Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasikiliza Mawaziri wa Nishati kutoka Tanzania na Zambia wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya Tathmini ya Ujenzi wa Bomba jipya la Mafuta Safi kutoka Tanzania hadi Zambia. Kulia ni Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo na kushoto ni Waziri wa Nishati wa Zambia, David Mabumba, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) na Ujumbe alioambatana nao wakati wa kuwasilisha taarifa ya Tathmini ya Ujenzi wa Bomba jipya la Mafuta Safi kutoka Tanzania hadi Zambia. Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa, Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Balozi Grace Mujuma na Kaimu Kamishna wa Nishati Tanzania, Mhandisi Innocent Luoga.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) na Waziri wa Nishati wa Zambia, David Mabumba (kushoto) mara baada ya kuwasilisha taarifa ya Tathmini ya Ujenzi wa Bomba Jipya la Mafuta Safi kwa Makamu wa Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waziri wa Nishati wa Zambia, David Mabumba (kushoto) mara baada ya kupokea taarifa ya tathmini ya ujenzi wa Bomba jipya la Mafuta Safi la litakaloanzia Dar es Salaam, Tanzania hadi Ndola, Zambia. Kulia ni Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Tanzania na Zambia ambao ulifika kuwasilisha taarifa ya tathmini ya ujenzi wa Bomba jipya la Mafuta Safi litakalotoka Dar es Salaam, Tanzania hadi Ndola, Zambia. Ujumbe huo uliongozwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Nishati wa Zambia, David Mabumba.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akifurahia jambo na Waziri wa Nishati wa Zambia David Mabumba (kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Zambia,Brigedia Jenerali Emelda Chola (katikati) mara baada ya kuwasilisha taarifa ya tathmini ya ujenzi wa Bomba jipya la Mafuta Safi litakalotoka Dar es Salaam, Tanzania hadi Ndola, Zambia.
..................................................................
Serikali ya Zambia imehakikishiwa ushirikiano wa kutosha kwenye ujenzi wa Bomba jipya la Kusafirisha Mafuta Safi kutoka Tanzania hadi Zambia unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Hayo yameelezwa hivi karibuni Ikulu, Jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya tathmini ya ujenzi wa bomba hilo kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Nishati wa Zambia, David Mabumba.
Makamu wa Rais alipongeza wazo hilo la ujenzi wa Bomba la Mafuta Safi na kueleza kwamba manufaa yatakayopatikana kutokana na ujenzi wa bomba hilo ni makubwa kwa nchi zote mbili na hivyo kuihakikishia Serikali ya Zambia ushirikiano wa dhati katika utekelezaji wake. “Nimefurahishwa na wazo hili na ninawahakikishia tupo pamoja,” alisema.
Alisema Tanzania imekuwa na mahusiano ya muda mrefu na Zambia kupitia maeneo mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili kupitia Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la TAZAMA pamoja na Reli ya TAZARA.
“Mbali na manufaa ya kiuchumi yatakayopatikana mara baada ya kukamilika kwa Bomba hili jipya lakini pia ni namna mojawapo ya kuzidi kuimarisha mahusiano yetu ambayo yana historia ndefu,” alisema.
Aliagiza maandalizi ya ujenzi wa Bomba hilo yaanze haraka iwezekanavyo ili likamilike katika kipindi kifupi na kuchangia kukua kwa uchumi wa nchi zote mbili.
Kwa upande wake, Waziri Muhongo alielezea faida mbalimbali zitakazopatikana kutokana na ujenzi wa Bomba hilo jipya la Kusafirisha Mafuta Safi ikiwa ni pamoja na kunufaika kwa maeneo mbalimbali yatakayopitiwa.
Vilevile alielezea kuhusiana na ziara aliyoifanya ya kutembelea njia nzima ya Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la TAZAMA na Vituo vya Kusukuma mafuta hayo (pumping stations) kwa kushirikiana na Waziri mwenza wa Nishati wa Zambia, Mulumba David.
Alimweleza Makamu wa Rais kuhusiana na umuhimu wa kufanya mabadiliko ya teknolojia na mitambo ya kusukuma mafuta ambayo alisema ilifungwa Mwaka 1968.
Naye Waziri David, alimweleza Makamu wa Rais kuwa huko Zambia, kwa sasa mafuta yana gharama kubwa ikilinganishwa na nchi nyingine barani Afrika na kutaja kuzorota kwa utendaji kazi wa TAZAMA kuwa ni mojawapo ya sababu zilizosababisha hali hiyo.
Alisema mahitaji ya mafuta nchini humo kwa sasa ni lita za ujazo tani milioni 1.2 na kwamba Bomba hilo linasafirisha chini ya uwezo wake jambo ambalo linachangia mafuta hayo kupanda bei.
“Kama Mafuta yangekuwa yanaingia mengi nchini, gharama ingepungua; lengo letu ni kuhakikisha mafuta yanakuwa mengi ili wananchi wapate unafuu wa maisha,” alisema.
Aliongeza kuwa ifikapo Mwaka 2030, mahitaji ya mafuta nchini Zambia yanatarajiwa kufikia lita za ujazo tani milioni 4 kwa mwaka na kwa sababu hiyo, uwekezaji mkubwa kwenye sekta husika nchini humo unahitajika ili kukidhi mahitaji hayo.
Kikao hicho cha Makamu wa Rais na Mawaziri hao na Ujumbe waliombatana nao kutoka pande zote mbili kinafuatia ziara yao ya siku Nne ya kutembelea njia ya Bomba la TAZAMA pamoja na Vituo vya Kusukuma Mafuta na kufanya tathmini ya ujenzi wa Bomba jipya la Kusafirisha Mafuta Safi waliyofanya kuanzia jijini Ndola, Zambia na kumalizia jijini Dar es salaam.
Aidha, ziara hiyo ni kufuatia makubaliano ya marais wa nchi husika, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mhe. Edgar Lungu ya Novemba 28, 2016 kuhusu kuboresha Bomba hilo la TAZAMA kwa manufaa ya nchi zote mbili pamoja na pendekezo la ujenzi wa Bomba jipya la kusafirisha Mafuta Safi lililotolewa na Rais Lungu.
Bomba la kusafirisha Mafuta Ghafi la TAZAMA linaloanzia nchini Tanzania hadi mji wa Ndola nchini Zambia lina urefu wa kilomita 1,710 na kipenyo cha inchi 8 hadi 12 na lilianza kazi Mwaka 1968.






0 Comments