Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na wananchi na wageni waalikwa
katika uzinduzi wa kampeni ya uhamasishaji uzazi wa mpango uliofanyika Mkwajuni
Wilaya ya Kasakazi A Unguja.
Picha na
Makame Mshenga-Maelezo
Mwakilishi wa Shirika la Engender Health Dkt. Martha Kisanga akizungumza na
wananchi wa Wilaya ya Kaskazini A wakati wa uzinduzi wa kampeni maalumu ya uhamasishaji
wa uzazi wa mpango katika kijiji cha Mkwajuni.
Wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa kampeni maalum ya uzazi wa mpango
wakifuatilia uzinduzi huo uliofanyika Mkwajuni Wilaya ya Kaskazini A Unguja.
Baadhi ya watoto walioshiriki uzinduzi wa kampeni maalum ya kuwahamasisha
wazazi wao kujiunga na uzazi wa mpango wakifuatilia uzinduzi huo uliofanyika
kijiji cha Mkwajuni.
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akipata maelezo ya matumizi ya huduma za
uzazi wa mpango kutoka kwa mhamasishaji wa Shirika la Engender Health Joyce
Ishengoma alipotembelea banda la maonyesho wakati wa uzinduzi wa kampeni ya
kuhamasisha huduma hiyo iliyofanyika kijiji cha Mkwajuni Wilaya Kaskazini A.
..................................................................
Na Ramadhani
Ali/Maelezo
Zaidi ya
akinamama 236 kati ya laki moja wanaofika hospitali na vituo vya afya kujifungua
Zanzibar wanafariki kila mwaka kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo kuacha
kutumia huduma za uzazi wa mpango.
Kutokana na
tatizo hilo Wizara ya Afya imeanzisha kampeni maalum ya wiki moja ya
kuwahamasisha akina mama na akinababa kujiunga na uzazi wa mpango katika juhudi
za kuokoa maisha ya wazazi na watoto.
Waziri wa
Afya Mahmoud Thabit Kombo alizindua kampeni hiyo katika kijiji cha Mkwajuni
Wilaya ya Kaskazini ‘A’ na kuwashauri akinababa kuwaruhusu wake zao kujiunga na
uzazi wa mpango .
Alisema hidi
sasa wanawake wanaostahiki kujiunga na uzazi wa mpango Zanzibar ni asilimia 14 tu
waliojiunga na juhudi inatakiwa ifanywe ili iweze kufikia asilimia 20 ifikapo
mwaka 2020 ili kulinda afya ya mama na mtoto.
Waziri Mahmoud
alisema idadi ya akinamama wanaofariki ni kubwa zaidi ya takwimu zilizopo kwani
wanaojifungulia hospitali ni asilimia hamsini tu na asilimia iliyobaki
wanajifungulia majumbani na hakuna takwimu zao.
Aliongeza kuwa
Serikali imefanya juhudi kubwa za kusambaza huduma za uzazi wa mpango katika
vituo vyote vya afya mijini na vijijini ili kuwaondoshea usumbufu wananchi
hivyo amewashauri kuvitumia.
Akizungumzia
vifo vya watoto chini ya miaka mitano, Waziri wa Afya alisema bado ni tatizo kubwa
Zanzibar watoto 56 kati ya 1000 wanaozaliwa wakiwa hao hufariki dunia.
Alisema sababu
kubwa ya vifo hivyo inatokana na wazazi kucheleweshwa kupelekwa hospitali ama
kutopelekwa kabisa na kupelekea kujifungua katika mazingira yasiyo salama.
Kutokana na
matatizo mengi yanayowapata akinamama wajawazito na watoto wakati wa kujifungua
na baada ya kujifungua, Waziri Mahmoud Thabit Kombo ameagiza kuundwa Kamati ya
kitaifa itakayowashirikisha viongozi kutoka kada mbali mbali na washirika wa
maendeleo kukabiliana nalo.
Mwakilishi wa
Shirika la Engender Health Dkt. Martha Kisanga alisema ushiriki mdogo wa
akinababa katika huduma ya uzazi wa mpango unachangia wanawake wengi kutojiunga
na huduma hizo.
Katika risala
ya wananchi wa Wilaya Kaskazini A iliyosomwa na Tatu Khamis Kombo walisema
pamoja na vituo vingi vya afya kutoa huduma za uzazi wa mpango, mwamko bado ni
mdogo na kufanyika kwa kampeni hiyo katika wilaya yao itasaidia wananchi wengi
kujiunga.
Wilaya Kaskazini
A na Wilaya ya Micheweni Pemba ndizo zenye asilimia ndogo zaidi ya akinamama
waliojiunga na huduma ya uzazi wa mpango Zanzibar.
IMETOLEWA NA
MAELEZO ZANZIBAR





0 Comments