya
Geita. Hadi sasa wachimbaji hao wapo Hospitali wakiendelea na matibabu kwa
uchunguzi zaidi wa afya zao.
Juhudi za kuokoa wachimbaji hao ambazo zilifanyika kwa kufukua kifusi katika
eneo la ajali zilianza mara baada ya tukio hilo kutokea. Uongozi wa Mkoa wa
Geita ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa Meja. Jen.(Mst) Ezekiel E. Kyunga
ulishirikiana na Wataalam wa Wizara ya Nishati na Madini na Kampuni za Madini
mbalimbali mkoani Geita katika zoezi la ufukuaji kifusi ili kuokoa maisha ya
wchimbaji hao.
Kampuni zilizoshiriki kwa kutoa
mitambo na vifaa mbalimbali ni Kampuni ya Busolwa
Mining Ltd; Kampuni ya Geita Gold
Mine (GGM); Kampuni ya Nyarugusu
Mining Ltd; Nsangano Mining Project; Metchell
Tanzania Drilling; WAJA Hospital pamoja
na wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Geita wakiongozwa na Viongozi wa wachimbaji
madini Wilaya, Mkoa na Taifa.
Akizungumza mara baada ya kuokolewa
wachimbaji hao, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard amewashukuru
wadau wote walioshiriki kwa hali na mali kufukua kifusi na hatimaye kufanikiwa
kuwatoa wachimbaji chini ya ardhi wakiwa hai.
Dkt. Kalemani amewaomba Watanzania
kuendelea na moyo huo pale majanga kama haya yanapotokea. Aidha, Dkt. Kalemani ameagiza
shughuli zifungwe kwa muda wa siku tano kwenye mgodi uliopata ajali kuanzia
tarehe 29/01/2017 ili kutoa nafasi kwa Kamishna wa Madini kufanya tathmini ya hali
ya usalama wa mgodi na kutoa maelekezo kabla ya shughuli kuanza.
Vilevile, amewataka wachimbaji wawe
watulivu katika kipindi ambacho tathmini ya hali ya usalama wa mgodi inafanyika
na kuagiza Uongozi wa Mkoa kuhakikisha kuwa ulinzi unaimarishwa eneo la mgodi
ili watu wasiweze kuingia na kuhatarisha maisha yao.
Pia, ameagiza ukaguzi wa kina ufanyike
kwenye migodi mingine ya wachimbaji wadogo na ya kati eneo la Nyarugusu na
kwingineko nchini ili kuhakikisha kuwa migodi inakuwa salama kwa wachimbaji wa
migodi husika.
Imetolewa na;
KATIBU
MKUU
WIZARA
YA NISHATI NA MADINI
29/1/2017


0 Comments