Na.
Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Serikali
itaendelea kutoruhusu uvuvi kufanyika ndani ya Pori la Akiba la Selous kutokana
na ukiukwaji wa taratibu zilizokuwa zimewekwa wa kuingia ndani ya hifadhi hiyo.
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Makani ameyasema hayo leo Bungeni,
Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Rufiji Mohamed Mchengerwa juu
ya hatua ambazo Serikali inazichukua kutoa ridhaa kwa wananchi waishio maeneo
ya hifadhi kupata ruhusa kisheria kuweza kuvua samaki.
“Mwaka
1994, wananchi wa Kata ya Mwaseni, Mloka, Ngoroka na Kipungila Wilaya ya Rufiji
waliruhusiwa kuingia ndani ya Pori la Akiba Selous na kuvua Samaki. Hata hivyo,
baadhi ya wanavijiji walikiuka taratibu zilizokuwa zimewekwa kwa kuingia ndani
ya hifadhi bila kujiandikisha na kuvua samaki kinyume cha sheria,” alifafanua
Mhandisi Makani.
Aliendelea
kwa kusema kuwa baadhi ya wavuvi walibainika kujihusisha na vitendo vya
ujangili wa wanyamapori, uvuvi haramu wa kutumia sumu, ukataji miti ovyo kwa
ajili ya kukausha samaki na kutengeneza mitumbwi pamoja na uharibifu wa
mazingira uliotokana na uchomaji wa moto ovyo kinyume cha sheria.
Mhandisi
Makani amesema kuwa kwa kuzingatia hali ya usalama katika maeneo ya uhifadhi wa
wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kutoruhusu uvuvi
kufanyika ndani ya Pori la Akiba Selous.
Aidha
Wizara inawashauri wananchi wa Kata za Mwaseni, Mloka na nyinginezo zilizo
jirani kutumia mabwawa mengine yaliyoko nje ya Pori hilo yenye fursa kubwa kwa
kufanya shughuli za uvuvi.
Mabwawa
ambayo wananchi wameshauriwa kuyatumia ni Bwawa la Zumbi lililoko vijiji vya
Nyaminywili, Kipugira na Kipo, Bwawa la Ruwe lililopo Mkongo, Lugongo lililopo
kijiji cha Mtanza na Bwawa la Zimbwini lililopo Mji wa Kibiti.
Mabwawa
hayo ya Mto Rufiji yatatoa fursa ya shughuli za uvuvi hivyo kusaidia kuinua
kipato cha wananchi.
Vile
vile Mhandisi Makani amesema kuwa, Wizara hiyo kwa kutambua mahitaji ya
wananchi katika maeneo hayo ya kufanyia kazi na kujiletea maendeleo kiuchumi na
kijamii. Wizara hiyo inaendelea kushauriana na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji
kuhusu namna ya kutekeleza mpango wa kuwajengea mabwawa ya samaki ili pamoja na
mabwawa ya asili yaliyopo yawawezeshe kufanya shughuli za uvuvi endelevu.

0 Comments